Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu kuwa msimamo wa chama chake wa “No Reform, No Election” haukuwa mpango wa kufanya uhaini wala kupindua Serikali, bali ulikuwa mkakati wa kisiasa wa kushinikiza mabadiliko ya Katiba na mfumo wa uchaguzi kwa njia za amani na kidemokrasia.

Lissu ametoa kauli hiyo leo Agosti 24, 2026 wakati akiendelea kujitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini inayomkabili, akieleza kwa kina mchakato wa kisiasa uliozaa msimamo huo na matukio yaliyotangulia mkutano wa Aprili 3, 2025 ambao upande wa mashtaka umeuhusisha na mashtaka dhidi yake.
Amesema suala la uchaguzi na Katiba lilikuwa sehemu ya mjadala mpana ndani ya CHADEMA, na kwamba msimamo wa “No Reform, No Election” haukuanzishwa na yeye binafsi.
“No Reform, No Election sio maneno ya Lissu, huo ni msimamo wa Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,” amesema.
Lissu amesema baada ya kifo cha Rais John Magufuli na kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, aliondoka Tanzania kwa sababu za kiusalama na baadaye akarejea baada ya Serikali kutoa ahadi kuhusu mazingira ya kisiasa.
Amesema Februari 17, 2022, wakati Rais Samia akiwa Ulaya, alipokea ujumbe kwamba Rais huyo alitaka kukutana naye.
Kwa mujibu wa Lissu, wakati huo Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alikuwa gerezani kwa takribani miezi sita.
Amesema viongozi wenzake walimshauri kutumia nafasi hiyo kujadili suala la Mbowe na masuala ya Katiba.
Lissu amesema pia aliomba Serikali itangaze kuwa yeye na viongozi wengine waliokuwa nje ya nchi wangekuwa salama endapo wangerudi Tanzania.
Baadaye, amesema Serikali ilitoa tamko kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Hamad Masauni, na ndipo aliporejea nchini.
Amesema baada ya kurejea kulianza mchakato wa mazungumzo na Serikali kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, amesema CHADEMA ilipoomba Serikali iweke msimamo wake kwa maandishi, ilipokea majibu yaliyokataa mapendekezo yao.
“Tukasema kama wanakataa hayo maridhiano ya kazi gani?” amesema.
“Tukaamua kampeni ya Katiba iwe ya nchi nzima”
Lissu amesema baada ya kuona mazungumzo hayakuwa na matokeo yaliyotarajiwa, CHADEMA iliamua kuendesha kampeni ya kudai mabadiliko ya Katiba nchi nzima.
Amesema wakati huo ndipo hali ya kisiasa ilianza kuwa ngumu zaidi, huku akidai baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA wakikabiliwa na vitendo vya kutekwa na kuuawa.
Amesema pia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 uliibua malalamiko ndani ya chama hicho baada ya wagombea wa CHADEMA kuenguliwa katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Lissu, matukio hayo yalichangia kuimarisha msimamo wa chama wa kutaka mageuzi kabla ya uchaguzi mkuu.
Amesema tarehe 3 Desemba 2024 ndipo kauli ya “No Reform, No Election” ilipoanza kujadiliwa ndani ya chama na tarehe 10 Desemba 2024 ikatangazwa hadharani.
Lissu aliendelea kuiambia Mahakama kuwa msimamo huo haukuwa uamuzi wake binafsi.
Amesema tarehe 20 Januari 2025, Baraza Kuu la CHADEMA lilijadili ajenda hiyo na kuupitisha msimamo wa “No Reform, No Election”, kisha kupendekeza uende kwenye Mkutano Mkuu wa chama.
Amesema Mkutano Mkuu uliujadili na kuupitisha msimamo huo kabla ya uchaguzi wa viongozi wa chama.
Lissu amesema Februari 22, 2025 alitangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CHADEMA, lakini msimamo huo ulikuwa tayari umeidhinishwa na chama kabla hajachaguliwa.
Kwa hiyo, amesema kazi iliyofuata ilikuwa kuandaa namna ya kuutekeleza.
“Tulisema tutahamasisha watu kwa njia za kidemokrasia”
Lissu amesisitiza kuwa utekelezaji wa msimamo huo haukuhusisha vurugu wala mapinduzi.
Amesema mpango wa CHADEMA ulikuwa kuzunguka nchi nzima kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kutumia njia za kidemokrasia kudai mabadiliko.
“Njia za amani. Hatukusema tunaenda kuchoma mtu au kupiga mtu yeyote. Tulisema tunatembea nchi nzima kuwaasa Watanzania wachukue hatua za kuendesha nchi kidemokrasia,” amesema.
Amesema chama pia kilipanga kukutana na makundi mbalimbali, yakiwemo taasisi za dini, Shura ya Maimamu, TEC, Baraza la Kikristo Tanzania, Jukwaa la Wahariri Tanzania na Baraza la Mawakili la TLS.
Amesema pia walitafuta ushauri na uungwaji mkono kutoka nje ya Tanzania, akitaja safari yake ya Kenya ambako alikutana na marehemu Raila Odinga na safari ya Uganda ya Machi 25, 2025.
“Nchi hii si kisiwa. Nchi hii ina majirani. Tukasema tutaenda kutafuta marafiki watakaotusaidia kwenye hili,” amesema.
