Mke wa aliyekuwa Naibu Rais Mchungaji Dorcas Rigathi amepaza sauti kuhusu kile alichokitaja kama ongezeko la changamoto zinazowakabili wavulani nchini, akionya kuwa matumizi ya pombe na dawa za kulevya yanaharibu familia na kuchangia vifo vya vijana.
Akizungumza na kundi la wanawake mjini Worcester, Massachusetts nchini Marekani, Dorcas aliibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya matumizi ya vileo na dawa za kulevya, visa vya kujitoa uhai, ajali za barabarani na uhalifu miongoni mwa vijana nchini Kenya.
Alidai kuwa kufikia wakati alipokamilisha muda wake wa kuhudumu katika afisi ya Mke wa Naibu wa Rais, nusu ya wanafunzi wa vyuo vikuu walikuwa wakikabiliwa na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya. Pia alisisitiza kuwa angalau wanafunzi kumi wa vyuo vikuu walikuwa wakifariki kwa kujitia kitanzi kila siku.
Hata hivyo, takwimu hizo zilizotolewa na Mke wa aliyekuwa Naibu Rais hazikaweza kudhibitishwa kwa njia huru.
Kwa mujibu wa Dorcas, takriban asilimia 90 ya wanaoathiriwa na changamoto hizo ni wavulana, hali inayoziacha familia nyingi katika njia panda huku baadhi ya wazazi wanaowapeleka watoto wao vyuoni kwa matumaini ya kuhitimu wakipokea miili yao badala ya kuwaona wakikamilisha masomo yao na kufanikiwa maishani.
Alitaja eneo la Mlima Kenya kuwa miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na hali hiyo akisema baadhi ya viongozi wa kidini wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kuwazika vijana wanaodaiwa kufariki kutokana na matatizo yanayaohusiana na unywaji wa pombe.
Alidai kuwa baadhi ya wachungaji hulazimika kuendesha mazishi ya vijana kila wiki, huku wengine wakiripotiwa kufariki baada ya kubugia pombe bila kula chakula.
Aidha, Dorcas alihusisha matumizi ya pombe na dawa za kulevya na ajali za barabara akidai kuwa baadhi ya madereva wa matatu na waendeshaji wa bodaboda huendesha magari na pikipiki wakiwa walevi chakari, hivyo kuhatarisha Maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Alionya kuwa ajali hizo zimechangia vifo na ulemavu wa kudumu huku hospitali zikiendelea kupokea waathiriwa wa ajali za pikipiki.
Katika maelezo yake, Dorcas pia alihusisha matumizi ya vileo na dawa za kulevya na ongezeko la uhalifu pamoja na ukatili wa kijinsia, akisema hali hiyo inazidisha ugumu wa maisha kwa familia zinazopoteza walezi na watu wanaowategemea kiuchumi.
Alidai kuwa wanaume ni asilimia 90 ya wafungwa nchini, akionya kuwa kufungwa jela na vifo vya mapema vya wanaume kunawaacha wajane na kina mama wanaohangaika kulea familia na watoto wanaokosa fursa za kupata elimu.
Akirejelea juhudi zake alipokuwa akihudumu kama Mke wa Naibu wa Rais, Dorcas alisema afisi yake ilikuwa imesaidia zaidi ya watu 2,000 waliopoteza uwezo wa kuona au viungo vya mwili baada ya kutumia pombe haramu kwa kuwapatia vifaa saidizi.
Aliwataka wanawake wakenya wanaoishi ughaibuni kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto hiyo, kuzungumza na wana wao na waume zao kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuunga mkono kampeni za uhamasishaji katika shule nchini Kenya.
Dorcas alisisitiza kuwa juhudi za kulinda mtoto wa kike hazipaswi kupuuza changamoto zinazowakabiliwa wavulana akisema vifo vyao na kufungwa kwao jela kuna athari kubwa kwa wanawake, watoto na jamii kwa ujumla.







