, ,

Maandamanao Ufaransa Yageuka Ghasia, Zaidi ya Waandamanaji 1000 Wakikamatwa

Victor Kayanda Avatar

Maandamano yanayoendela nchini Ufaransa kupinga changamoto katika mfumo wa elimu na kupanda kwa gharama ya maisha yamegeuka kuwa ghasia, huku zaidi ya waandamanaji 1,200 wakikamatwa na majengo kadhaa kuchomwa moto na kuharibiwa.

Serikali ya Ufaransa imesema kumekuwa na ongezeko la vurugu wakati takriban watu 550,000 walipojitokeza katika maandamano yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Katika jiji la Lyon, ofisi ya utalii iliteketezwa kabisa baada ya kuchomwa moto, huku jengo la halmashauri ya jiji la Limoges pia likiteketezwa moto. Moto huo ulisababisha mnara wa kihistoria wenye umri wa miaka 143 kuporomoka

Katika mji mkuu wa Paris, maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika maeneo mbalimbali, huku polisi wakitumia vitoa machozi na magari ya kunyunyizia maji kutawanya umati katika uwanja wa Place de la République.

Hali ilikuwa vivyo hivyo katika jiji la Marseille, ambapo waandamanaji waliingia kwa nguvu katika jengo la halmashauri ya mji na kuwasha vizuizi vya moto barabarani. Picha zilizosambazwa pia zilionyesha watu wakilishambulia jengo la benki.

Inaripotiwa kuwa kijana mmoja alipoteza mkono baada ya kulipukiwa na guruneti, huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Laurent Nuñez, akisema visa vya uporaji na majaribio ya uporaji vilirekodiwa katika miji kadhaa.

Maandamano hayo yanafuatia wiki kadhaa za malalamishi ya wanafunzi na wananchi kuhusu hali ya maisha na changamoto zinazokumba sekta ya elimu.

Wanafunzi wamekuwa wakitaka serikali kuongeza uwekezaji katika shule, wakilalamikia uhaba wa walimu na wafanyakazi wengine, msongamano wa wanafunzi madarasani pamoja na uchakavu wa majengo ya shule.

Hata hivyo, maandamano ya hivi punde yamepanuka na kujumuisha malalamishi mapana kuhusu gharama ya maisha na huduma za umma, hali inayoongeza shinikizo kwa serikali ya Ufaransa kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wananchi.

 

Our Correspondent Avatar