Kiongozi wa chama cha Jubilee Fred Matiang’I amemtaka Rais William Ruto kuwacha kuwapotosha wakenya kuhusu mauaji yaliotokea Mto Yala, akisema kuwa hawezi kamwe kujitenga na maamuzi ya kiusalama yaliyofanywa wakati alipohudumu kama Naibu wa Rais na mjumbe wa Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC).
Akiongea akiwa kaunti ya Mombasa, Matiang’I alisema Ruto alikuwa miongoni mwa Baraza la juu zaidi ya kufanya maamuzi kuhusu usalama wa kitaifa, wakati miili 36 ilipongunduliwa katika Mto Yala kati ya mwaka wa 2021 na 2022. Alisema kwa hivyo, Ruto hafai kulichukulia suala hilo kana kwamba hakujua chochote kuhusu kilichokuwa kikitendeka.
Matiang’i alisema hakuna uwezekano wa maafisa wa usalama kufanya makosa wakati Ruto akiwa mwanakamati wa Baraza la Kitaifa la Usalama bila yeye kufahamu makosa hayo na jinsi yalivyofanyika.
Alisema kuwa mujibu wa Katiba, Baraza la Kitaifa la Usalama linajumusha Rais, Naibu Wake, Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Usalama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Hazina ya Kitaifa, Waziri wa Masuala ya Kigeni pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Usalama akiwemo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Inspekta Jenerali wa Polisi.
“Tulihudumu pamoja naye katika Baraza la Kitaifa la Usalama kwa miaka hiyo yote, na sasa yeye ndiye Rais. Anaweza kuuliza maswali kuhusu watu waliouawa katika Mto Yala na kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria,” alismea Matiang’i.
Matiang’I alisisitiza kuwa Ruto, akiwa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Usalama anapaswa kuchunguza kilichotokea badala ya kuligeuza suala hilo kuwa la kisiasa katika mikutano ya hadhara.
“Kwa sasa yeye ndiye Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Usalama. Badala ya kulalamikia wakenya katika mikutano ya kisiasa kila mahali anapokwenda anapaswa kuagiza uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu suala hilo ili waliohusika wakamatwe na kuwajibishwa ipasavyo,” alisisitiza Matiang’i.
Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani alisema amekuwa akitaka kubuniwe kwa tume ya uchunguzi kuhusu vifo hivyo katika Mto Yala na yuko tayari kueleza yaliyotokea wakati alipokuwa serikalini.
Amefichua kuwa msimamo wake unaendana na matamshi yake ya awali, ambapo alitaka tume hiyo iundwe na kueleza kuwa alikuwa tayari kufika mbele yake na kutoa Ushahidi.
“Tunapopokea taarifa, ni muhimu kuelewa kuwa mauaji yanaweza kutokea kupitia njia mbalimbali zinazokiuka sheria. Ikiwa zaidi ya miili mitatu au minne ingepatikana katika eneo moja, polisi wangeanza uchunguzi,” alisema kiongozi huyo.
Kinara huyo wa chama cha Jubilee alitetea rekodi yake ya utumishi wa umma, akisema iko wazi kwa uchunguzi wa yeyote anayetaka kuikagua.
“Rekodi yangu ya utumishi wa umma ni safi kabisa, na utendakazi wangu ni jambo ambalo kila mtu huzungumzia,” alisema Mating’i
Matiang’i aliongeza kuwa hivi majuzi alishangazwa na matamshi ya kasisi mmoja kuhusu kazi yake serikalini, akisema hilo lilionyesha kuwa wananchi walikuwa wakifuatilia utendakazi wake alipokuwa mamlakani.
Hata hivyo, aliwashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kutumia suala la vifo vya Mto Yala kama kisingizio cha kumshambulia kisiasa.








