Mji mkuu wa Somaliland wapata hasara kubwa baada ya moto kuzuka

Meya wa Hargeisa, mji mkuu wa Somaliland, alikadiria moto ulioteketeza soko la Waheen ulisababisha hasara ya hadi $2B

0

Wakaazi kutoka mji wa kaskazini mwa Somalia wa Hargeisa walipigwa na butwaa baada ya moto mkubwa kuharibu soko kuu siku ya Jumapili.
Meya wa Hargeisa, mji mkuu wa eneo lililojitenga la Somaliland, alikadiria moto ulioteketeza soko la Waheen ulikuwa umesababisha hasara ya hadi dola bilioni 2.
Maafisa wametoa wito wa haraka wa kusaidiwa kujenga upya soko la wazi, ambalo lilikuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi cha Hargeisa na takriban maduka na vibanda 2,000.
Moto huo ulizuka Ijumaa jioni na ulisambaa kwa kasi sokoni, na kuteketeza kila kitu kabla ya kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa siku ya Jumamosi.
Hakuna aliyepoteza maisha katika maafa yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhani, lakini watu 28 walijeruhiwa na mamia ya biashara kuharibiwa, maafisa walisema. Sababu bado haijajulikana.
“Kulingana na taarifa za awali kuhusu uharibifu uliosababishwa na moto, kuna makadirio ya hasara ya mali kati ya dola bilioni 1.5 hadi bilioni 2,”meya wa Hargeisa Abdikarim Mohamed Moge aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi jioni.
“Mji haujawahi kushuhudia janga kubwa kama hilo.”
Alisema shughuli ya kusafisha itaanza kwa kasi Jumanne baada ya kuwaruhusu wakaazi na wafanyabiashara wa eneo hilo kujaribu kuopoa mali yoyote iliyonusurika kutokana na moto huo.
Kamati ya watu watano imeundwa na rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi kuongoza shughuli ya uokoaji na juhudi za kuwasaidia wale ambao maisha yao yameharibiwa.
Waziri wa habari Saleban Yusuf Ali Kore aliwaambia waandishi wa habari kuwa moto huo uliharibu eneo la takriban mita za mraba 99,000 (kama ekari 24).

Matatizo ya msongamano
Picha kutoka eneo la tukio zilionyesha miali mikubwa ya moto na mawingu ya moshi yakitanda angani juu ya Hargeisa huku moto ukiendelea kushika kasi, na majengo mengi yakiteketea.
Mkuu wa kikosi cha zima moto na uokoaji cha Somaliland Ahmed Mohamed Hassan alisema takriban magari 24 yalitumika katika operesheni ya kuzima moto lakini yalitatizwa na barabara duni kuelekea soko hilo.
“Tumekuwa tukilalamikia msongamano wa watu hapa kwa muda na kupeleka kero zetu kwa wamiliki wa biashara, lakini wamepuuza wito wetu wa kupanua barabara.
“Natumai watajifunza kutokana na hili.”
Nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Uingereza, ambayo iliwahi kutawala Somaliland na nchi jirani za Ethiopia na Djibouti zimetoa msaada kutokana na maafa hayo.
“Mji wako utainuka tena na Uingereza itafanya tuwezalo kuunga mkono juhudi za ujenzi wa Somaliland,”Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alitweet Jumamosi, bila kutoa maelezo zaidi.
Somaliland ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991, kitendo ambacho hakijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa ambacho kimeacha eneo hilo lenye watu milioni 4.5 wakiwa maskini na kutengwa.
Somaliland hata hivyo imesalia kuwa mwanga linganishi wa utulivu wakati Somalia imekumbwa na miongo kadhaa ya ghasia za kisiasa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted