Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitishwa na maneno anayodaiwa kuyatamka, akisema kutokuwepo kwa ushahidi huo kunafanya jibu la hoja hiyo kuwa moja kwamba Serikali haikutishika.

Lissu ametoa hoja hiyo leo, Ijumaa Septemba 25, 2026, wakati akiendelea na majumuisho yake ya mwisho katika kesi ya uhaini inayomkabili, ambapo pia ametumia sehemu ya muda wake kuijadili historia ya sheria ya uhaini na msimamo wa Mahakama ya Rufani kuhusu maneno pekee katika kosa hilo.Akizungumzia hoja hiyo Lissu amesema suala la iwapo Serikali ilitishwa linapaswa kuangaliwa pamoja na nia inayodaiwa na upande wa mashtaka chini ya kifungu cha 39(2) cha Penal Code.Amesema ikiwa upande wa mashtaka unadai kwamba maneno yake yalikuwa na nia ya kuitisha Serikali, ulipaswa kuonyesha katika hati ya mashtaka na kuthibitisha kwa ushahidi matokeo ya nia hiyo, ikiwemo kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilitishwa.Kwa mujibu wa Lissu, hakuna sehemu katika hati ya mashtaka inayoeleza namna Serikali ilivyotishwa wala hakuna ushahidi wa kiongozi au mamlaka ya Serikali aliyefika Mahakamani kuthibitisha kuwa Serikali ilitishwa na kauli hizo.Amesema aliomba baadhi ya viongozi wa Serikali waitwe kama mashahidi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Philip Mpango na aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lakini Mahakama ilikataa maombi hayo.Lissu amesema hata baada ya Mahakama kumruhusu kuwaita Mkuu wa Majeshi, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, hakuna aliyetoa ushahidi unaothibitisha kwamba Serikali ilitishwa.Ametaja pia Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, ambaye alifika lakini hakutoa ushahidi wa kumtetea.Kwa msingi huo, Lissu amesema mzigo wa kuthibitisha shtaka ulikuwa kwa upande wa mashtaka na si kwa upande wa utetezi.“Kwenye rekodi, hakuna hata mmoja aliyekuja kuthibitisha kama Serikali ilitishika. Kama Serikali haikutishika, maana yake sina kosa.”Lissu ameendelea kusema kuwa upande wa utetezi haukuwa na wajibu wa kuthibitisha kwamba Serikali haikutishwa, bali jukumu hilo lilikuwa kwa upande wa mashtaka kuthibitisha vipengele vinavyounda kosa linalodaiwa.Amesema hakuna ushahidi uliowasilishwa Mahakamani unaoonyesha kwamba viongozi wa Serikali au Serikali yenyewe walihisi kutishiwa kutokana na kauli anazodaiwa kutoa.Akihitimisha hoja hiyo, Lissu amesema jibu la swali la iwapo Serikali ilitishwa linapaswa kuwa hasi.“Jibu la swali hili ni: Serikali haikutishwa.”Hoja hiyo imekuja baada ya Lissu pia kutumia majumuisho yake kueleza msimamo wake kwamba maneno pekee hayawezi kuunda kosa la uhaini, akirejea kesi ya Hatibu Gandhi na wenzake na historia ya sheria ya uhaini.Katika kuunda hoja hiyo ametumia kizimba cha Mahakama kuweka mjadala wa historia ya Sheria akirejea chimbuko lake kutoka mfumo wa sheria wa Uingereza na namna ilivyoingia katika sheria za Tanganyika.Amesema historia ya sheria ya uhaini Tanzania ni muhimu katika kutafsiri kifungu cha 39 cha “Penal Code, akidai kuwa masharti ya uhaini katika sheria ya Tanzania yalitokana na mfumo wa sheria wa Uingereza ambako, kwa mujibu wa hoja yake, masharti yaliyohusu uhaini unaotokana na maneno yaliondolewa.Kwa msingi huo, Lissu amesema upande wa mashtaka haupaswi kujaribu kuingiza katika sheria ya Tanzania, dhana ya “uhaini wa maneno” ambayo, kwa madai yake, haijawahi kuwa sehemu ya sheria hiyo.Akiirejea kesi ya Hatibu Gandhi na wenzake, Lissu amesema Mahakama ya Rufani ilieleza umuhimu wa kuwepo kwa kitendo cha wazi (overt act) katika kuthibitisha kosa la uhaini.Kwa mtazamo wake, uamuzi huo unaonyesha kuwa kauli au maneno pekee hayawezi kuwa msingi wa kumtia mtu hatiani kwa kosa la uhaini bila kuwepo kwa kitendo kinachokidhi matakwa ya sheria.“Je, maneno ya mdomo yanatengeneza kosa la uhaini?” amehoji Lissu, akisema hilo ni moja ya maswali ambayo Mahakama inapaswa kuyajibu katika kesi yake.Lissu amesema upande wa mashtaka unataka Mahakama ikubali kwamba kauli alizodaiwa kutoa Aprili 3, 2025 zinatosha kuunda kosa la uhaini, jambo ambalo ameliita jaribio la kuingiza tafsiri mpya katika sheria.“Rai yangu waheshimiwa majaji, mtakapofanya uamuzi kwa kufahamu historia hii, msikubali mwaliko wao wa kuingiza kwenye sheria yetu ya uhaini mambo ambayo hayajawahi kuwepo kabisa na mambo ambayo Mahakama ya Rufani ya Tanzania imeshayawekea msimamo wa wazi,” amesema.Lissu pia amehusisha hoja hiyo na suala la uchapishaji wa maneno anayodaiwa kuyatamka kupitia Jambo TV, akisema hata suala hilo linahitaji upande wa mashtaka kuthibitisha kwa ushahidi kwamba yeye ndiye aliyechapisha video hiyo.Amesema mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi kuhusu uchapishaji huo walitoa maelezo yenye tofauti kuhusu nani aliyeweka video hiyo kwenye mtandao wa Jambo TV.Kwa upande wa shahidi wa 3 wa Jamhuri, Lissu amesema shahidi huyo alikiri kwamba alikuta video hiyo kwenye YouTube ya Jambo TV lakini hakubaini katika uchunguzi wake nani aliyeiweka.Kuhusu shahidi wa 16 wa Jamhuri, amesema shahidi huyo alidai kuwa Lissu ndiye aliyechapisha video hiyo, lakini wakati wa kuhojiwa alikiri kutokuwa na uhakika kama Lissu alikuwa mwajiriwa wa Jambo TV au kama alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye akaunti ya YouTube ya kituo hicho.Lissu amesema tofauti hizo zinapaswa kuzingatiwa katika kuamua iwapo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha vipengele vinavyounda kosa analokabiliwa nalo.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu, Septemba 28, 2026, saa tatu asubuhi, wakati Lissu anatarajiwa kumaliza majumuisho yake ya mwisho ili kutoa nafasi kwa upande wa Jamhuri.Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini katika Kesi ya Jinai Na. 19605/2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akidaiwa kutenda kosa kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Penal Code kupitia kauli alizodaiwa kutoa Aprili 3, 2025.Alikamatwa kwa mara ya kwanza tarehe 9 Aprili 2025, mkoani Ruvuma katika mji wa Mbinga na kusafirishwa siku hiyo hiyo kuletwa Dar es Salaam na Aprili 10,2025 alipandishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu.







