Shahidi wa Kificho Asema Ana Hofu Kutoa Ushahidi Hadharani Katika Kesi ya Uhaini ya Lissu

Shahidi wa kificho katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameieleza Mahakama Kuu kuwa ana hofu ya kutoa ushahidi wake hadharani, akisema suala hilo ni “very sensitive” na kwamba wafuasi wa chama hicho wanaweza kuwa na hasira naye licha ya kuwa na mahusiano mazuri na Viongozi wakuu wa Chadema.

Shahidi wa Kificho Asema Ana Hofu Kutoa Ushahidi Hadharani Katika Kesi ya Uhaini ya Lissu

Kauli hiyo imetolewa wakati shahidi huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye ni Muislamu, akijibu maswali ya Lissu baada ya mawakili wa Serikali kumaliza kumuhoji. Utambulisho wa shahidi huyo umefichwa na Mahakama kwa sababu za ulinzi.

Kabla ya kufikia hatua hiyo, shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa ni mwandishi wa habari anayefanya kazi katika Jambo TV tangu mwaka 2023, akiwa na jukumu la kupiga picha na kurekodi video. Amesema ana Diploma ya Uandishi wa Habari kutoka Dar es Salaam School of Journalism, DSJ, aliyopata mwaka 2023.

Shahidi huyo amesema Aprili 3, 2025 alitumwa na bosi wake, John Marwa, kwenda kuripoti mkutano wa CHADEMA uliofanyika katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam. Amesema yeye na wenzake walirekodi na kurusha mubashara mkutano huo kupitia YouTube kwa jina la Jambo TV.

Amesema miongoni mwa viongozi waliozungumza katika mkutano huo walikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu John Mnyika, huku akidai walizungumzia msimamo wa “No Reform, No Election”.

Awali, mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili Thawabu Issa walimuhoji shahidi huyo kuhusu taaluma yake, kazi yake Jambo TV na tukio la Aprili 3, 2025.

Wakili Thawabu Issa: Iambie Mahakama unajishughulisha na nini?

Shahidi: Najishughulisha na kazi ya uandishi wa habari.

Wakili: Shughuli hizo unazifanyia wapi?

Shahidi: Jambo TV.

Wakili: Upo hapo tangu lini?

Shahidi: Tangu mwaka 2023.

Wakili: Majukumu yako ni yapi?

Shahidi: Ni kuchukua picha na video.

Wakili: Ujuzi wako ni nini?

Shahidi: Nina Diploma ya Uandishi wa Habari.

Wakili: Uliipata wapi na mwaka gani?

Shahidi: Niliipata katika Chuo cha Uandishi wa Habari, DSJ, mwaka 2023.

Wakili: Unaweza kuiambia Mahakama unatumia vifaa gani?

Shahidi: Nachukua matukio hayo kwa kutumia kamera aina ya Sony NX.

Wakili: Kamera hiyo unaitumia kwenye matukio gani?

Shahidi: Kwenye matukio ya video pekee.

Wakili: Nikurejeshe tarehe 3 Aprili 2025. Siku hiyo nini kilitokea?

Shahidi: Siku hiyo nilipewa majukumu na bosi wangu, mimi na wenzangu, kwenda kwenye tukio la CHADEMA lililokuwa linafanyika katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni.

Wakili: Bosi wenu ni nani?

Shahidi: John Marwa.

Wakili: Ulikuwa na nani?

Shahidi: Nilikuwa na watu watano, mimi, P1 pamoja na wenzangu wengine.

Wakili: Nini kiliendelea kwenye mkutano huo?

Shahidi: Tulipofika tulifunga vifaa vyetu kwa ajili ya mkutano huo.

Wakili: Unaweza kutuambia hali ilikuwaje eneo hilo?

Shahidi: Wakati tunafika eneo husika tulikuta wanachama wa CHADEMA, waandishi wa habari, lakini pia viongozi wengine wakuu wa CHADEMA.

Wakili: Mlikuwa mkiandaa kurusha matukio hayo mubashara kwa kutumia njia gani?

Shahidi: Tulikuwa tunarusha kutoka kwenye kamera na kupeleka mubashara YouTube.

Wakili: Huko YouTube ulikuwa unarusha kwa jina gani?

Shahidi: Jambo TV.

Wakili: Mkutano ulikuwa wa nini?

Shahidi: Ulikuwa mkutano wa watia nia wa CHADEMA kwa ajili ya uchaguzi.

Wakili: Unaweza kuwakumbuka waliozungumza?

Shahidi: Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti John Heche na John Mnyika.

Wakili: Kwa namna unavyokumbuka, miongoni mwa wazungumzaji unaweza kukumbuka baadhi ya maneno yaliyozungumzwa?

Shahidi: Naweza kuyakumbuka, lakini kwa ujumla walizungumzia “No Reform, No Election” na namna watakavyoingia kwenye uchaguzi.

Wakili: Walisema wataingia kwenye uchaguzi kwa namna gani?

Shahidi: Kwamba bila mabadiliko hawawezi kuingia kwenye uchaguzi na Mwenyekiti alizungumzia namna watakavyoweza kuzuia uchaguzi.

Wakili: Kama unakumbuka baadhi ya maneno ya Mwenyekiti kuhusiana na uchaguzi?

Shahidi: Nakumbuka machache tu. Alizungumza maneno mengi lakini alisema, “Tutazuia huu uchaguzi, tutakinukisha.”

Wakili: Umesema ulikuwa unatumia vifaa aina ya Sony NX. Unaweza kutuambia hali ya vifaa hivyo siku hiyo?

Shahidi: Hali ya vifaa ilikuwa nzuri.

Wakili: Malengo ya kurusha matukio haya yalikuwa nini?

Shahidi: Malengo yalikuwa ni kuuabarisha umma.

Wakili: Zoezi lenu la kuchukua video na kuanza kurusha lilichukua muda gani?

Shahidi: Masaa matatu.

Wakili: Nini kiliendelea baada ya kurusha?

Shahidi: Tulirusha tukio zima. Baada ya hapo waandishi wa habari tuliambiwa tutoke nje ili kuwapisha wao kuzungumzia mambo yao ya ndani.

Wakili: Bwana P, tarehe 7 Aprili 2025 unakumbuka kitu gani kilitokea?

Shahidi: Siku hiyo nilikuwa Dodoma kikazi. Wakati nikiwa huko nilipokea simu kutoka kwa bosi wangu John Marwa, akiniambia niende kituo cha polisi kwa ajili ya kukabidhi kadi ya kamera niliyofanyia kazi ya mkutano wa CHADEMA wa tarehe 3 Aprili 2025.

Wakili: Ulipata maelekezo hayo, nini kilifuatia?

Shahidi: Nilielekea kituo cha polisi pale Dodoma nikakabidhi kwa polisi ambaye alinisimamia wakati naandika maelezo.

Wakili: Tarehe 3 Aprili 2025, kama unakumbuka, Tundu Lissu alikuwa kwenye muonekano gani?

Shahidi: Alikuwa kwenye mavazi ambayo rangi yake siifahamu lakini ni kombati.

Wakili: Kwa namna unavyokumbuka, yale maongezi kwenye ule mkutano yalikuwa yanazungumzia uchaguzi gani?

Shahidi: Wa Oktoba 2025.

Baada ya maswali hayo, mawakili wa Serikali walimaliza kumuhoji shahidi.

 

-Lissu aanza kumuhoji shahidi-

Baada ya upande wa Serikali kumaliza, Lissu alimhoji shahidi kuhusu uhusiano wake na Jambo TV na namna kituo hicho kilivyokuwa kikifuatilia shughuli zake za kisiasa.

Lissu: Ni kweli kwamba waandishi wa habari wa Jambo TV mmefanya kazi na mimi kwa muda mrefu sana?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Mmeendelea kutangaza mikutano yangu karibu nchi nzima?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Ni kweli kwamba Jambo TV imekuwa ikifunika mikutano yangu katika sehemu mbalimbali za nchi hii?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Hata niliporudi nchini kutoka Ulaya kwenye matibabu, Jambo TV mlinisindikiza nyumbani kwetu?

Shahidi: Sikumbuki vizuri.

Lissu: Kuna mpiga picha anaitwa Shadrack na Oscar unawakumbuka, ambao nimetembea nao mpaka nyumbani?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Hata siku nilipokamatwa Aprili 9, kule Mbinga, Ruvuma, waandishi wa habari niliokuwa nao walikuwa Shadrack Simba na Oscar?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Katika ziara zote hizo tumekuwa tukienda msafara mmoja?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Tumekuwa tukilala pamoja?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Tumekuwa tukikula pamoja?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Nikisema mimi pamoja na waandishi wa Jambo TV na bosi wenu John Marwa tumekuwa na mahusiano ya karibu sana, nitakuwa nimekosea?

Shahidi: Hapana, hujakosea.

Lissu: Katika kipindi chote ambacho tumekuwa tukifanya kazi pamoja, mmekuwa marafiki zangu?

Shahidi: Kweli.

Lissu aliendelea kumuuliza shahidi kama waandishi wa Jambo TV waliwahi kuogopa kuripoti mikutano yake na kama yeye au wafanyakazi wenzake waliwahi kutishiwa na wanachama au viongozi wa CHADEMA.

Lissu: Ni kweli kwamba wakati mwingine vyombo vingine vikiogopa ku-cover mikutano yangu, nyinyi hamjawahi kuogopa?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Mara nyingi nazungumzia mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025. Mliadhibiwa mara tu baada ya kurusha mkutano wangu?

Shahidi: Sikumbuki juu ya hilo.

Lissu: Kwa yote ambayo nimeyasema juu ya mahusiano yangu, naomba uwaeleze Waheshimiwa Majaji kama kuna mwanachama au kiongozi yeyote wa CHADEMA aliyekutishia au kukuahidi kukudhuru?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Kuna mfuasi wa CHADEMA aliyewahi kukutishia wewe au wafanyakazi wenzako wa Jambo TV?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Tangu siku uliporusha matangazo ya tarehe 3 Aprili 2025, kuna mtu yeyote au mamlaka yoyote ambayo umempa taarifa kwamba viongozi au wanachama wa CHADEMA wanakutishia wewe au wafanyakazi wenzako?

Shahidi: Hapana, sijafanya hivyo.

Katika sehemu iliyovuta hisia zaidi wakati wa mahojiano hayo, Lissu alimuuliza shahidi kama ana hofu au woga wa kutoa ushahidi wake wa kweli mbele ya Mahakama.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama una hofu au woga wowote wa kutoa ushahidi wako wa kweli hadharani?

Shahidi: Nina hofu ya kutoa ushahidi hadharani.

Lissu: Una hofu gani? Waeleze Waheshimiwa Majaji.

Shahidi: Kwa sababu hili suala liko very sensitive. Nyie viongozi wakuu mnaweza msiwe na shida lakini wafuasi wanaweza wakawa na hasira.

Lissu aliendelea kumuuliza shahidi kuhusu maelezo aliyowahi kuyatoa polisi, akitaka kujua kama baadhi ya mambo aliyoyasema Mahakamani yalikuwa pia katika maelezo hayo.

Lissu: Siku ya tarehe 3 Aprili 2025 ulipewa maagizo na bosi wako John Marwa kwenda ku-cover mkutano wa CHADEMA?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema wazungumzaji wakuu walikuwa Mwenyekiti Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu. Angalia kwenye hicho kielelezo, hayo maneno yapo yote?

Shahidi: Lipo jina lako peke yake.

Lissu: Leo ulipoulizwa kuhusu maneno yaliyotamkwa kwenye mkutano huo ulisema kulikuwa na maneno mengi lakini walikuwa wanazungumzia “No Reform, No Election”?

Shahidi: Ndiyo.

Lissu: Hayo maneno kuhusu namna wataenda kwenye uchaguzi kwenye maelezo yako yapo?

Shahidi: Hayapo.

Lissu pia alimuuliza kuhusu simu aliyodai kupokea kutoka kwa bosi wake Aprili 7, 2025.

Lissu: Kwenye ushahidi wako wa leo umesema tarehe 7 Aprili ulipigiwa simu na bosi wako John Marwa kwamba uende kituo cha polisi Dodoma. Hayo maneno yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi: Hayapo.

Lissu: Leo umesema kwenye hiyo simu uliambiwa uende kituo cha polisi Dodoma ukakabidhi kadi yenye mkutano wa CHADEMA. Hayo maneno yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi: Hayapo.

Lissu: Ulipofika makao makuu ya CHADEMA mlikuta wanachama wa CHADEMA na watu wengine lakini viongozi walikuwa hawajafika. Ni sahihi?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Kwa uliyoyaona, ni nani aliyekuwa akifanya maandalizi ya huo mkutano?

Shahidi: Sikulizingatia hilo.

Lissu: Mimi nilikuwa mmoja wa waliokuwa wakifanya hayo maandalizi?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Mtu akisema Mwenyekiti Tundu Lissu ndiye aliyealika na kufanya maandalizi ya mkutano huo, atakuwa anasema ukweli au anadanganya?

Shahidi: Atakuwa si sahihi.

Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu madai yanayomhusisha yeye na urushaji mubashara wa mkutano huo.

Lissu: Shahidi, nimeshtakiwa kwa uhaini, unajua?

Shahidi: Ndiyo.

Lissu: Kwa sababu inadaiwa kwamba mimi ndiye niliyerusha hayo matangazo mubashara na kuyaweka kwenye mitandao ya Jambo TV. Hiyo tuhuma ni ya kweli au si kweli? Je, mimi ndiye niliyeyarusha au wewe na watu wako ndio mliorusha?

Shahidi: Sisi kupitia wewe.

Lissu: Siku hiyo ambayo mnadai mlikuwa na kamera tatu, mimi niligusa moja wapo ya hizo kamera?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Mimi nilikuagiza wewe au wenzako kwamba mrushe hayo matangazo mubashara?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Nilikuagiza wewe au wenzako kwamba mrushe matangazo kwenye YouTube, Instagram na X?

Shahidi: Hapana.

Ushahidi wa shahidi huyo unakua ni wa shahidi wa 17 kati ya mashahidi 30 wa Jamhuri ambaye leo amehitimisha ushahidi wake.

Lissu ambaye leo Agosti 13, 2026 anatimiza siku 492 gerezani anashtakiwa kwa kosa la Uhaini kosa ambalo anadaiwa kulitenda mnamo mwezi Aprili 2025.

Alikamatwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Aprili 9,2025 na kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kufikishwa kwa mara ya kwanza Mahakama ya Kisutu Aprili 10, 2025.

Kesi imeahirishwa mpaka kesho Agosti 14,2026 ambapo Jamhuri wanatarajia kumleta shahidi wa 18.