Baraza la usalama Kenya yapinga kutaka kubadili matokeo ya urais

Baraza la kitaifa la usalama Kenya limepinga kujaribu kuitilafiana na matokeo ya urais.

0
Baraza la usalama nchini Kenya.

Baraza la kitaifa la usalama nchini Kenya (NSAC) limekubali kuwa lilikutana na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Wafula Chebulat lakini likapinga kujaribu kuitilafiana na matokeo ya uchaguzi wa urais.

Katika hati kiapo iliyotiwa saini na waziri msaidizi katika afisi ya rais Kennedy Kihara na mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua baraza hilo imesema walikwenda katika ukumbi wa Bomas kujadili masuala ya kiusalama pekee.

Kulingana na Kihara, tarehe 15 agosti wakati akitekeleza majukumu alivyoelekezwa na baraza la NSAC, aliongoza ujumbe uliojumuisha Kennedy Ogeto, inspekta jenerali Hillary Mutyambai na Francis Ogolla kukutana na Wafula Chebukati na makamishna wengine wa IEBC katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo ya urais katika ukumbi wa Bomas.

 “Ilitulazimu kufanya mkutano huo na tume ya IEBC kwa kuwa kama baraza la kitaifa la usalama nchini Kenya kulikuwepo habari kuwa matokeo ya urais yangechelewa kutangazwa kulingana na jinsi matokeo yalikuwa yanasambazwa na pamoja na hatua ya kuzuia runinga kuonyesha matokeo kwa umma ilikuwa imeaanza kuzua hofu,” alisema Kihara katika hati kiapo.

NSAC imesema wakati wakisaka nafasi ya kukutana na Chebukati,haikuwa bayana iwapo Chebukati angeweza kuafikia makataa ya kutangaza matokeo ya urais ambayo ni siku saba tangu wakenya kushiriki zoezi la kupiga kura au iwapo walikumbwa na changamoto kwa kuwa matokeo hayakuwa yanaonyesha katika runinga bila kuwepo mawasiliano rasmi kwa umma.

 “Nafahamu kuwa sheria inasema matokeo yatangazwe baada ya siku saba ambayo ilikuwa ikamilike tarehe 16 agosti. Kucheleweshwa kwa matokeo ya urais hakukuwa kinyume cha sheria ila kulizua tumbo joto nchini Kenya,” Kihara alisema.

Kwa upande wake Joseph Kinyua amesema alimtaka Chebukati kumjulisha uamuzi wake kuhusu ombi la kutuma timu la baraza la usalama ikutane na tume ya uchaguzi ili wajadili kuhusu athari zilizokuwa zinazingira ujumuishaji, usambazaji na utangazaji wa matokeo ya urais.

Kinyua amesisitiza kuwa walijaribu wawezavyo kufanya mkutano na Chebukati awali lakini hawakufaulu kwani Chebukati hakuwapa nafasi hiyo.

“Ni kutokana na ugharura na uzito wa suala hilo ndiposa NSAC ikaamua kuwa na mkutano wa ana kwa ana kinyume na kuwa na masiliano kupitia mbinu zingine za mawasiliano,” amesisitiza Kinyua

Ameendelea kusema hakuna kitu kisichokuwa cha kawaida katika mkutano huo kwa kuwa NSAC na IEBC wameshirikiana awali katika masuala yanayohusiana na usalama wakati wa uchaguzi huku kukiwa na uhuru katika pande zote mbili.

“Kama mwenyekiti wa NSAC, sina ufahamu kuhusu uamuzi wa kukutana  na Chebukati kwa nia ya kubatilisha matokeo ya urais  katika uchaguzi mkuu,” Kinyua alisema.

Mkuu huyo wa utumishi wa umma ameendelea kusema NSAC haina majukumu katika mchakato nzima wa uchaguzi mbali na kutoa ushauri kuhusu usalama wakati na baada ya wa uchaguzi ili kuhakikisha taifa linasalia salama wakati huu wa uchaguzi.

Baraza hilo limejitokeza na kuweka mambo wazi baada ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kudai katika majibu yake kwa kesi ya Azimio la Umoja One Kenya kupinga matokeo ya urais.

Katika majibu yake Chebukati alidai kuwa baraza hilo lilimtaka kupunguza matokeo ya rais mteule William Ruto ili kumfanya Raila Odinga kuwa rais ama kulazimu marudio ya urais ila akakataa katakata.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted