Chivayo na Mkewe kuzikwa Oktoba 8 mjini Harare

Victor Wanaswa Avatar

Mfanyibiashara mashuhuri wa Zimbabwe Wicknell Chivayo pamoja na mkewe Lucy Muteke, wanatarajiwa kuzikwa Alhamisi, Oktoba 8, katika makaburi ya Glen Forest, Harare baada ya kufariki katika ajali ya helikopta iliyotokea Marondera.

Familia ya bwenyenye huyo imetangaza mipango ya mzishi huku ndugu, jamaa, marafiki na washirika wa karibu wakikusanyika katika makazi ya familia mjini Harare kuomboleza na kujiandaa kwa ajili ya mazishi ya wanandoa hao.

Familia pia imethibitisha kuwa hakutakuwa na zoezi la kutazama miili ya marehemu kabla ya mazishi kutokana na hali ya miili hiyo kufuatia ajali hiyo.

Kulingana na msemaji wa familia Herbert Chivayo, hatua ya kutoruhusu umma kutazama miili iliafikiwa baada yao kufika katika eneo la ajali na kuona hali ya miili ilivyo kutokana na ukubwa wa mkasa huo wa ajali.

“Hali ya miili ya Chivayo na mkewe si nzuri. Hivyo kama familia tumekubaliana kwamba kusikuwepo zoezi la kutazama miili hiyo kabla ya mazishi,” Alisema Herbert.

Alisema eneo la ajali katika shamba la Kudenga karibu na Marondera lilikuwa la kutisha huku waathiriwa wakipata majeraha zaidi kutokana na ukubwa wa ajali na moto uliofuata.

Msemaji huyo wa familia aliweka wazi kuwa mabaki ya miili yalitawanyika katika eneo la ajali na baadhi yaliteketea vibaya. Pia alisema miili hiyo ilikatika vipande kutoka na ajali hiyo.

“Tulipowasili katika eneo la mkasa miili na sehemu za binadamu zilikuwa zimwetawanyika na kutapakaa. Ilikuwa hali ya kutisha na kuogofya mno,” Alisema Herbert

Chivayo, mkewe Lucy Muteke, marubani wawili na mlinzi mmoja waliangamia baada ya helikopta yao kuanguka katika shamba la Kudenga siku ya Jumatano.

Uchunguzi wa kitabibu pamoja na vipimo vya DNA vinaendelea huku mamlaka zikifanya juu chini kubaini na kutambua mabaki ya wote waliofariki katika ajali hiyo.

Marubani, Calvin Tafirei Soda na Courage Matavirwa, pia wanaombolezwa na familia zao huku maandalizi ya mazishi yao yakiendelea.

Mazishi ya Chivayo na Muteke hata hivyo, hayatakuwa ya faragha kwani umma utaruhusiwa kuhudhuria na kutoa heshima zao za mwisho kwa wanandoa hao wawili.

Herbert pia amefichua kwamba Chivayo aliwahi kueleza nia yake ya kuwaachia watoto wake sehemu kubwa ya utajiri wake. Familia imesema itaheshimu matakwa hayo na kuhakikisha watoto wake wananufaika na mali aliyoacha.

 

 

 

 

 

Our Correspondent Avatar