Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amewaambia majaji wanaosikiliza kesi ya uhaini inayomkabili kuwa wasisite kutoa hukumu inayostahili kosa la uhaini iwapo wataona ushahidi uliowasilishwa mahakamani unathibitisha kuwepo kwa kosa hilo.
Lissu amesema kinyume chake, iwapo majaji wataona hakuna uhaini uliothibitishwa, wasiwe na hofu ya kusema kuwa hana hatia, akisisitiza kuwa katika shtaka la uhaini hakuna kosa dogo ambalo mshtakiwa anaweza kuhukumiwa iwapo shtaka kuu litashindwa kuthibitishwa.“Kosa la uhaini halina kosa dogo, halina kosa ambalo ukishindwa kuthibitisha uhaini unadhibiwa kwa kosa dogo.“Mzigo ambao mnakabiliwa mabegani mwenu ni kuamua kama kwa ushahidi huu kuna uhaini. Kama mkiona kuna uhaini msiogope. Kama mnaamini kuna uhaini hapa, toeni hukumu inayostahili uhaini.“Na kama hakuna uhaini, msiogope kusema kwamba mshtakiwa hana hatia. Hakuna kosa dogo kwenye uhaini na kama ushahidi haufiti, ondoeni. Huo ni mzigo wenu peke yenu,” amesema Lissu wakati akihitimisha mawasilisho yake ya mwisho leo.Kauli hiyo imekuja baada ya Lissu kutumia sehemu kubwa ya mawasilisho yake kuichambua hoja ya upande wa mashtaka, akisisitiza kuwa ushahidi unapaswa kuangaliwa kwa ujumla wake na pia kuchambuliwa kipande kwa kipande ili kubaini iwapo unathibitisha shtaka linalomkabili.“Waheshimiwa majaji, ushahidi unapaswa kuchambuliwa vyema, kila mmoja kiundani. Nimeuzungumzia ushahidi wa upande wa mashtaka kwa ujumla wake na vipande vipande vyake. Nimeirejea kesi ya Nguza Viking na Oscar Lwela na ndivyo nilivyofanya, waheshimiwa majaji.”Lissu aliwaambia majaji kuwa swali muhimu wanalopaswa kujiuliza ni namna ushahidi wa pande zote mbili unavyolinganishwa.“Swali muhimu la kujiuliza ni je, huu ushahidi unalinganishwaje?”
Akizungumzia mashahidi wa utetezi, Lissu aliwataja DW1 ambaye ni mwanaharakati anayejulikana kwa masuala ya demokrasia na haki za binadamu, DW2 ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema, DW3 Amani Golugwa, DW4 Brenda Rupia na DW5 John Wegesa Heche.
“Waheshimiwa majaji, hao ndio walikuja kutoa ushahidi mbele yenu, watu wa maana katika siasa na uongozi wa nchi hii, sio watu wa mafichoni, watu wa maana kabisa,” amesema.Lissu alisema mashahidi hao walitoa ushahidi kuhusu matukio ya Aprili 3, 2025, lakini pia walieleza mazingira na muktadha wa kisiasa ambao, kwa mujibu wake, ni muhimu katika kuelewa maneno yanayodaiwa kuwa ya kihaini.
Alisema mashahidi wa utetezi waliieleza mahakama uzoefu wao binafsi kuhusu masuala ya siasa, demokrasia na matukio waliyowahi kukutana nayo, ikiwamo kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Waheshimiwa majaji, viongozi wote hawa waliambia mahakama hii kile ambacho hawakuambiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka, context. Hayo maneno yalizungumzwa katika mazingira gani na kwanini?”
Lissu alikiri kuwa mashahidi wa utetezi walikuwa na maslahi katika kesi hiyo, lakini akasema maslahi hayo hayakuwa sababu ya kukataa ushahidi wao kwa kuwa walikuwa wakitaka haki itendeke kwa mwenyekiti wao.
“Mwenyekiti wao yuko ndani anashtakiwa kwa kesi ya uhaini. Ni kiongozi gani ataona mwenyekiti wao yuko ndani na hawakuwa na maslahi? Walikuja kwa sababu wanataka haki na ukweli.”
Akiirejea kesi ya Goodluck Kyando, Lissu alisema Mahakama ya Rufani ilieleza kuwa kila shahidi anastahili kupewa uzito wa ushahidi wake isipokuwa pale ambapo kuna sababu za kutosha za kuukataa.
Akauliza:“Swali langu, kati ya ushahidi wa viongozi hawa na wahalifu hawa na mapolisi hawa, mahakama inatakiwa iamini ushahidi upi?”Hata hivyo, Lissu alisisitiza kuwa hamaanishi kwamba ushahidi wa mashahidi wa utetezi hauna dosari yoyote.
“Kwa Mungu huko ndio ushahidi unakuwa spotless, lakini duniani hapa ni ushahidi wa binadamu, hivyo dosari hazikosekani.”
Alitoa mfano wa baadhi ya mashahidi wa utetezi ambao, alisema, walihojiwa kwa kina wakati wa cross-examination na udhaifu wa baadhi ya majibu yao ukaibuliwa.
Lissu alisema hata hivyo dosari hizo hazikuhusu mambo ya msingi yanayoamua kesi hiyo.Kwa kurejea kesi za Nguza Viking, Babu Seya, Mohamed Haruna na Vitalis Joseph, Lissu aliwasilisha hoja kuhusu namna mahakama inavyopaswa kuangalia contradictions na discrepancies katika ushahidi.
Kwa mtazamo wake, dosari hizo haziwezi kuondoa ushahidi wa msingi iwapo sehemu muhimu ya ushahidi bado inaendana na kuthibitisha hoja inayowasilishwa.
“Kwa ushahidi huu hakuna ushahidi wa kumfunga mshtakiwa, badala yake kuna ushahidi wa kutosheleza kumuachia mshtakiwa,” amesema.
Lissu pia alizungumzia kile alichokiita mashaka makubwa katika namna upande wa mashtaka ulivyowasilisha hotuba yake ya Aprili 3, 2025.Alidai kuwa upande wa mashtaka ulichagua baadhi ya maneno na kuyaondoa mengine katika hotuba hiyo, jambo aliloliita cherry picking.
Kwa mujibu wa Lissu, alama za nukta tatu katika baadhi ya sehemu za hati ya mashtaka zinaonesha kuwa kuna maneno yaliyoachwa nje ya nukuu.
“Hayo ndio maneno mtu asiye makini ataona shida inaanza. Kabla ya neno la kwanza kuna zile doti tatu. Zina maana kwamba kulikuwa na maneno kabla.”
Lissu alihoji sababu ya kuondolewa kwa maneno hayo na kusema mahakama inapaswa kujiuliza yalikuwa yanasema nini na kwa nini hayakuingizwa katika hati ya mashtaka.Alisema muktadha mzima wa hotuba hiyo ungeweza kubadilisha namna maneno yanayolalamikiwa yanavyoeleweka.
“Ushahidi wa utetezi umetupatia missing context, hicho ambacho upande wa mashtaka haukutaka kijulikane kwa kunyofoa nyofoa maneno na kimejulikana kwa sababu ya ushahidi wa utetezi.”
Akaongeza:“Once it is understood, haya maneno yanayolalamikiwa kuwa ni ya kihaini yanapoteza hiyo maana mbaya yaliyopewa na upande wa mashtaka.”
Lissu pia alipinga uzito wa ushahidi unaohusiana na video inayodaiwa kuwa na hotuba hiyo, akisema upande wa mashtaka uliahidi kuleta video hiyo lakini haukuwasilisha video aliyodai kuwa ndiyo ingethibitisha shtaka.
Alisema mashahidi mbalimbali walitoa muda tofauti kuhusu urefu wa video hiyo.
“PW17 aliyerekodi na kuirusha anasema video yake ina karibu saa tatu. Sasa hapa ni ipi ya kwenda nayo? Hizi ni za upande wa mashtaka, kuna version sita na hamjaona hata moja. Mtaenda na version ipi?”
Lissu alisema tofauti hizo zinaibua swali kuhusu video ipi mahakama inapaswa kuamini.“Ni upande wa mashtaka ambao ulikuwa na wajibu wa kuthibitisha juu ya video. Hawajathibitisha video yoyote.”
Katika hoja nyingine, Lissu alipinga namna kesi hiyo ilivyofunguliwa, akisema baadhi ya masuala yanayohusu chama cha siasa na viongozi wake yana taratibu za kiutawala chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Alisema Chadema ni chama kinachotambuliwa kisheria na kwamba masuala yanayohusu uendeshaji wake na viongozi wake yanapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa, ikiwemo kifungu cha saba alichokitaja mahakamani.
Baada ya kumaliza hoja hizo, Lissu alitoa maneno yake ya mwisho kwa majaji, akiwashukuru kwa kumpa nafasi ya kujieleza na kujitetea katika kesi hiyo.
“Iko hivi, tulivyoanza niliijulisha Mahakama kwamba kesi ya uhaini sio kesi ya Rais, na nafikiri nikisema hapa hata nyie mnajua, ukiachia mbali siasa zangu.
“Pamoja na magumu yote ya kesi hii, mmefanya kazi nzuri, mmetupa nafasi ya kujieleza, mmenipa nafasi ya kujitetea, mmekuwa wavumilivu sana, mmefanya kazi nzuri.
“Nilitaka nisimalize bila kusema hayo. Nilitaka niseme pengine tunaweza tusikutane tena kwenye mazingira haya, nani anayejua kesho.
“Nilitaka nimalize bila kuacha kusema haya, na nafikiri hawa mawakili wa Serikali wamepambana. Nafikiri niwape pongezi zao na nawatakieni kila la kheri.”
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho, Septemba 29, 2026, ambapo upande wa Jamhuri unatarajiwa kufanya mawasilisho yake ya mwisho.
Lissu anakabiliwa na Kesi ya Uhaini Na. 19605 ya mwaka 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam. Shtaka hilo linahusishwa na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).
Upande wa mashtaka unadai kuwa Aprili 3, 2025, Lissu alitamka maneno yaliyolenga kuhamasisha umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, likiwamo dai kwamba alikusudia “kuzuia uchaguzi,” “kuhamasisha uasi” na “kuvuruga uchaguzi.”Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, wakati wa shughuli za Chadema zilizokuwa zikihusisha kampeni ya kauli ya “No Reforms, No Election”. Alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo








