Zelensky: Mazungumzo ya amani na Urusi magumu

Amebainisha kuwa wapatanishi wanafanya kazi bila kuchoka na kwamba watapumzika watakaposhinda. Kiongozi huyo wa Ukraine ameishukuru jumuiya ya kimataifa kwa kuiunga mkono nchi yake. 

0
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyaelezea mazungumzo ya amani na Urusi kama yaliyo magumu sana. Katika ujumbe wake wa video uliotolewa leo, Zelensky amesema wakati mwingine yanakuwa kama kashfa, lakini wanasonga mbele hatua kwa hatua.

Ameongeza kusema kuwa wawakilishi wa Ukraine katika mazungumzo hayo wamekuwa wakijadiliana kila siku. Zelensky amesema watafanya kazi, watapambana kadri wawezavyo hadi mwisho. 

Amebainisha kuwa wapatanishi wanafanya kazi bila kuchoka na kwamba watapumzika watakaposhinda. Kiongozi huyo wa Ukraine ameishukuru jumuiya ya kimataifa kwa kuiunga mkono nchi yake. 

Amesema ana matumaini kwamba mikutano mitatu iliyopangwa kufanyika juma hili ya kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya itachangia katika uungwaji mkono zaidi.

Katika hatua nyingine Zelensky kesho anatarajiwa kuuhutubia mkutano maalum wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. 

Kwa mujibu wa Sergey Nikiforov, ambaye ni msemaji wa Zelensky mkutano huo wa Brussels utaangazia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na msaada wa NATO kwa Ukraine. 

Zelensky atauhutubia kwa njia ya video mkutano huo ambao utahudhuriwa na Rais wa Marekani, Joe Biden. 

Zelensky amedokeza kuwa yuko tayari kufikiria kuachana na matakwa ya kuwa mwanachama kamili wa NATO, ili Ukraine nayo ipewe uhakikisho wa usalama. 

Zelensky pia amekuwa akishinikiza mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa Urusi, Vladmir Putin kufahamu iwapo Urusi inakusudia kusimamisha vita. 

Hadi sasa Putin amepuuzia ombi la mara kwa mara la Zelensky kuhusu mazungumzo hayo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted