Kenya: Vijana wadai kupewa ksh.30 kabla wajisajili kama wapiga kura

Zoezi hilo la siku 20 lilitarajiwa kupata wapiga kura wapya milioni 4.5.

0

Idadi ndogo ya watu waliojitokeza kujisajili katika siku ya mwisho ya awamu ya pili ya Usajili wa Wapigakura wa Kitaifa Jumapili licha ya juhudi za mwisho za wawaniaji na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwataka watu wajitokeze kwa wingi kujisajili.

Kupuuza kujisajili kama mpigaji kura na madai kwamba vijana walikuwa wakisubiri kuhongwa ni miongoni mwa sababu kuu zinazotajwa kusababisha idadi ndogo iliyoshuhudiwa katika zoezi la siku 20 ambalo lilitarajiwa kupata wapiga kura wapya milioni 4.5.

“Ninahitaji kitu, unatarajiaje nizungumze na wewe bila chochote,” kijana mmoja mwenye umri wa miaka ishirini alisema, “Sichukui kadi ya kupiga kura, waambie wanaotaka tupige kura watupe kitu kidogo kwanza.”

Ikiwa ni siku ya mwisho ya usajili wa wapiga kura, watu wengi walitarajiwa kujitokeza lakini afisa wa IEBC alisema kuwa wengi watu waliokuwa kwenye foleni ni wale waliotaka kuhamisha eneo lao la kupigia kura na wachache sana waliojiandikisha.

Katika vituo mbalimbali jijini, kulikuwa na visa mbalimbali ambapo vikundi vya vijana vilikuwa vimekaa karibu na vituo vya kujiandikisha na kudai kiasi cha Sh30 ili kujiandikisha kama wapiga kura.

Kampeni ya kusajili wapiga kura wapya ilianza Januari 17 baada ya kampeni ya kwanza kufanyika kati ya Oktoba 4 hadi Novemba 5 mwaka jana kukamilika na kufaulu kuwasajili wapiga kura wapya milioni 1.52.

Awamu ya pili ya usajili wa Wakenya walioko ughaibuni  katika nchi za Amerika, Sudan Kusini na Ujerumani ilianza Januari 21 hadi Februari 6.

Zoezi hilo katika miji ya London nchini Uingereza, Canada na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) litaongezwa muda ili kuwapa makarani nafasi ya kusajili wapiga kura baada ya makarani wa usajili kuchelewa kuripoti kwa Tume Kuu kwa sababu ya vizuizi vya usafiri vinavyohusiana na UVIKO-19.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted