Search
Close this search box.
Africa

Augustine Lyatonga Mrema Mwanasiasa aliyetamba kwenye ulingo wa siasa na kuacha gumzo kila mahali 

9

Augustine Lyatonga Mrema ni mwanasiasa mashughuli nchini Tanzania alitamba katika jukwaa la siasa tangu alipokuwa mwanachama wa chama tawala hadi alipingia katika chaa cha upinzani.

Mrema ambaye hivi sasa hayupo katika uso wa dunia kufuati kifo chake kilichotokea Agosti 21,2022 katika hospitali ya Taifa Muhimbili nchini Tanzania alipokuwa amelazwa akipokea matibabu atakumbukwa kwa mengi hasa katika nguvu yake ya kujenga hoja za kisiasa dhidi ya watawala wa nchi.

Mwanasiasa huyo mkongwe amefariki akiwa na miaka 77 na alizaliwa huko mkoani Kilimanjaro , katika kijiji cha Kilaracha kilichopo katika Wilaya Moshi Vijijini  akiwa mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano ya Lyatonga Mrema. 

Aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mnamo mwaka 1990 hadi 1994 na baada ya alipewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu cheo ambacho hakikuwepo kwenye katika ya nchi. 

Mrema atabakia katika kumbukumbu za watu wengi hususan alipokuwa katika kilele cha umaarufu wakati wa uchaguzi wa Mkuu wa Tanzania wa mwaka 1995. 

Huo ulikuwa uchaguzi wa kwanza baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hii ilikuja kufuatia marekebisho ya ya Katiba ya Tanzania kuanzia Julai 1992, yaliyofuta mfumo wa chama kimoja cha siasa uliokuwa umedumu kwa  miaka 27 kuanzia 1965.

Akiwa mwanachama mgeni katika vyama vya upinzani Mrema alichochea moto wa siasa baada ya kujiunga na kilichokuwa chama kikubwa zaidi cha upinzani cha NCCR-Mageuzi Februari 1995, kisha kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

Katika uchaguzi huo, Mrema alikuwa mshindani wa karibu wa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Mkapa ambaye akiungwa mkono na muasisi na baba wa wa taifa hilo, Julius Kambarage Nyerere, hatimaye alishinda uchaguzi huo wa Oktoba 29,  kwa kunyakuwa asilimia 61.8 ya kura huku Mrema akiibuka wa pili kwa kupata asilimia 27.7 ya kura zote halali.

Waswahili husema mtembea bure si sawa na mkaa bure, Mrema alikosa kiti cha urais lakini nguvu yake ilikifanya chama cha NCCR Mageuzi kunyakua viti 17 vya ubunge Tanzania Bara. 

Miongoni mwa majimbo ambayo NCCR- Mageuzi ilishinda ni: Ubungo, Arusha Mjini, Mbeya Mjini, Iringa Mjini, Hai, Muleba Kaskazini, Vunjo, Urambo, Moshi Mjini, Musoma Vijijini na Bunda.

Hali hii ilionekana kuleta sura mpya katika Bunge lililokuwa na mchanganyiko wa wabunge kutoka vyama vya siasa. Ikumbukwe walikuwepo pia wabunge wa majimbo matatu ya Tanzania Bara: Karatu, Rombo na Kigoma Mjini kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wabunge zaidi ya 20 wa CUF kutoka Zanzibar.

Mara zote Mrema alikuwa akijinadi na kujenga wasifu wake juu ya uwezo wa ufuatiliaji wa kazi ikiwemo kuzuru maeneo tofauti kwa ghafla hata nyakati za usiku, na  kupambana na rushwa, ufisadi, magendo na ulanguzi wa mali.

Alisifika kwa kuhamasisha umma kujenga vituo vya polisi ili kuimarisha ulinzi pamoja na kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa jeshi la polisi katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Pia uongozi wa Mrema ulihamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi vilivyoundwa na wananchi, maarufu Sungunsungu.

Hata hivyo, vikundi hivyo vya sungusungu mara kadhaa vilishutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kujichukulia sheria mkononi kwa kuwatesa baadhi ya watuhumiwa wa uhalifu.

Alipobadilishwa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuhamishiwa wizara ya Kazi, Vijana na Michezo, akahamaki akidai mabadiliko hayo yalilenga kumnyamazisha asiendelee kupamba na na rushwa na wizi wa mali ya umma, akitolea mfano wa dhahabu iliyokamatwa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam lakini wahusika hawakuchukuliwa hatua yoyote.

Hapo ndipo akahamia upinzani akipoteza kiti cha ubunge wa Moshi Vijijini alichokuwa amekishikilia tangu 1987.    

Hata baada ya kushindwa urais, Mrema aliendelea na harakati za kuchaguliwa kwani Novemba 1996 alichaguliwa kuwa mbunge wa Temeke jijini Dar es Salaam katika uchaguzi mdogo, baada ya Mahakama Kuu kutengua matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa 1995 yaliyompa ushindi Ally Ramadhan Kihiyo wa CCM kwa sababu za udanganyifu.

Baadaye Mrema alikihama chama cha NCCR-Mageuzi na kujiunga na Tanzania Labour Party (TLP). Hatua hii ilikuwa baada ya mgogoro mkubwa wa kiuongozi ndani ya NCCR-Mageuzi kiasi cha kukiyumbisha chama na kukosa wabunge kwa muda mrefu. 

Pamoja na hayo umaarufu wa Mrema katika siasa ulianza kupotea kuanzia miaka 2000 ambapo aligombea tena kiti cha Urais kupitia chama cha TLP ambapo kwa mwaka huo alishika nafasi ya tatu na mwaka 2005 akashika nafasi ya nne.

Kuanzia hapo jina la Mrema lilikua ni nadra kulisikia katika vinywa vya watu ama vyombo vya habari hadi hapo alipokuja kuibuka tena alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya msamaha kwa wafungwa, maarufu bodi ya Parole nafasi ambayo alifumu nayo kwa takribani miaka 10.

Atakumbukwa pia kwa kauli tata kadhaa alizowahi kuzitamka katika uwanja wa Siasa. Kwa mfano wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 na yeye akiwa anagombea ubunge wa jimbo la Vunjo, alitamka kuwa anamuunga mkono mgombea wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete huku chama chake cha TLP kikiwa na mgombea urais, Muttamwega Mgaywa.                

Machi 2022 Augustine Mrema alitawala mitandaoni kwa taarifa na picha zake  baada ya kufunga ndoa na Doreen. Watu wengi walizungumzia ndoa hiyo hasa kwa kuzingatia tofauti ya umri kati ya Mrema Doreen.

Kazi na kujiendeleza kielimu

Mwaka wa 1955 hadi 1963  alianza masomo yake ya darasani mpaka shule ya kati katika Wilaya aliyopo huko huko mkoani Moshi vijijini. Ilivyofika 1964 hadi 1965  Mrema alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick. Tangu 1966 Mrema alikuwa mwanachama mkubwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM)

Baada ya kumaliza mafunzo yake ya Ualimu na kupata kazi Mrema alianza kuchukua mafunzo yake ya sekondari ambapo mwaka 1968 alifanya mtihani wake wa kidato cha nne, wakati huo mitihani ilikuwa ikitoka Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza.

Mwaka wa 1970 hadi 1971  alijiunga kwenye mafunzo maalumu ya siasa na uongozi katika Chuo cha Kivukoni na mwaka wa1980 -1981 alienda nchini Bulgaria ambako alifanikiwa kutunukiwa Diploma ya sayansi ya Ustawi wa jamii na Utawala

Alisoma shule ya msingi huko kijiji kwao na baadaye kujiendeleza na kufanya mtihani wa sekondari mwaka 1968 wakati huo mitihani ikiandaliwa na chuo kikuu cha Cambridge cha Uingereza.

Aliwahi kuhudumu pia kama Mwalimu katikka shule mbalimbali kabla ya kujiunga na Idara ya usalama wa Taifa. Huko amewahi kushika nafasi mbali mbalimbali ikiwemo kuwa Afisa Usalama wa Taifa mkoa wa Dodoma. Pia amewahi kuwa afisa mwanadamizi katika kituo cha Usalama wa Taifa kilichopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Comments are closed

Related Posts