Shahidi Wa Jamhuri Asema Hajui Kama Lissu Ni Wakili Kitaaluma

Shahidi wa nne katika kesi ya Kikatiba ambaye ni Mkuu wa Gereza la Ukonga Edward Shabani amesema hafahamu wala hajui kwamba Tundu Lissu ni Wakili kitaaluma na aliwahi pia kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika(TLS).

Shahidi Wa Jamhuri Asema Hajui Kama Lissu Ni Wakili Kitaaluma

Ameyasema hayo leo Julai 23,2026 kwenye ushahidi wake wakati akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa waleta maombi kutoka TLS ambao kimsingi wanamaslahi na shauri hilo, Wakili Emmanuel Ukashu muda mfupi kabla ya kusawazisha maswali ya dodoso kutoka jopo la mawakili wa Jamhuri.

Katika hoja hizo Wakili Ukashu pia alimuuliza shahidi iwapo anajua chochote kuhusu maelekezo kutoka ambapo shahidi alijibu kwa uelewa wake ni maelekezo ya kiutendaji.

Wakili: Nitakua sahihi kusema kwamba waleta maombi wote ni mawakili.

Shahidi: Sahihi

Wakili: Nitakua sahihi nikisema mleta maombi namba 4 ambaye ni mshtakiwa Lissu ni Wakili.

Shahidi: Sifahamu.

Wakili: Nitakua sahihi nikisema mleta maombi 4 aliwahi kuwa Rais wa TLS.

Shahidi: Sifahamu

Wakili: Kwa kiapo chako ulicholeta hapa Mahakamani ili mtu aweze kuingia Gerezani maana yake taarifa zake zimehakikiwa na wewe.

Shahidi: Sahihi

Wakili: Nitakua sahihi bosi wako ni Kamishina General wa Magereza

Shahidi: Sahihi

Wakili: Kwa uelewa wako ukiambiwa malekezo kutoka juu Unaelewa nini.

Shahidi: Ni maelekezo ya kiutendaji

Wakili: Usipoyafanya haufukuzwi kazi

Shahidi: Inategemea

Wakili: Unajua taaluma ya Sheria inaheshimiwa sana

Shahidi: Najua

Wakili: Unajua kwamba Wakili anatakiwa awe na chumba chake

maalum kwa ajili ya kuongea na mteja wake.

Shahidi: Najua.

Wakili Ukashu alihitimisha hoja hiyo akimpa kijiti Wakili Edson Kilatu ambaye katika msingi wa hoja zake kwa Shahidi alimuuliza shahidi juu ya utaratibu wa watu kuingia gerezani kwenye kuona ndugu au kama ni wakili kwenda kuonana na wateja wake.

Wakili: Ni sahihi kuna kitabu ambacho raia wa kawaida wakiingia ni lazima wawe wanasaini

Shahidi:Sahihi

Wakili: Na ni sahihi vile kuna kitabu cha Mawakili kusaini

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Na ni sahihi vilevile kuna watu wanaosimamia wanaoingia

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Ni sahihi kwamba vitabu vya pale kwenye geti la kuingia wanasaini

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Ni sahihi kwamba kwa utaratibu inatakiwa kujiandikisha na kwa  waliokataliwa kuingia kumuona ndugu au kama wakili kumuona mteja wake ni lazima iandikwe kwanini alikataliwa.

Shahidi: Sina Uhakika

Wakili: Ilizungumziwa suala la ukaguzi wa nyaraka hapa, sasa umeleta kiapo cha afisa yoyote ambaye alikagua hizo nyaraka

Shahidi: Sijaleta

Wakili: Ni sahihi kwamba bwana Lecha ambaye ni Msaidizi wako hajaleta kiapo chochote.

Shahidi: Anayetakiwa kuleta hicho kiapo ni Mkuu wa Gereza kwa ajili ya watendaji wote.

Wakili: Wakati unahojiwa na Lissu ulizungumzia kwamba ya kitu ambacho umekubali ni kwamba Lissu ameleta orodha ya watu ambao amewaleta

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Na ni sahihi kwamba wewe unakua unaruhusu watu ambao hawajawekwa kwenye Orodha kuonana na Lissu

Shahidi: Inategemea

Katika maswali ya kusawazisha yaliyoulizwa na Wakili wa Serikali Francis Wisdom, Shahidi aliieleza Mahakama kwamba, suala la mtu kuandikisha au kufanyiwa ukaguzi ni la lazima na kuhusu mshtakiwa kulindwa analindwa wakati wote mpaka kesi itakapoisha.

Shauri hili la kikatiba namba 7300/2026 leo limehitimishwa baada ya mashahidi kumaliza kutoa ushahidi kwa siku nne mfululizo, na sasa kinachosubiriwa ni uamuzi ambapo Mahakama  chini jopo la majaji watatu wakiongozwa  jaji Amiri Mruma, wamepanga tarehe 16 Septemba 2026, kuja kwa ajili ya kutaja tarehe ya uamuzi

Katika shauri hilo, mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo wanailalamikia Mamlaka ya Magereza kwa madai ya kuwazuia kuingia Gereza la Ukonga kumwona mteja wao na kutowapatia faragha ya kufanya mazungumzo naye waliporuhusiwa kuingia gerezani.