Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Amani Golugwa, ameibua wasiwasi kufuatia taarifa zinazodaiwa kusambaa kuhusu uwezekano wa Mwenyekiti wao Tundu Lissu, kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 5, 2026, Golugwa amesema wasiwasi huo unatokana na madai yanayotolewa na baadhi ya wanaharakati kuhusu kuvuja kwa taarifa za siri zinazohusiana na hukumu inayotarajiwa kutolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam hapo kesho.
Golugwa amedai kuwa kuna mpango wa kumhukumu Lissu kifungo cha miaka mitano jela kwa sababu za kisiasa, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kumwekea vikwazo vya kisheria vitakavyomzuia kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao pamoja na kuendelea kutekeleza majukumu yake ya uongozi ndani ya CHADEMA.
Amesema madai hayo yameibua hofu miongoni mwa wanachama wa chama hicho, wanaharakati, familia ya Lissu na jumuiya ya kimataifa inayofuatilia kwa karibu masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, Golugwa ametetea hatua za wanaharakati wanaopaza sauti kupinga kile wanachokieleza kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya haki, akisema wana wajibu wa kuhimiza uwajibikaji na kudai mabadiliko yanayolenga kulinda haki na utawala wa sheria.
Amesisitiza kuwa CHADEMA itaendelea kusimamia misingi ya haki na kutetea kile inachoamini kuwa ni sahihi, bila kutishwa wala kurudi nyuma.
Akiendelea kuwasilisha maswali hayo, Golugwa amehoji pia iwapo Mwanasheria Mkuu aliwasiliana na Jaji Ndunguru kuhusu hukumu hiyo ya Tundu Lissu, na kama Jaji Ndunguru naye aliwasiliana na kiongozi wa serikali na kumweleza kuwa wameelekezwa na watu wa mfumo kumfunga Lissu miaka mitano jela. Pia amehoji iwapo majaji waliosikiliza kesi hiyo wamekuwa wakifanya kazi chini ya uangalizi au ushawishi wa vyombo vya serikali na Usalama wa Taifa.
Katika kumalizia mfululizo wa maswali hayo, Golugwa amehoji iwapo yupo mtu yeyote ndani ya mahakama anayejua matokeo ya hukumu hiyo ya Tundu Lissu kabla ya kutangazwa rasmi, pamoja na kuhoji kama kuna maagizo, maelekezo au shinikizo lolote la kisiasa lililotolewa kwa majaji kuhusu matokeo ya kesi hiyo.
Golugwa amesisitiza kuwa haya si maswali ya kawaida, bali ni hoja nzito zinazogusa msingi wa haki, uaminifu wa wananchi kwa mahakama na uhai wa utawala wa sheria nchini, kuelekea kusomwa kwa hukumu hiyo ya Tundu Lissu kesho ambayo tayari imezua mjadala mzito miongoni mwa wananchi, wanaharakati, familia na jumuiya ya kimataifa.
Haya yanajiri huku Jumuiya ya Madola ikikabiliwa na wimbi la lawama kutoka kwa wachambuzi na wakosoaji wa kimataifa kufuatia kumalizika kwa muda maalum uliowekwa kwa Serikali ya Tanzania bila kuchukua hatua zozote za kinidhamu.
Mvutano huo unatokana na makataa rasmi yaliyotolewa na chombo hicho kuitaka Serikali ya Tanzania kumwachia huru Mwenyekiti huyo wa CHADEMA, pamoja na kutoa maelezo ya kina kuhusu ghasia zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Hata hivyo, muda huo wa mwisho uliopangwa ulipita bila kuwepo kwa dalili zozote za vikwazo au adhabu dhidi ya serikali.
Wakosoaji hao wanailaumu Jumuiya ya Madola kwa kudhihirisha udhaifu wa wazi katika kusimamia maazimio na maagizo yake yenyewe mbele ya msimamo thabiti wa Tanzania, wakati serikali ya nchi hiyo ikiendelea kusimamia sheria zake za ndani bila kuyumbishwa.
Kufeli kwa vitisho na mikakati hiyo ya kimataifa kunaonyesha taswira mpya ya kijiografia, ikidhihirisha jinsi mamlaka za ndani zinavyoweza kulinda uhuru na taratibu zao za kisheria bila kuathiriwa na shinikizo za nje.







