EU inakanusha kutumia vigezo viwili tofauti kushughulikia wakimbizi wa Syria na wale wa Ukraine

Zaidi ya watu milioni 1 wengi wao kutoka Syria walifika ufuo wa Ulaya mwaka 2015, lakini hawakupewa hadhi ya ulinzi wa moja kwa moja.

0
Wakimbizi wa Syria wakisubiri na watoto wao katika mpaka wa Uturuki na Ugiriki karibu na lango la Pazarkule la Edirne mnamo Machi 5, 2020 . (Photo by BULENT KILIC / AFP)

Umoja wa Ulaya ulisema Ijumaa kuwa hautumii vigezo viwili tofauti kwa wakimbizi kutoka Ukraine ikilinganishwa na wale wa Syria, huku ikikabiliana na mzozo mkubwa zaidi wa uhamiaji barani Ulaya tangu Vita vya Dunia vya pili.

Umoja huo umekosolewa vikali kwa madai ya kuwapokea wakimbizi kutoka Ukraine kwa uwazi zaidi, ikilinganishwa na wenzao wasio wazungu wanaokimbia mzozo Mashariki ya Kati.

Lakini makamu wa rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas alisema Ijumaa hakuna tofauti katika sera ya wakimbizi ya umoja huo kulingana na asili ya waimbizi.

Aliongeza hata hivyo kuwa hali ya sasa ya wakimbizi kutoka Ukraine ni “ya kipekee” kwani nchi hiyo inapakana moja kwa moja na mataifa kadhaa ya EU, tofauti na Syria.

“Tuna idadi nyingi ya mataifa wanachama (EU) ambayo yanapakana na Ukraine, kwa hivyo wakimbizi wanakuja moja kwa moja katika Umoja wa Ulaya,” aliwaambia waandishi wa habari mjini Istanbul.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni tatu wameikimbia Ukraine tangu uvamizi wa Urusi Februari 24, huku zaidi ya watu milioni mbili wakivuka na kuingia Poland mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

EU imewapa wakimbizi wa Kiukreni hadhi ya ulinzi wa muda, ambayo inawapa haki ya kukaa, kupata huduma za afya, kuenda shule na kufanya kazi.

“Tutahakikisha kuwa nafasi ambayo tumewapa watu hawa unatumika kama kanuni kwa watu wote katika EU,”Schinas alisema.

Kwa kulinganisha, zaidi ya watu milioni 1 wengi wao kutoka Syria walifika ufuo wa Ulaya mwaka 2015, lakini hawakupewa hadhi ya ulinzi wa moja kwa moja.

Umoja wa Ulaya unasema nchi wanachama ziliishia kutoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi 550,000 wa Syria mwaka wa 2015 na 2016. Wasyria wengi badala yake wamehamia Uturuki kulingana na makubaliano ya 2016 ya Umoja wa Ulaya yanayotoa motisha kwa Ankara, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kifedha, kwa ajili ya kuwapokea. Schinas alisema EU ilitekeleza wajibu wake kwa wakimbizi wa Syria.

“Tulifanya tuwezavyo upande wetu na nisingeona kuna tofauti katika hoja hii,” alisema.

Wasyria waliokimbia vita wanaweza kuomba hifadhi Ulaya, lakini hawapewi hadhi ya moja kwa moja kama ilivyo kwa wakimbizi wa Ukraine.

Schinas alisema hii inatokana na jiografia, kwani Ukraine inapakana na nchi tano wanachama wa EU.

“EU daima itasalia kuwa kimbilio la hifadhi kwa wale wanaokimbia vita au mateso,”aliongeza.

“Hiyo ndiyo inatueleza sisi kama Wazungu.”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted