Wakati Taasisi ya Katiba Institute ikiadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, inaendelea kuuenzi mchango wa Profesa Yash Pal Ghai, mmoja wa watu waliokuwa na nafasi muhimu katika safari ndefu ya Kenya kuelekea kupitishwa kwa Katiba mpya ya mwaka 2010.
Maadhimisho hayo pia yanaendana na tarehe muhimu katika historia ya Kenya. Novemba 10, 2000, Ghai aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mapitio ya Katiba ya Kenya (CKRC), wakati ambapo wananchi walikuwa wakishinikiza mabadiliko ya kisiasa na kupatikana kwa Katiba mpya.
Ghai, ambaye ni mwanasheria na msomi anayeheshimika katika masuala ya Katiba, alikuwa na mchango mkubwa katika kuzikutanisha pamoja pande mbalimbali zilizokuwa zikishiriki mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Pande hizo zilijumuisha timu ya mapitio ya Katiba iliyoongozwa na Bunge pamoja na Ufungamano Initiative, iliyoundwa na taasisi za kidini na mashirika ya kiraia.
Moja ya michango yake muhimu ilikuwa kuhakikisha kwamba wananchi wa kawaida wanapata nafasi ya kutoa maoni kuhusu aina ya Katiba waliyotaka kwa nchi yao. Katika video iliyoshirikishwa na Katiba Institute wakati wa maadhimisho hayo, Ghai anakumbuka jinsi yeye na wajumbe wa tume walivyosafiri katika maeneo mbalimbali ya Kenya kusikiliza maoni ya wananchi. “Lakini safari hii, mimi sitazungumza, ninyi ndiyo mtazungumza,” anakumbuka akiwaambia wananchi. Hata hivyo, baadaye aligundua kuwa baadhi ya wananchi waliogopa kutoa maoni yao kwa uhuru, hasa pale maafisa wa polisi na viongozi wa serikali walipohudhuria mikutano hiyo.
Ghai anakumbuka jinsi mwananchi mmoja alivyomuuliza kama kweli walitarajiwa kuzungumza kwa uhuru wakati kulikuwa na afisa wa polisi kwenye mkutano. Baada ya hapo, aliwaomba maafisa hao kuwaachia wananchi nafasi ya kuzungumza bila uwepo wao, na hatua hiyo ilisaidia watu wengi zaidi kuanza kutoa maoni yao. “Nilitaka kuwaonyesha kwamba tunawaheshimu,” anasema Ghai.
Maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi yalichangia mchakato wa mapitio ya Katiba uliozaa Rasimu ya Katiba ya Bomas mwaka 2004. Ingawa tofauti za kisiasa zilichelewesha mabadiliko hayo, hatimaye Kenya ilipitisha Katiba mpya Agosti 2010, iliyoleta mabadiliko makubwa, yakiwemo ugatuzi wa madaraka kupitia serikali za kaunti, kuimarishwa kwa haki za msingi za wananchi na kuwekwa kwa mifumo ya kudhibiti matumizi ya madaraka ya serikali.
Mchango wa Ghai katika masuala ya Katiba hauishii Kenya pekee. Amefundisha sheria katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania, ambako alikuwa Mwafrika wa kwanza kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria. Pia ameshiriki katika michakato ya uandaaji na marekebisho ya Katiba katika nchi zaidi ya 20 duniani. Hata hivyo, hata baada ya Kenya kupitisha Katiba mpya, Ghai aliamini kuwa bado kulikuwa na kazi ya kufanya.
Mwaka 2011, kwa kushirikiana na msomi mwenzake wa sheria, Jill Cottrell Ghai, alianzisha Katiba Institute, huku Waikwa Wanyoike akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa taasisi hiyo. Wasiwasi wao ulikuwa kwamba kupitishwa kwa Katiba mpya hakukumaanisha moja kwa moja kuwa sheria na haki zilizowekwa ndani yake zingeheshimiwa na kutekelezwa. Miaka 15 baadaye, Katiba Institute inaendelea kutetea haki za kikatiba kupitia kesi zinazohusu maslahi ya umma, elimu kwa wananchi kuhusu Katiba, tafiti na juhudi za kuhakikisha taasisi za umma zinawajibika. Taasisi hiyo inaadhimisha miaka 15 kupitia kampeni ya mitandaoni inayoendelea kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 13, 2026, ikiwakumbuka watu waliochangia kuijenga na kutafakari kazi ambayo bado inahitaji kufanyika.
Mchango wa Ghai pia una mafunzo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania, ambako madai ya kupatikana kwa Katiba mpya yameendelea kwa miaka mingi.
Uzoefu wake nchini Kenya unaonyesha umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba, kusikiliza maoni yao na kuhakikisha kwamba mambo yanayoahidiwa katika Katiba mpya yanatekelezwa kwa vitendo.







