
Kauli hiyo ya Brenda imeibuka wakati Jamhuri ikiendelea kumhoji kwa maswali ya dodoso, ikimchunguza kuhusu matamshi ya Lissu, msimamo wa Chadema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 na maana ya kauli ya “No Reforms, No Elections.”
Alipoulizwa kama alimuunga mkono Lissu kwa kukubaliana na maneno aliyoyasema, Brenda alijibu kuwa si tu alimuunga mkono wakati huo, bali “mpaka leo” bado anakubaliana naye.
Katika mahojiano hayo, Brenda pia alikataa kwamba Chadema ilisusia uchaguzi wa mwaka 2025, akieleza kuwa kauli ya “No Reforms, No Elections” ililenga kushinikiza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi. Miongoni mwa mabadiliko aliyoyataja ni kutaka Rais asiwe na mamlaka ya kumteua Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi na kutaka wasimamizi wa uchaguzi katika kata wasiwe watendaji wa kata.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu iwapo kuvuruga uchaguzi mkuu kungekuwa ukiukaji wa Katiba au kama sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu kitendo hicho, Brenda alisema hajui. Kauli hiyo imekuja wakati Jamhuri ikijaribu kuhusisha ushahidi wake na hoja zinazohusu Katiba, sheria za uchaguzi na matamshi yaliyomo katika hati ya mashtaka.
Brenda, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, pia alikabiliwa na maswali kuhusu taaluma yake, akieleza kuwa amesomea uhasibu na kwamba yeye si mwandishi wa habari. Hata hivyo, alieleza kuwa moja ya majukumu yake ni kusimamia mawasiliano ya chama na umma pamoja na kuwaalika waandishi wa habari kwenye mikutano ya Chadema.
Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Brenda alieleza uelewa wake kuhusu “Uhaini” kuwa ni kutaka kuipindua au kuisaliti nchi, huku akisema haoni maneno “uasi” na “kukinikisha” kama kosa. Alipoulizwa iwapo kauli hiyo ina msingi wa kisheria, alisema yeye si mtaalamu wa sheria.