Seneta Sifuna Ajipanga na Chama cha TEP Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027

Victor Wanaswa Avatar

Seneta wa kaunti ya Nairobi na kiongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna amezindua chama kipya cha kisiasa cha The Equitable Party of Kenya (TEP) ambacho anatarajiwa kutumia kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Wakati wa uzinduzi wa chama hicho Sifuna alitangazwa kama kiongozi na mwanaiaji rasmi wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa uongozi wa chama hicho, Sifuna alitoa hakikisho kuwa chama cha TEP kitaweka kipaumbele kuleta mabadiliko na uongozi unaozingatia mahitaji ya wananchi, sera ambayo anaamini itakuwa suluhisho kwa changamoto za kisiasa zinazoikabili Kenya.

“Tunaamini katika fursa sawa kwa kila mmoja katika taifa hili. Tutaskiliza kabla ya kuzungumza, tutashauriana kabla ya kufanya maamuzi, na kutaeleza sera zetu pamoja na kuwajibika kwa kila hatua tunayochukua,” alisema Sifuna.

Viongozi wa mrengo huo wa Linda Mwananchi waliohudhuria uzinduzi huo walisema chama hicho kitatoa jukwaa la kisiasa ambalo viongozi wake watatumia kutekeleza maono yao kwa taifa la Kenya.

“Wakati kiongozi wetu Edwin Sifuna anazungumzia maadili, wengine humkosoa kwa sababu hawaelewi kuwa mataifa makubwa hujengwa kwa maadili, wala si matofali na saruji,” alisema Mbunge Caroli Omondi.

Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka amemhimiza Sifuna kuanza rasmi mazungumzo kuhusu atakayepeperusha bendera ya upinzani na viongozi wengine wa upinzani kama vile aliyekuwa Naibu Rais na aliye pia Kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua, Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Kiongozi wa chama cha Jubilee Daktari Fred Matiang’i.

“Nataka kumuambia ndugu yangu Sifuna kuwa sasa ndio kazi imeanza, usilale, jumuisha viongozi wengine wa upinzani ili tupate mtu atakayekabiliana na Rais Ruto kwa debe ifikapo mwaka wa 2027 na kumbandua afisini,” alisema Onyonka.

Kwa upande wake Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ameweka wazi kuwa hatua inayofuata uzinduzi huo ni kubadili sura ya chama hicho kuwa Chama cha Linda Mwananchi.

“Nataka kutangaza kuwa chama hiki tutakibadili jina na kuwa chama cha Linda Mwananchi. Nataka kuwahimiza wafuasi wetu kujiunga na chama cha TEP ili tuwe na ufuasi mkubwa kote nchini,” alisema Osotsi.

Aliyekuwa kiongozi wa TEP, Gilbert Marava alisema chama hicho kiliamua kufanya mageuzi katika uongozi wake ili kumpa Sifuna na wafuasi wake nafasi ya kujiunga nacho na kukiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Marava alisema kuwa baadhi ya viongozi waliosajiliwa awali wataendelea kuhudumu huku wengine wapya wakijumushwa katika uongozi wa chama hicho. Aliongeza kuwa Sifuna ndio mgombea wa urais na kinara wa TEP.

Hatua hiyo inajiri huku Sifuna akijitahidi kugeuza vuguvugu la Linda Mwananchi kuwa jukwaa rasmi la kisiasa litakalomwezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Uzinduzi huo pia unaashiria mwanzo wa sura mpya ya kisiasa kwa Sifuna kufuatia mgogoro wake na chama cha ODM, ambako awali alikuwa akihudumu kama katibu mkuu.

Hatua ya Sifuna kujiunga na TEP inajiri wakati ambapo viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa wanazidisha mikakati ya kujipanga na kuimarisha ushawishi wao huku taifa likisubiri uchaguzi mkuu mwakani.

Hafla hiyo ilihudhuhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa wakiwemo Magavana George Natembeya wa Trans Nzoia, James Orengo wa Siaya, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria (LSK) Faith Odhiambo na wabunge mbalimbali wanaoegemea upande wa Linda Mwananchi.

 

 

 

 

Our Correspondent Avatar