Shahidi wa nne wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, Brenda Rupia, amemaliza kutoa ushahidi wake baada ya kuhojiwa kwa kina na upande wa Jamhuri kuhusu hotuba ya Lissu ya Aprili 3, 2025 na tafsiri ya baadhi ya kauli zilizotolewa katika mkutano huo.

Rupia, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA na alianza kutoa ushahidi wake Agosti 7, 2026, alimaliza ushahidi wake baada ya kukabiliana na maswali ya Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga, yaliyolenga kubaini uelewa wake kuhusu maana ya maneno kama “uasi”, “kuhamasisha uasi”, “kuzuia uchaguzi” na “kuvuruga uchaguzi”. Maswali hayo pia yaligusa ushahidi wake kuhusu madai ya kuwepo kwa njama ya kumpa Lissu sumu akiwa gerezani.
Katika sehemu hiyo ya ushahidi, Rupia alikiri kuwa anafahamu kwamba kutoa taarifa za uongo mtandaoni na kutoa ushahidi wa uongo chini ya kiapo ni makosa ya jinai. Hata hivyo, alipoulizwa kama kukamatwa kwa Lissu kulimpa yeye kinga ya kutokamatwa kwa makosa ya jinai, alijibu kuwa hakukuwa na kinga hiyo.
Kuhusu uchunguzi alioufanya juu ya taarifa za madai ya njama ya kumpa Lissu sumu, Rupia alisema alimtafuta mtu kwa simu na mtu huyo akathibitisha kuwa taarifa hizo alikuwa amezipata na zilikuwa za kweli.
Sehemu kubwa ya dodoso ilijikita kwenye hotuba ya Lissu, huku Katuga akimuuliza Rupia kama kauli kama “tutazuia uchaguzi” na “tutavuruga uchaguzi” ni sentensi zilizokamilika na zenye maana. Rupia alikubali kuwa zote ni sentensi kamili na zina maana.
Pia alikubali kuwa kuchoma vituo au kura, kuharibu mali za umma na vitendo vingine vya uhalifu vinaweza kuvuruga amani na kuzuia uchaguzi kufanyika.
Hata hivyo, alipoulizwa kauli ya Lissu kuhusu “kuhamasisha uasi” ililenga nini, alieleza kuwa ililenga “sheria kandamizi”.
Katika maswali hayo, Rupia pia alikiri kuwa CHADEMA inaamini katika demokrasia na kwamba Tanzania ina mfumo wa vyama vingi, huku akitambua kuwa uchaguzi mkuu unaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na mabadiliko ya Katiba ni mchakato. Alipoulizwa kuhusu kundi la wanachama wa G55 waliowahi kuhusishwa na msimamo wa chama kuhusu uchaguzi, Rupia alisema walikuwa wanachama wa CHADEMA na kwamba baadaye waliondoka baada ya kutofautiana na msimamo wa chama waliouona ukielekea kwenye uasi.
Baada ya kumaliza maswali ya Jamhuri, Lissu alimuuliza Rupia maswali ya kusawazisha ushahidi wake, hasa kuhusu tafsiri ya kauli alizotumia katika hotuba hiyo. Rupia alifafanua kuwa aliposema Lissu alielekeza namna ya kuzuia uchaguzi, alimaanisha kutoshiriki uchaguzi, akisema kwa kutoshiriki “tutakuwa tumeuzuia huo uchaguzi”.
Kuhusu madai kwamba Lissu alielekeza namna ya kuvuruga uchaguzi, alithibitisha kuwa alielekeza namna ya “kukinikisha”. Pia alieleza kuwa chama kinaweza kufanya shughuli zake sehemu yoyote na si lazima wafanyakazi wake wawe ofisini. Kwa kukamilika kwa ushahidi wake, Rupia anakuwa shahidi wa nne wa upande wa utetezi katika kesi hiyo, huku kesi ikiendelea na mashahidi wengine wa utetezi.
Kesi inaendelea ambapo shahidi wa tano Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche anatoa ushahidi wake