Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania watoa neno mauaji ya mwandishi wa Al-Jazeera

Mwanamke huyo alikuwa amevalia fulana yake iliyoandikwa "PRESS", hata hivyo alipigwa risasi licha ya kuvaa kizibao chenye alama hiyo ambayo ilidhaniwa itamlinda kama mwandishi wa habari katika maeneo...

0

Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania umelaani vikali mauaji ya kikatili ya Israel yaliyomlenga mwandishi wa habari mkongwe wa Al-Jazeera, Shireen AbuAqla katika kambi ya wakimbizi ya Jenin.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ubalozi huo jana Mei 11, 2022, wanajeshi wa Israel walimpiga risasi Shireen kichwani. Mwandishi huyo aliuawa wakati akiripoti uhalifu wa Israeli huko Jenin.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia fulana yake iliyoandikwa “PRESS”, hata hivyo alipigwa risasi licha ya kuvaa kizibao chenye alama hiyo ambayo ilidhaniwa itamlinda kama mwandishi wa habari katika maeneo yenye migogoro.

Taarifa hiyo ya Ubalozi wa Palestina, inaeleza kwamba mwanahabari mwingine wa Al Jazeera, Ali Samoudi, pia alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi mgongoni.

Pia, inabainisha kwamba picha za mauaji hayo zinaonyesha kuwa hakukuwa na upinzani wa Wapalestina wala makabiliano na jeshi la Israel katika eneo hilo wakati Shireen alipouawa kwa kupigwa risasi, ikimaanisha kuwa wanajeshi wa Israel waliwalenga waandishi wa habari kwa makusudi ili kuwazuia kuripoti ukatili katika kambi ya Jenin.

“Lengo ni kuwatisha waandishi wa habari dhidi ya kuangazia vitendo vya kikatili vilivyopangwa katika eneo hilo. Kwa miongo kadhaa, Shireen kwa ujasiri alifichua makosa ya jinai ya Israel dhidi ya watu wa Palestina.

“Kwa kuripoti kwake bila woga na kuendelea kwake kwa nguvu, Shireen alikua alama ya ukweli; shujaa wa taifa kwa wale ambao sauti zao zilinyamazishwa na uhalifu wa Israeli,” inaeleza taarifa hiyo.

Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania umemtaka Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kufungua uchunguzi mara moja na kwa haraka kuhusu uhalifu wa Israel dhidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari. Pia, wamelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukue jukumu lake na kuhakikisha ulinzi wa watu wa Palestina, kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Aidha ubalozi huo umetoa wito kwa waandishi wa habari nchini Tanzania kuungana katika kulaani mauaji ya wenzao wenzao na kutoa msimamo mmoja dhidi ya uhalifu huo unaofanywa na serikali ya Israel ambayo ni uhalifu dhidi ya binadamu, uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari.

Pia, wanatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama pamoja kuiwajibisha Israel na kuwajibika kwa uhalifu huu mkubwa. Taifa la Palestina linatoa wito kwa mashirika huru ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa kuichunguza Israel kwa uhalifu huu na kukataa wazo la uchunguzi wa Israel kuhusu suala hilo.

Taarifa ya Ubalozi inaeleza kwamba zaidi ya waandishi wa habari 55 wameuawa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kila moja ya nyakati hizi, Israel imeweza kukwepa jukumu la jinai hizo na kukwepa haki.

“Tunapoomboleza msiba huu mbaya wa kitaifa, tunawapa salamu wanahabari wetu na wafanyakazi wa vyombo vya habari pamoja na uandishi wa habari huru wa kimataifa kwa ushujaa wao na kuendelea kuueleza ulimwengu ukweli kuhusu kile kinachotokea Palestina licha ya kulengwa na walowezi katili wa Israel na utawala wa kibaguzi.

“Pia, tunatambua na kuheshimu sana uungwaji mkono kutoka kwa maofisa tofauti wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ambao walionyesha kukataa uhalifu huu mkubwa uliofanywa na Israeli. Leo sauti ya Wapalestina imeuawa, lakini mwangwi wake ni wa milele,” inafafanua taarifa hiyo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted