Kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua, ametetea mikutano ya kitamaduni inayoandaliwa na jamii ya Mlima Kenya, akipuuza madai kuwa mikutano hiyo inachochea ukabila na kusisitiza kuwa wenyeji wa eneo hilo hawapaswi kujutia kupigania haki zao kama jamii.
Gachagua amesema jamii zote nchini zina haki ya kukutana, kusherehekea urithi wao wa kitamaduni na kujadili masuala yanayowahusu, akihoji kwa nini mikutano kama hiyo inayoandaliwa na jamii nyingine nchini haijakosolewa.
Alizungumza hayo wakati wa toleo la pili la hafla ya kila mwaka ya Ngemi cia Watho, iliyoandaliwa na chama cha GEMA WATHO Association mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja mawakili na wataalamu wengine wa masuala ya sheria kutoka jamii za Wakikuyu, Waembu, Wameru na Wakamba, pamoja na viongozi wa kisiasa, akiwemo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Katika hotuba yake, Gachagua alitaja mikutano inayoandaliwa na jamii ya Mulembe pamoja na jamii za wafugaji kaskazini mwa Kenya, akisema mikutano ya jamii ya Mlima Kenya inapaswa kutambuliwa pia kama majukwaa ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kikanda.
“Wakati jamii ya Mulembe, kupitia Wetang’ula na Musalia, inapowakusanya watu wake kwa mazungumzo, huo unaitwa ushirikiano wa eneo la Magahribi. Wakati jamii za kaskazini mwa Kenya zinapokutana, wanasema wafugaji wanajadili masuala yao. Jamii nyingine zinapokutana, hakuna anayekuwa na tatizo. Lakini watu wa Mlima Kenya wanapokutana, kama walivyofanya leo, tunatuhumiwa kwa ukabila,” alisema.
Kiongozi huyo aliwataka wakaazi wa Mlima Kenya kutofedheheka na utambulisho wao wa kikabila, akisema wanapaswa kuendelea kuthamini utamaduni na lugha yao bila kujali kiwango chao cha elimu au mafanikio yao ya kitaaluma.
Alisisitiza kuwa jamii mbalimbali nchini Kenya ni sehemu ya utajiri wa utofauti wa taifa hili na zina haki ya kuhifadhi utambulisho wao wa kitamaduni.
Gachagua pia alimkosoa Rais William Ruto, akisema watu wa Mlima Kenya hawapaswi kufanywa wajihisi kama wageni katika nchi yao wenyewe.
“William Ruto ajue kuwa watu wa Mlima Kenya si wakimbizi katika nchi yao wenyewe. Na ndiyo maana tumeamua kama eneo na jamii kwamba lazima tumpeleke nyumbani kwa njia moja au nyingine,” alisema.
Aidha, alisema eneo la Mlima Kenya litamteua mgombea mmoja wa urais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Aliongeza kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais, atakuwa mwenyeji wa toleo la tatu la hafla ya Ngemi cia Watho katika Ikulu ya Sagana.
Naibu Rais wa zamani pia alitumia hafla hiyo kuwataka mawakili kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kutetea Katiba, kulinda haki za binadamu na kuhakikisha mchakato wa uchaguzi nchini unalindwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Aliwataka mawakili kushiriki kikamilifu katika kufuatilia shughuli za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiwahimiza kujitolea kuwa waangalizi wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uadilifu.
Gachagua alisema mawakili wana wajibu wa kuchunguza kwa makini taratibu zote za uchaguzi, akibainisha kuwa michakato inayotangulia uchaguzi ni muhimu sawa na zoezi lenyewe la kupiga kura.
“Taratibu za uchaguzi ni muhimu sawa na uchaguzi wenyewe. Tunapaswa kushirikiana nanyi ili muwe waangalizi katika maeneo mbalimbali nchini na kuhakikisha kuwa William Ruto haibi uchaguzi wetu,” alisema.
Pia aliitaka Jumuiya ya Wanasheria nchini (LSK) kukemea kwa nguvu zaidi kile alichokitaja kuwa dhuluma zinazotekelezwa nchini, akiwataja viongozi wa zamani wa LSK, Paul Muite, Nelson Havi na Martha Karua, kama mifano ya mawakili ambao wamekuwa wakijitokeza kuzungumzia masuala ya kitaifa.
Kiongozi huyo wa DCP aliwapongeza mawakili kutoka eneo hilo kwa kutoa huduma za kisheria bila malipo kwa vijana waliokamatwa wakati wa maandamano yaliyoongozwa na kizazi cha Gen Z kati ya mwaka 2024 na 2025.
Alisema mawakili hao waliwatetea vijana waliokamatwa bila kuwatoza ada za uwakili, wakasaidia kuchangisha fedha za dhamana ya pesa taslimu na kuwasilisha maombi ya masharti ya dhamana ambayo aliyataja kuwa ya gharama kubwa kupita kiasi.
Aliwashukuru zaidi mawakili hao kwa kuingilia kati kesi za baadhi ya waandamanaji waliokuwa wamefunguliwa mashtaka yanayohusiana na ugaidi, akisema juhudi zao zilisaidia kuwalinda vijana hao dhidi ya madhara yaliyoweza kutokana na mashtaka hayo.
Kuhusu visa vya utekaji nyara, Gachagua alilaani kutoweka kwa wakili Abshir Abdi, ambaye alisema alitekwa nyara katika eneo la Kilimani mnamo Novemba Mosi.
Aliitaka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kubaini aliko wakili huyo na kuhakikisha anafikishwa mbele ya umma akiwa hai au amefariki.
“Ikiwa mawakili wanatekwa nyara, itakuwaje kwa Wakenya wa kawaida?” alihoji.
Gachagua pia aliwapongeza mawakili walioshiriki katika shughuli za kisiasa eneo la Ol Kalou, akielezea matukio hayo kama mfano wa namna wapiga kura wanavyoweza kuwachukulia hatua za kisiasa viongozi wanaohisi wamewadanganya.
Aidha, alisema amevutiwa na uwezo na hadhi ya watu wanaowania nyadhifa za kisiasa katika eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Kiongozi huyo wa DCP alilinganisha muundo wa kisiasa anaotaka kujenga katika eneo hilo na ule wa marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ambaye alimsifu kwa kuijenga chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kukifanya kuwa chama chenye uwakilishi mkubwa bungeni.
Kwa upande wake, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambaye pia alihutubia hafla hiyo, alikiri kuwa amekuwa na tofauti za kisiasa na Gachagua hapo awali, lakini akasema wawili hao wamekubaliana kuweka kando tofauti zao kutokana na kile walichokitaja kuwa tishio linalotokana na utawala wa Rais Ruto.
“Sisi ni watu ambao kwa kawaida usingetarajia kushirikiana kisiasa, kama wanavyosema, na historia yetu imekuwa na misukosuko mingi,” alisema Sifuna.
Seneta huyo alisema upinzani unapaswa kuweka mbele azma yake ya pamoja ya kisiasa badala ya kuruhusu tofauti binafsi kuzuia ushirikiano kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Pia aliwataka mawakili kuendelea kuwa katika mstari wa mbele katika kutetea Katiba na kulinda haki za Wakenya.








