Jamhuri, Lissu Ngoma Nzito Kesi Yaahirishwa

Kesi ya Uhaini inayomkabili Tundu Lissu leo imechukua sura mpya baada ya kuibuka kwa mvutano mkali kati ya Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA, na upande wa Jamhuri wakati wa maswali ya dodoso yanayolenga kuhoji na kupima ushahidi alioutoa katika kesi inayomkabili.

Shahidi wa Kificho Asema Ana Hofu Kutoa Ushahidi Hadharani Katika Kesi ya Uhaini ya Lissu

Maswali yaliyoulizwa na mawakili wa Jamhuri, yakiongozwa na Wakili wa Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga na baadaye Wakili Job Mrema, yaligusa maeneo mbalimbali ya ushahidi wa Lissu, kuanzia tuzo alizowahi kupata, uanaharakati wake, uchaguzi, mashahidi wa polisi, matumizi ya vifungu vya sheria, hadi tafsiri ya baadhi ya kauli zilizotolewa katika mikutano na hotuba zake.Katika baadhi ya majibu, Lissu alionekana kutofautiana moja kwa moja na tafsiri iliyokuwa ikiwekwa na upande wa mashtaka, huku akisisitiza kuwa baadhi ya mambo aliyowasilisha mahakamani hayakuwasilishwa kwa namna Jamhuri ilivyokuwa ikiyaeleza.Miongoni mwa maeneo yaliyoibua mvutano ni hoja kuhusu mashahidi wa kificho waliotajwa kwa namba badala ya majina yao.Katuga alimtaka Lissu kueleza ni sheria gani inayomtaka shahidi kutajwa kwa jina halisi kabla ya kutoa ushahidi mahakamani.Lissu akajibu kwa kurejea Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), akitaja Kifungu cha 192 na kueleza kuwa hakuna sharti la jumla linalosema shahidi hawezi kutoa ushahidi kwa sababu majaji hawajui jina lake.Alipoendelea kubanwa kuhusu mashahidi waliotajwa kama P1 na P2, Lissu alisema hizo siyo majina bali ni namna ya kuwaficha utambulisho.Mvutano mwingine ulijitokeza katika hoja kuhusu waandishi wa habari waliowahi kuondolewa katika mkutano.Katuga alimtaka Lissu kuthibitisha kama katika ushahidi wake aliwahi kukanusha kuwa waandishi waliondolewa baada ya hotuba.Lissu alisema hakuwahi kukanusha kwa sababu jambo hilo halikuwa miongoni mwa masuala yaliyowapeleka mahakamani, lakini alipoulizwa kama wao ndio waliowatoa waandishi, alijibu kwa kifupi: “Tuliwatoa.”Katika sehemu nyingine, Katuga alirejea kauli za Lissu kuhusu mashahidi wa polisi na kudai kuwa baadhi yao waliandika wenyewe maelezo yao ya ushahidi, jambo ambalo Lissu alilipinga kwa msingi kwamba polisi ambao hawakufuata utaratibu wa kisheria hawawezi kuaminika katika ushahidi wao.Lissu alirejea Kifungu cha 11(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, akisema kinahusu utaratibu wa kuandika maelezo.Maswali yalihamia pia kwenye tuhuma za uchochezi, kauli za “tutakinukisha”, kuzuia uchaguzi na kile ambacho Jamhuri ilikitafsiri kama kuhamasisha uasi.Katuga alitaka kujua kama Lissu anaona kuhamasisha uasi au “kukinikisha” ni njia ya kidemokrasia.Lissu alijibu “ndiyo”, huku akisisitiza katika sehemu nyingine kwamba alichokuwa akizungumzia ni kuipinga Serikali, siyo kuipindua.Alipoulizwa kama kuzuia uchaguzi ni sawa na kuipinga Serikali, Lissu alijibu kwa kusisitiza: “Kuzuia uchaguzi ni kuzuia uchaguzi.”Jamhuri pia ilimkabili Lissu kuhusu ushahidi wa video, baada ya Lissu kueleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka kwa kutowasilisha video.Katuga alimtaka Lissu kueleza kama katika hati ya mashtaka kuna sehemu inayomtuhumu kwa kuchapisha video.Lissu akajibu kuwa ameshtakiwa kwa kuchapisha maneno kwenye mtandao wa Jambo TV, akisisitiza tofauti kati ya maneno na video.Katika sehemu nyingine ya dodoso, Lissu alikiri kwamba yeye ndiye mhusika wa baadhi ya maneno yaliyo kwenye hati ya mashtaka, lakini akapinga tafsiri iliyotolewa na mashahidi wa Jamhuri, akisema hawakuyatafsiri maneno hayo kwa usahihi.Baadaye Wakili Mrema alichukua nafasi na kuendelea kumhoji Lissu kuhusu historia yake kama mwanaharakati, maana ya uanaharakati na iwapo uanaharakati unatambulika kisheria.Lissu alisema amekuwa mwanaharakati kwa muda mrefu na akarejea Katiba akisema inatoa haki na wajibu kwa wananchi kupigania mambo wanayoamini.Mrema pia alimuuliza Lissu kama mtu akiwa mwanaharakati ana haki ya kuvunja sheria, na Lissu akajibu kuwa hana haki hiyo. Jibu hilo hilo alilitoa alipoulizwa kuhusu mwanasiasa.Katika swali lililozua mvutano mwingine, Mrema alimuuliza Lissu kama ni sahihi kusema kwamba baada ya Mahakama kumtia hatiani atakuwa “mtu wa hovyo.”Lissu alijibu: “Sio sahihi.”Mrema akarudia: “Ni sahihi.”Sehemu hiyo ikawa miongoni mwa nyakati zilizovuta hisia wakati wa dodoso hilo.Kwa ujumla, maswali ya Jamhuri leo yalionekana kulenga kutengeneza picha kwamba baadhi ya kauli na hoja zilizotolewa na Lissu katika utetezi wake zinapingana na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, huku Lissu akijibu kwa kusisitiza tafsiri yake ya matukio, sheria na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.Kesi imeahirishwa mpaka kesho Agosti 28,2026 saa tatu asubuhi