, , , , , , ,

Amnesty yaishutumu Tanzania kwa kutumia sheria dhidi ya ugaidi kunyamazisha wakosoaji

Victor Wanaswa Avatar

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeishutumu serikali ya Tanzania kwa kutumia sheria za kupambana na ugaidi kunyamazisha wakosoaji wake na kukandamiza uhuru wa raia, mwaka mmoja baada ya operesheni kali ya kukabiliana na maandamano yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, iliyosababisha vifo vya mamia ya watu na kuwajeruhi maelfu ya Watanazania.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, shirika hilo limesema hakuna afisa yeyote wa serikali aliyefunguliwa uchunguzi wa jinai au kufunguliwa mashtaka kuhusiana na matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyotekelezwa na vyombo vya usalama wakati wa maandamano hayo.

Amnesty imesema serikali ya Tanzania imeimarisha vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza na haki ya kufanya mikutano ya amani, huku waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu wakiendelea kukamatwa kiholela, kutekwa nyara, kupotezwa na kudhulumiwa.

“Hakuna hata afisa mmoja aliyechunguzwa kwa makosa ya jinai, kando na kufunguliwa mashtaka na kuadhibiwa, kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyofanywa na vyombo vya usalama vya Tanzania dhidi ya waandamanaji,” amesema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International anayesimamia ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Katika taarifa hiyo, Amnesty imesema mamlaka pia zimeficha matokeo ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi kuhusu mauaji yaliyohusishwa na uchaguzi, licha ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Aprili 2026.

Mwezi Agosti, Rais Samia alizindua tume nyingine iliyopewa jukumu la kubaini watu waliopanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza vitendo vya ghasia, kuchunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi na kubaini waliko watu waliopotea.

Amnesty imeitaka tume hiyo mpya kufanya uchunguzi huru, usioegemea upande wowote na ulio wazi kwa umma, ukiwemo uchunguzi kuhusu nafasi ya vyombo vya ndola katika ghasia hizo. Shirika hilo pia limetaka ripoti ya uchunguzi huo kuwekwa wazi mara baada ya kukamilika.

Aidha, shirika hilo limesema uchunguzi wake uliofanywa kati ya Septemba 3 na 17, 2026, kwa kuwahoji watu 17 wakiwemo waathiriwa, wanahabari, viongozi wa upinzani, mawakili na ndugu za waathiriwa, umebaini kuwa hali ya haki za binadamu nchini Tanzania inazidi kuzorota.

Kwa mujibu wa nyaraka za mashtaka zilizothibitishwa kuhusu watu waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, kisa kimoja kinamhusu Ibrahim Myovella, kiongozi wa vijana wa chama cha upinzani cha CHADEMA.

Myovella alitoweka pamoja na marafiki zake wawili Aprili 18, baada ya kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Iringa, kama walivyotakiwa kufanya chini ya masharti ya dhamana yao. Shirika hilo limesema watatu hao walikuwa wakituhumiwa kuhusika katika maandamano ya Oktoba 2025. Hata hivyo, mamlaka zilikana kufahamu waliko.

Taarifa hiyo pia imetaja kutekwa nyara kwa Mashaka Nestory Kindikwa, aliyekuwa afisa wa chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye inadaiwa alichukuliwa nyumbani kwake Juni 25 na wanaume saba wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama. Polisi pia walikanusha kumshikilia.

Katika kisa kingine, David Djumbe, msaidizi wa kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu, alidaiwa kutekwa karibu na nyumbani kwake jijini Dar es Salaam Mei 20 na kupigwa vikali na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama wa serikali ya Tanzania.

Yamkini Djumbe alifanikiwa kutoroka. Hata hivyo, Amnesty imesema hakuna taarifa zozote kuhusu uchunguzi wa polisi uliotangazwa baada ya tukio hilo.

Shirika hilo pia limenakili kuhusu madai ya kuteswa kwa mfuasi mmoja wa maandamano aliyekuwa kizuizini kwa siku 47 bila kufunguliwa mashtaka. Mwanamume huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Stefano Patrick, alisema waliomhoji walimpiga, wakamnyima chakula na maji na kutishia kumuua huku wakimtaka kutoa habari kuhusu watu waliokuwa wakifadhili maandamano hayo.

Kwa mujibu wa Amnesty, matumizi mabaya ya sheria za kupambana na ugaidi kuwalenga wafuasi wa upinzani na wakosoaji wengine wa serikali yanaonekana katika tangazo la msemaji wa polisi, David Misime, aliyesema watu 130 walikuwa wamekamatwa kwa madai ya kupanga mikutano na kusambaza ujumbe uliohimiza vitendo vya uhalifu vilivyolenga kuhujumu ustawi wa taifa hilo.

Amnesty imesema angalau watu 64 kati yao walishtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Mnamo Julai 9, visa vingine vilivyohusisha wanachama wa CHADEMA, wanafunzi wa vyuo vikuu na mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma aliyekamatwa kwa madai ya kuchochea watu kushiriki maandamano ya kuadhimisha Siku ya Saba Saba. Ingawa mhadhiri huyo aliachiliwa Septemba 10 baada ya mashtaka yanayohusiana na ugaidi kuondolewa, alitakiwa kuripoti katika kituo cha polisi kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Kwa kutumia mashtaka yanayohusiana na ugaidi dhidi ya watu wanaowaona kuwa wakosoaji wao, serikali ya Tanzania inatuma ujumbe wa kutisha kwamba haitasita kutumia njia yoyote katika juhudi zake za kukandamiza maoni yote yanayoipinga,” amesema Chagutah.

Amnesty pia imetaja vikwazo dhidi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, marufuku ya mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya watu wengi, pamoja na kuongezwa kwa vikosi vya usalama kabla ya maandamano yaliyopangwa, kama ishara za kupungua kwa nafasi ya raia kutumia haki zao za msingi.

Mashirika ya habari pia yamekabiliwa na hatua za kinidhamu nchini Tanzania. Mfano hai ukiwa uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusimamisha kwa muda leseni ya utangazaji ya Jambo Online TV kwa siku 90 mwezi Aprili, kutokana na maudhui yaliyohusu uchunguzi wa mauaji yaliyohusishwa na uchaguzi. Kituo hicho kilirejelea utangazaji mwezi Julai baada ya muda wa kusimamishwa kwa leseni kukamilika.

Aidha, mwezi Agosti, Idara ya Habari ilisimamisha kwa miezi sita leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Mwanahalisi kutokana na ripoti iliyohusu aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye Emmanuel Nchimbi.

Shirika hilo limeitaka serikali ya Tanzania kuondoa marufuku dhidi ya gazeti hilo, kurejesha upatikanaji wa majukwaa ya mitandao ya kijamii yaliyopigwa marufuku, kukomesha udhibiti wa maudhui ya mtandaoni na kuruhusu wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa uhuru bila hofu ya kulipiziwa kisasi.

Vilevile, shirika hilo limeitaka serikali kuondoa mashtaka ya ugaidi dhidi ya watu waliowekwa kizuizini bila haki na kukomesha vitendo vya kuwasumbua na kuwatisha watu wanaotumia haki zao za uhuru wa kujieleza na kufanya mikutano ya amani.

Our Correspondent Avatar