Bei mpya ya mafuta kuanza kutumika leo huku ikiendelea kupanda

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne Julai 5, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja jijini Dar es Salaam itakuwa shilingi 3,220 kwa...

0

Bei ya mafuta imepanda tena mwezi huu na kuivuka ile ya Mei, iliyokuwa kubwa zaidi katika historia ya Tanzania kiasi cha kuilazimu Serikali kutoa ruzuku.

Mei, bei ya petroli ilifika shilingi 3,148 jijini Dar es Salaam ikipanda kwa shilingi 287 kutoka Aprili kwa kila lita moja huku dizeli ikipanda kwa shilingi 566 kutoka shilingi 2,692 hadi shilingi 3,258 katika kipindi hicho.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne Julai 5, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), bei ya rejareja jijini Dar es Salaam itakuwa shilingi 3,220 kwa lita moja ya petroli na shilingi 3,143 kwa dizeli huku mafuta ya taa yakifika shilingi 3,442.

Maumivu yatakuwa makali mkoani Kagera hasa katika Wilaya ya Kyerwa ambako lita moja ya petroli itauzwa shilingi 3,458 na dizeli shilingi 3,381 na mafuta ya taa ni shilingi 3,679.

Ewura imesema bei hizo mpya ambazo zitaanza kutumika leo Jumatano zimejumuisha ruzuku ya shilingi 100 bilioni iliyotolewa na Serikali vinginevyo, lita ya petroli ingeuzwa shilingi 3,497 na dizeli shilingi 3,510 jijini Dar es Salaam wakati Kyerwa ingekuwa shilingi 3,735 kwa petrol na shilingi 3,748 kwa dizeli. Mafuta ya taa hayana ruzuku.

“Katika kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta hapa nchini Serikali imetoa ruzuku nyingi ya shilingi 100bilioni kwa mwezi Julai. Ruzuku hiyo imeelekezwa katika mafuta ya petroli na dizeli na kiasi kikubwa kimeelekezwa katika dizeli kwa lengo la kudhibiti mfumko wa bei,” imeeleza taarifa ya Ewura.

Mwezi uliopita, lita ya petrol iliuzwa shilingi 2,994 na dizeli shilingi 3,131 mkoani Dar es Salaam huku Kyerwa ikiwa shilingi 3,539 kwa petroli na shilingi 3,232 kwa lita ya dizeli.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted