Kenya: Karua amkosoa rais mteule William Ruto

Mgombea mwenza wa  Azimio la Umoja Martha Karua amemkashifu rais mteule William Ruto kwa kile ametaja kama kwenda kinyume na sheria ya Kenya katika kuvutia upande wake vyama...

0
Rais mteule William Ruto na Mgombea mwenza wa Azimio la Umoja Martha Wangare Karua.

Mgombea mwenza wa  Azimio la Umoja Martha Karua amemkashifu rais mteule William Ruto kwa kile ametaja kama kwenda kinyume na sheria ya Kenya katika kuvutia upande wake vyama washirika wa Azimio la Umoja.

Karua amesema kuwa ni jambo la kuatua moyo kuona kiongozi ambaye anaazimia kuiongoza taifa la Kenya akivunja sheria kwa kuvutia vyama vya kisiasa upande wa muungano wake bila wao kufuata mchakato uliopo katika sheria za vyama vya kisiasa.

“Uhalisia wake umeanza kujithihirishwa; ukosefu wa heshima kwa sheria na upungufu wa demokrasia. Ni mapema sana kwa yeyote kuanza kujaribu kupangua vyama vya kisasa bila kufuata sheria,”  amesema Martha Karua

Wakati huohuo Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni amepinga madai kuwa chama hicho tawala kinapania kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Kioni amesisitiza kuwa cha cha Jubilee bado kinaongozwa na mwafaka wa kabla ya uchaguzi na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya ambayo inahifadhifa na msajili wa vyama vya kisiasa.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa  amewaonya wabunge 28 waliochaguliwa kupitia chama hicho dhidi ya kufanya kazi na muungano wa rais mteule wa Kenya Kwanza.

“Sisi kama chama cha Jubilee iwapo tutakupata mbunge ama mwakilishi wadi akijihusisha na muungano wa Kenya Kwanza basi atapoteza kiti chake,” Aalisema Kioni.

Vilevile amewaonya viongozi walioibuka washindi kama wawaniaji huru dhidi ya kujihusisha na muungano wowote akisema wakifanya hivyo watapokonywa wadhifa wao.

Tamko la katibu huyo wa Jubilee linajiri siku chache tu baada ya wagombea 8 wa kibinafsi kati ya 12 kujiunga na Kenya Kwanza wakati wa mkutano wa kwanza wa viongozi waliochaguliwa kupitia muungano huo.

“Ikiwa ulichaguliwa kama mgombea huru unafaa kusalia huru katika kipindi cha miaka mitano. Ukifanya kosa la kujhusisha na chama kingine ikiwemo Jubilee basi utapoteza kiti chako,” alisisitiza Kioni.

“Wakati wa kupiga kura bungeni inakubalika upige upande unataka ila kujiusisha na chama chochote cha kisiasa haikubaliki kwa vyovyote vile,” aliongeza Kioni.

Haya yanajiri huku gavana mteule wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza akijiunga na Kenya Kwanza.

Ruto alitangaza kupitia ukurasa wake wa facebook na kupongeza hatua ya gavana huyo wa Meru ambaye alichaguliwa kama mgombea huru.

Hatua ya gavana huyo mteule ikija siku moja baada ya seneta mteule wa Mandera Ali Roba na chama chake United Democratic Movement (UDM) kugura Azimio la Umoja na kujiunga na Kenya Kwanza.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted