Kenya imerekodi kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo (BDBV), baada ya raia mmoja wa Kenya aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufariki kutokana na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya Aden Duale akiongea na Wanahabari alisema mgonjwa huyo aliwasili nchini Oktoba 3, baada ya kuishi DRC kwa miaka saba.
Wizara ya Afya imesema kuwa mwathiriwa huyo alianza kuugua mwezi mmoja uliopita akiwa DRC, ambako alitibiwa katika hospitali kadhaa kabla ya kusafiri kwa barabara kutoka DRC hadi Kampala Uganda.
Kutoka Kampala, mgonjwa huyo alipanda ndege ya Jambojet nambari ya usajili 8523 hadi Jijini Nairobi, ambako alifanyiwa ukaguzi wa kawaida wa afya ya umma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Baadaye alichukuliwa na ndugu na rafiki kwa kutumia gari aina ya Toyota Fielder lenye nambari ya usajili KDG 699Z na kupelekwa Hospitali ya Nairobi ambako alitengwa katika chumba cha dharura.
Waziri Duale alisema mgonjwa huyo baadaye alihamishiwa katika wodi maalum ya kutenga wagonjwa katika upande wa Mashariki mwa hospitali hiyo, kituo kilichotumika wakati wa janga la Covid-19 na chenye vitanda zaidi ya 145 pamoja na vifaa muhimu vya matibabu.
Vipimo vya kimatibabu vilionyesha kuwa mgonjwa huyo alikuwa na homa, uchovu na udhaifu mkubwa wa mwili, maumivu ya misuli, maumivu wakati wa kumeza pamoja na kutokwa na damu kwenye ngozi eneo alikodungwa sindano.
Madaktari walishuku kuwa huenda alikuwa akiugua homa ya virusi inayosababisha kutokwa na damu na kuchukua sampuli za vipimo, ambazo baadaye zilithibitisha uwepo wa virusi vya Ebola.
Licha ya kupewa matibabu ya kumsaidia mwili kukabiliana na ugonjwa huo, Duale alisema mgonjwa huyo alifariki Jumatatu usiku.
Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika baadaye leo kwa kuzingatia taratibu maalum za afya ya umma zinazohusiana na Ebola.
Wizaya ya afya imesema hadi sasa imetambua watu 28 waliowasiliana na marehemu, huku juhudi zikiendelea kuwasaka abiria 23 na wahudumu wanne walikuwa kwenye ndege aliyosafiria kutoka Kampala hadi Nairobi.
Duale alisema mipango ya kuwaweka karantini watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa imekamilika kwa lengo la kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kulinga afya ya umma.








