Upande wa Jamhuri umeendelea kuuchambua ushahidi wa John Heche, shahidi wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kwa kumuuliza maswali kuhusu msingi wa taarifa alizotoa kuhusu watu waliodaiwa kutekwa, kupotea na kuuawa.

Katika dodoso hilo, mawakili wa Serikali Ignas Mninuka na Nassoro Katuga walitaka kufahamu iwapo Heche mwenyewe aliwahi kushuhudia baadhi ya matukio aliyoyataja katika ushahidi wake.
Heche alisema hakuwahi kushuhudia mtu akitekwa kwa macho yake wala kumwona mtu akipotea, huku kuhusu baadhi ya matukio ya mauaji aliyoyataja akisema hakuwapo wakati yakitekelezwa.
Katika suala la Simon Kaguye, Heche alisema hakufanya uchunguzi wa tukio hilo mwenyewe, bali alizungumza na familia yake ambao walimweleza kuwa mtu huyo alikuwa ametoweka.
Alipoulizwa aliyempa taarifa hizo, alisema ni mke wa Kaguye.
Maswali hayo yalimfanya Katuga kuchunguza tofauti kati ya taarifa ambazo Heche alizishuhudia mwenyewe na zile alizozipata kutoka kwa watu wengine au kupitia vyombo vya habari.
Heche ambaye ni shahidi wa tano utetezi pia alikiri kuwa baadhi ya ripoti za uchaguzi za kikanda na kimataifa alizozitumia katika ushahidi wake alizipata kupitia vyombo vya habari.
Baadhi ya ripoti hizo, alisema, zilikuwa zimeandikwa kwa Kiingereza na yeye ndiye aliyekuwa akizitafsiri kwenda Kiswahili mahakamani.
Katika hatua nyingine, upande wa Jamhuri uliingia kwenye taarifa binafsi za Heche, ukiuliza kuhusu elimu yake, majina aliyotumia tangu shule, familia, nafasi yake ndani ya Chadema, kipato, umiliki wa magari pamoja na miamala ya fedha kwenye akaunti yake ya benki.
Heche alieleza kuwa kuanzia shule ya msingi hadi sekondari alisoma kwa jina la Wengesa Chacha Suguti na alipoulizwa kuhusu matokeo yake ya kidato cha nne, alikanusha kupata daraja la nne la pointi 26, akisema alipata Division One ya pointi 11.
Alipoulizwa kuhusu Suguta David Heche, alisema ni mdogo wake na akaeleza kuwa ana wadogo zake watatu, huku akisema baba yake alikuwa na wake nane.
Maswali hayo yaliendelea kwenye nafasi yake ndani ya Chadema, ambapo Heche aliulizwa kama mbali na cheo chake cha Makamu Mwenyekiti anajishughulisha na shughuli nyingine na kama aliwahi kuiambia Mahakama kuhusu mshahara au posho anayopata kutokana na nafasi hiyo.
Heche alisema hajawahi kuiambia Mahakama kuwa anajishughulisha na shughuli nyingine, na kwamba kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema halipwi mshahara wala posho.
Jamhuri pia ilimuuliza kuhusu umiliki wa mali, ikiwemo madai ya kuwa ana malori yanayoendesha shughuli nchini Kenya na magari ya bei kubwa.
Heche alikanusha kuwa na malori nchini Kenya, huku akisema ana magari mawili. Hata hivyo, baada ya Wakili kuomba kwa ridhaa ya Mahakama kumuonyesha nyaraka za kadi za magari, akaeleza kuwa nyaraka hizo zilikuwa tano na kwamba si zote zilikuwa magari, kwa kuwa kulikuwa pia na mashine.
Alipotakiwa kutaja mali hizo, Heche alisema ni trekta kwa ajili ya kilimo cha parachichi, Mitsubishi Canter, Toyota Crown, Harrier Double Cabin na Toyota Prado.
Katika masuala ya fedha, Wakili alimuuliza kuhusu utaratibu wa Chadema kwa viongozi wanaopokea michango kwa ajili ya chama, pamoja na fedha zinazodaiwa kutoka kwa watu mbalimbali. Heche alisema masuala ya fedha ni eneo la Katibu Mkuu na alikanusha kumjua mtu aliyetajwa kama Salman katika maswali kuhusu fedha.
Jamhuri pia ilimhoji kuhusu ripoti ya TLS aliyotumia katika ushahidi wake kuhusu watu waliodaiwa kupotea. Heche awali alitaja idadi ya watu 781, lakini baada ya Wakili kumuonyesha ripoti aliyokuwa akiirejea na kusema inaonyesha watu 718, Heche aliomba kufanya marekebisho na kusema idadi hiyo ni 718.
Maswali yaliendelea kuhusu ripoti za TLS za mwaka 2024, ambapo Heche alisema anafahamu kuwa taasisi hiyo ilitoa taarifa kuhusu watu 83.
Katika sehemu nyingine, Heche aliulizwa kuhusu Simon Kangwire na kusema anamjua na kwamba alitekwa mwaka 2023. Alipoulizwa kama alikuwepo wakati akitekwa, alisema alisikia.
Jamhuri pia ilimuuliza kuhusu matukio mengine ya uhalifu na mauaji, ikitaka kujua kama Heche anatambua kwamba baadhi ya watu wanaweza kuuawa kwa sababu nyingine, zikiwemo visasi.
Heche alisema hafahamu, huku kuhusu tukio alilolisikia la mwanamke kumuua mpenzi wake na kumfukia akisema taarifa hiyo aliipata kupitia vyombo vya habari.
Wakili Katuga alisisitiza mbele ya Mahakama kwamba kinachotakiwa ni ushahidi na si siasa, jambo ambalo Heche alisema analifahamu.
Maswali hayo yaliendelea kwenye mada ya taarifa za watu waliodaiwa kutekwa, ambapo Heche alisema alizungumza na ndugu wa Simon Kangwire na kuambiwa kuwa ametekwa. Kwa mujibu wa Heche, ni wajibu wa vyombo vya dola kufanya uchunguzi.
Katika sehemu nyingine ya dodoso, Wakili alimuuliza Heche kuhusu kauli mbalimbali zinazohusiana na Mahakama, sheria na ushahidi. Heche alisema ameanza kusoma sheria, lakini alipoulizwa kuhusu msemo unaodai kuwa “Mahakama sio mama yako”, alisema haujui na kwamba yeye si mwanasheria.
Maswali ya Jamhuri pia yaligusa maisha binafsi ya Heche, ikiwemo jezi ya Arsenal aliyodaiwa kununua kwa pauni 517 ikiwa na jina lake. Heche alisema alinunua mwenyewe na akaeleza kuwa ana jezi nyingi na hununua kila mwaka.
Baadaye aliulizwa kuhusu mtu anayeitwa Salman na madai ya fedha zilizoingia kwenye akaunti yake. Heche alisema hamfahamu Salman na akakanusha madai kwamba aliingiziwa Sh10 milioni na baadaye Sh20 milioni na mtu huyo.
Hata hivyo, alipoulizwa kama ana akaunti ya benki ya CRDB na kama namba iliyotajwa ni ya kwake, alikiri kuwa ni yake. Pia alikiri kuwa Sh30 milioni ziliingia kwenye akaunti hiyo na kwamba kwa mujibu wa risiti aliyoonyeshwa, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake.
Maswali hayo ni sehemu ya dodoso la Jamhuri linalolenga kuchunguza msingi wa ushahidi wa Heche, pamoja na taarifa na nyaraka mbalimbali alizowasilisha au kuzirejea katika ushahidi wake.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo), James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya utetezi.
Katika kesi hiyo, Lissu ambaye pia ni Wakili anakabiliwa na kesi ya uhaini akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) Rekebu ya mwaka 2023.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika (kuchapisha) mtandaoni maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.