FAO: Bei za vyakula duniani zimeshuka kutoka rekodi ya juu kutokana na vita vya Ukraine

Bei ya vyakula duniani ilishuka kidogo mwezi uliopita baada ya kufikia rekodi yake ya juu mwezi Machi lakini imesalia kuwa juu kutokana na vita vya Ukraine

0

Bei ya vyakula duniani ilishuka kidogo mwezi uliopita baada ya kufikia rekodi yake ya juu mwezi Machi lakini imesalia kuwa juu kutokana na vita vya Ukraine, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa lilisema Ijumaa.

Vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi pamoja na matatizo ya usafirishaji wa bidhaa nje uliotokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24 umezusha hofu ya mzozo wa njaa duniani.

Urusi na Ukraine, zinaongoza katika upanzi wa vyakula tofauti maeneo hayo yakichangia sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya dunia katika bidhaa kuu kadhaa, ikiwa ni pamoja na ngano, mafuta ya mboga na mahindi.

Fahirisi ya bei ya chakula ya FAO, ambayo ilikuwa imeripoti rekodi za Machi na Februari, ilipungua kwa asilimia 0.8 mwezi Aprili ikilinganishwa na mwezi uliopita, shirika hilo lilisema katika taarifa.

“Kupungua kidogo kwa fahirisi ni afueni , hasa kwa nchi zinazokabiliwa na upungufu wa chakula, lakini bado bei za vyakula zinaendelea kuwa katika viwango vya juu jambo linaloakisi mkwamo wa soko na kuleta changamoto kwa usalama wa chakula duniani kwa walio hatarini zaidi,”Mchumi mkuu wa FAO Maximo Torero Cullen alisema.

Kushuka kwa wastani kulianza na kushuka kwa bei ya mafuta ya kupikia, huku bei ya mafuta ya kupikia ya FAO ikishuka kwa asilimia 5.7 mwezi Aprili.

Hata hivyo, FAO ilisema kuwa bei zinasalia kuwa juu sana huku kukiwa na “wasiwasi kuhusu upatikanaji wa mauzo ya nje kutoka Indonesia, nchi inayoongoza duniani kwa uuzaji nje wa mafuta ya mawese.”

Uamuzi wa Indonesia wa kusimamisha uuzaji wa mafuta ya mawese nje ya nchi kutokana na uhaba wa ndani umesukuma bei ya mafuta ya kupikia kupanda, na hivyo kuimarisha soko ambalo tayari liko kwenye makali kutokana na vita vya Ukraine na ongezeko la viwango vya joto duniani.

Fahirisi ni kipimo cha mabadiliko ya kila mwezi ya bei ya kimataifa ya kapu la bidhaa za chakula.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted