, ,

Lissu: Kesi Ya Uhaini Dhidi Yangu Imejengwa Kwenye Msingi Wa Hisia

Wadh Kassim Avatar

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haujaonyesha kwamba alikuwa na nia ya kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akidai kesi hiyo imejengwa zaidi kwenye hisia kuliko masharti ya sheria.

Lissu: Kesi Ya Uhaini Dhidi Yangu Imejengwa Kwenye Msingi Wa Hisia

Lissu ameyasema hayo leo Septemba 24,2025, katika siku ya pili ya mawasilisho yake ya mwisho mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa Aprili 3, 2025, katika mkutano wa Chadema jijini Dar es Salaam, alitoa maneno yaliyoonyesha nia ya kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Miongoni mwa maneno ambayo upande wa mashtaka unadai Lissu aliyatoa ni: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli… kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana.”

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, maneno hayo ndiyo yanayotumiwa na upande wa Jamhuri kuonyesha madai ya nia ya Lissu ya kuchochea umma kuzuia uchaguzi na kutishia Serikali.

Hata hivyo, katika mawasilisho yake ya mwisho, Lissu amepinga tafsiri hiyo akisema ushahidi uliotolewa mahakamani haujaonyesha kwamba maneno hayo yalikuwa na nia ya kufanya kitendo cha uhaini kinachotambuliwa na sheria.

Amesema kati ya mashahidi 17 waliotoa ushahidi kwa upande wa mashtaka, ni mashahidi wanne pekee waliotoa ushahidi unaohusiana na madai ya nia ya kuchochea umma kuzuia uchaguzi.

Ametaja mashahidi hao kuwa George Bagemu, Inspekta John Kahaya, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Amini Mahamba na PW17 ambaye ni shahidi wa siri.

Kwa mujibu wa Lissu, watatu kati ya mashahidi hao ni polisi, huku mmoja akiwa si polisi. Amesema pia watatu kati yao hawakuwapo kwenye mkutano ambao maneno hayo yanadaiwa kutamkwa.

Lissu amesema PW17 ndiye shahidi pekee aliyekuwepo kwenye mkutano huo na aliyedai kuyaona na kuyasikia maneno hayo. Aidha, amesema shahidi huyo ni mwandishi wa habari ambaye alieleza kuwa ndiye aliyerusha matangazo ya mkutano huo.

Kutokana na hilo, Lissu amehoji msingi wa ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu nia yake, akisema kesi hiyo imejengwa kupitia ushahidi wa mashahidi ambao, kwa sehemu kubwa, hawakuwa kwenye eneo la tukio.

Akirejea ushahidi wa PW1, Lissu amesema shahidi huyo alikiri wakati wa kuhojiwa na upande wa utetezi kwamba katika maneno yanayodaiwa kutamkwa hakukuwa na neno “Serikali”, “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”, wala majina ya Rais Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Isdor Mpango.

Amesema pia hakuna mahali ambapo Halmashauri za Temeke, Kinondoni au Ilala zilitajwa.

Kwa msingi huo, Lissu amehoji namna ambavyo upande wa mashtaka umefikia hitimisho kwamba maneno hayo yalilenga kuitishia Serikali.

Amesema PW1 alidai maneno hayo yanaweza kuunda kosa la uhaini, lakini alikiri kwamba baadhi ya maneno hayo hayajaainishwa katika kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu kinachotumika katika shtaka dhidi yake.

Lissu amesema baada ya PW1 kutoa tafsiri hiyo, hoja kwamba maneno hayo yanaweza kuunda uhaini iliendelea kujitokeza katika ushahidi wa mashahidi wengine wa polisi.

“Nilichotaka kusema ni kwamba kesi kwenye shtaka hilo imejengwa kwenye hisia. Serikali haijatajwa mahali popote, viongozi hawajatajwa mahali popote, kwa hiyo ni imani yao. Kesi imejengwa kwenye msingi wa hewa,” amesema.

Lissu pia amehoji msingi wa nadharia kwamba kuvuruga uchaguzi ni uhaini kwa sababu uchaguzi unapaswa kufanyika kwa mujibu wa Katiba.

Amesema upande wa utetezi umeeleza kuwa nia yake ilikuwa kuitisha mkutano wa watia nia kutoka nchi nzima kwa ajili ya kuelimishana kuhusu msimamo wa Chadema wa “No Reform, No Elections”.

Kwa mujibu wa Lissu, ushahidi wake kuhusu suala hilo upo katika kurasa za 589 hadi 590 za kumbukumbu za kesi na kwamba msimamo huo uliungwa mkono pia na mashahidi wa pili, wa tatu na wa nne wa upande wa utetezi.

Katika hoja nyingine, Lissu amehoji iwapo maneno anayodaiwa kuyatamka yanaweza kuunda kosa lolote linalotambuliwa na sheria za Tanzania.

Amesema upande wa mashtaka haujafafanua maana ya “kuvuruga uchaguzi”, “kuhamasisha uasi”, “kuzuia uchaguzi” wala “kukinikisha”, na haujaeleza kwa nini maneno hayo yanapaswa kuunda kosa la jinai.

“Si wajibu wangu kisheria kama mshtakiwa kuyatolea ufafanuzi na kusema kwa nini ni makosa. Ni wajibu wao na hauhamii kwangu,” amesema.

Lissu amesema uhaini unatakiwa kutambuliwa kwa mujibu wa sheria na si kwa tafsiri ya mashahidi.

Ameielekeza Mahakama kwenye kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu, akisema hicho ndicho kifungu kinachofafanua matendo yanayoweza kuunda kosa la uhaini.

Kwa hiyo, amehoji iwapo maneno anayodaiwa kuyasema yanaingia katika matendo yaliyoainishwa na kifungu hicho.

“Je, kwenye haya maneno ninayodaiwa kusema, yametajwa kwenye hii list ya matendo 10 ambayo ukiyafanya yanatengeneza uhaini? Waheshimiwa Majaji, kwenye haya maneno ambayo nimeyasema, maneno yote hayapo,” amesema.

Kesi hiyo sasa ipo katika hatua ya mawasilisho ya mwisho, ambapo pande zote zinawasilisha hoja zao kabla ya jopo hilo la Majaji watatu kutoa uamuzi kwa mujibu wa sheria.

Our Correspondent Avatar