-Aprili 3, 2025: Mkutano uliozaa kesi-
Lissu amesema ziara za CHADEMA za kuhamasisha wananchi zilipofikia Iringa, alipokea taarifa kuwa chama kilikuwa kikijiandaa na mkutano utakaowakutanisha na watia nia wa uchaguzi mkuu.
Amesema alirudi Dar es Salaam Aprili 1, 2025 na Aprili 3 akahudhuria mkutano wa watia nia wa CHADEMA katika makao makuu ya chama.
Amesema yeye ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu kwa sababu alikuwa Mwenyekiti wa chama, lakini mkutano huo haukuandaliwa na yeye.
Kwa mujibu wa Lissu, mkutano huo uliandaliwa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA kupitia Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa.
Amesema video inayodaiwa kuwa na kauli zilizotumika katika kesi hiyo iliwekwa YouTube na Jambo TV, lakini yeye mwenyewe hakuwahi kuiona video hiyo yote.
-Sikuwa na mpango wa kufanya uhaini-
Lissu amekanusha kuwa shughuli za CHADEMA za kuhamasisha wananchi kuhusu “No Reform, No Election” zilikuwa sehemu ya mpango wa uhaini.
Amesema ziara zote za chama zilifanyika hadharani na kwamba hawakuwa wakipanga kwa siri.
“Mipango yetu hatukuwa tunaipanga kwa siri, hatukuwa tunapanga uhaini wala hatukuwa tunapanga kupindua Serikali,” amesema.
Kwa msingi huo, Lissu ameieleza Mahakama kuwa kile ambacho upande wa mashtaka unakiona kama mpango wa kuhamasisha wananchi kuvuruga uchaguzi, yeye anakiona kama kampeni ya kisiasa ya kushinikiza mabadiliko ya Katiba na uchaguzi.
-Lissu: “Kesi hii ni mgogoro wa kisiasa kuhusu uchaguzi”-
Lissu amesema kesi hiyo kwa uhalisia ni mgogoro wa kisiasa unaohusu uchaguzi wa Tanzania.
Amesema mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka walizungumzia kauli zake kuhusu uchaguzi, huku nyaraka za D1 hadi D16 pia zikihusisha masuala ya uchaguzi.
Amesema baadhi ya mashahidi walieleza kuwa video ya Jambo TV inayodaiwa kuwa na kauli zake ilikuwa na urefu wa takribani saa mbili hadi tatu.
Lissu amehoji kwa nini Mahakama izingatie vipande vya maneno vilivyomo kwenye hati ya mashtaka bila kuangalia maudhui ya hotuba nzima.
Amesema masuala ya Katiba na uchaguzi ni mambo ambayo yamekuwa yakijadiliwa nchini kwa muda mrefu na kwamba matatizo katika mfumo wa uchaguzi yamekuwa yakionyeshwa katika ripoti mbalimbali.
-Masuala ya uchaguzi si ya kuchezea-
Lissu amesema masuala ya uchaguzi na Katiba yakiachwa bila kutatuliwa yanaweza kusababisha migogoro na maafa.
Amehusisha hoja hiyo na historia ya Tanzania na Muungano, akisema hata Tume ya Jaji Nyalali iliangazia historia ya mfumo wa kisiasa na matukio ya umwagaji damu yaliyohusishwa na siasa.
Ametaja pia Tume ya Jaji Chande, akisema ripoti yake ilihusisha matukio ya mwaka 2025 na historia ndefu ya migogoro kuhusu uchaguzi na madai ya Katiba.
Kwa mujibu wa Lissu, CHADEMA ilisema ilikuwa ikijaribu kuzuia maafa kwa kushinikiza mageuzi kabla ya uchaguzi.
–Lissu aeleza kwa nini anaona kesi ina mizizi ya kisiasa–
Katika sehemu nyingine ya utetezi wake, Lissu ameeleza historia yake ya kukamatwa na kufunguliwa kesi katika tawala mbalimbali, akisema kesi ya sasa ni mwendelezo wa kile anachokiona kama matumizi ya vyombo vya dola dhidi yake kutokana na misimamo yake ya kisiasa.
Ametaja kesi za kipindi cha Mkapa, Kikwete na Magufuli, pamoja na kukamatwa kwake mara kadhaa katika utawala wa Samia.
Amesema pia amekaa gerezani kwa miezi 16 na anaelekea miezi 17, akidai ni kipindi kirefu zaidi ambacho amewahi kukaa gerezani.
-Taasisi za Afrika nazo zatajwa–
Lissu pia ameitaja orodha ya taasisi za kikanda na kimataifa ambazo amesema zililaani kukamatwa kwake na mashtaka ya uhaini.
Ametaja vyama vya wanasheria vya Afrika Mashariki, SADC, Afrika, Zambia, Kenya na Tanganyika, pamoja na Uganda Law Society, Amnesty International na Tume ya Wanasheria Duniani.
Amesema Tume ya Haki za Binadamu na Haki za Wananchi ya Afrika ilifanya kikao cha dharura Julai 30, 2025 na kupitisha azimio kuhusu hali ya haki za binadamu Tanzania.
Utetezi wa Lissu leo umeingia siku ya pili na anatarajia kumaliza utetezi siku ya Jumatano Agosti 26, 2026.
Kesi imeahirishwa mpaka siku hiyo kwa
Kuzingatia kwamba kesho Jumanne Agosti 25, 2026 ni siku ya mapumziko ambapo Waislam kote nchini wanaadhimisha Sikukuu ya Maulid.