Wizara ya Afya nchini Kenya imetangaza kuwa watu 122 waliotagusana na mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola wametambuliwa na kuthibitishwa huku 108 kati yao wakiwekwa karantini kwa ufuatiliaji wa karibu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, wizara hiyo ilisema kuwa hakuna mtu hata mmoja kati yao ameonyesha dalili za ugonjwa huo hatari. Juhudi za kuwafuatilia watu wengine ambao huenda waliotangamana na mgonjwa huyo zinaendelea.
Wakati huohuo, hatua za kudhibiti maambukizi zinaendelea kuimarishwa nchini. Wizara ilisema jumla ya sampuli 293 zimefanyiwa uchunguzi kutokana na visa 289 za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa na maambukizi.
Idadi ya wasafiri waliochunguzwa katika vituo 26 vya kuingia nchini imefikia 667,675 huku 2,345 wakifanyiwa uchunguzi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Wizara pia ilifichua kuwa maabara tano zimetengwa kwa ajili ya kupima sampuli za Ebola, zikiwemo maabara mbili tamba katika mpaka wa Lwakhakha na Busia ili kuimarisha uwezo wa kutambua maambukizi mapema.
Jumla ya vitanda 241 vya kutenga wagonjwa vinapatikana katika hospitali tano zilizoko Nairobi, Eldoret na Mombasa. Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi Eldoret ina vitanda 50 vya wagonjwa mahututi katika mpango huo wa maandalizi.
Kwa mujibu wa wizara, sampuli kutoka kaunti zote zinaweza kupelekwa katika maabara hizo huku matokeo ya vipimo vya kuthibitisha maambukizi yakipatikana ndani ya saa sita hadi 12.
Wahudumu wa afya 4,917 wamepata mafunzo kuhusu usimamizi wa ugonjwa wa Ebola. Kikosi cha dharura chenye wataalamu 343 waliofunzwa pia kiko tayari kupelekwa katika maeneo yatakayohitaji msaada, wakiwemo wataalamu 102 walioshiriki katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi kati ya mwaka wa 2014 na 2016.
Hata hivyo, wizara imesisitiza kuwa hakuna marufuku iliyowekwa kuhusu usafiri, biashara, usafirishaji au mikusanyiko ya umma wala hakuna amri ya kutotoka nje iliyotangazwa.
“Viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani vinaendelea kufanya kazi kama kawaida japo uchunguzi wa afya umeimarishwa kwa wasafiri wanoingia nchini,” Wizara ya Afya.
Hatua hizi zinafuatia kisa cha kwanza cha Ebola nchini kilichoripotiwa Oktoba 6 ambapo mgonjwa aliyekuwa ametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alifariki katika Hospitali ya Nairobi akipokea matibabu.
Waziri wa Afya Aden Duale alikuwa ametangaza Oktoba 7 kuwa safari za ndege kutoka nchi 10 zitaimarishiwa uangalizi huku ndege kutoka DRC, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Angola, Zambia, Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati zikielekezwa kutumia lango maalum ya kuingia katika Uwanja wa ndege wa JKIA.
Wizara imehaidi kuwa itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hali ya ugonjwa huo na kusisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema na hatua za kuzuia kuenea kwa maambukizi.







