Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Antipas Lissu, Novemba 6, 2026, baada ya upande wa Jamhuri na utetezi kukamilisha mawasilisho yao ya mwisho.
Tarehe hiyo imetajwa mwishoni mwa mawasilisho ya upande wa Jamhuri, huku Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, akiieleza Mahakama kuwa Jamhuri inaamini imeweza kuthibitisha pasi na shaka viini vya kosa linalomkabili Lissu.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, akituhumiwa kuwa Aprili 3, 2025, ndani ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, akiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitengeneza nia ya kuchochea umma kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025 kwa nia ya kuitishia Serikali na kudhihirisha nia hiyo kwa kutoa na kusambaza maneno yaliyotajwa katika hati ya mashtaka.
Miongoni mwa maneno hayo ni kauli zinazodaiwa kutolewa na Lissu kwamba, “tunazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi” na “tutauvuruga huu uchaguzi”, ambazo Jamhuri imezitumia kama sehemu ya msingi wa hoja yake kwamba kauli hizo zililenga kuitishia Serikali ili kupata mabadiliko.
Katika mawasilisho yake, Katuga ameanza kwa kuielekeza Mahakama kwenye kifungu cha 39(2)(d), akisema kifungu hicho kinahusu mtu aliye chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe ndani au nje ya Tanzania, anayekuwa na nia ya kuchochea umma kwa madhumuni yanayotajwa katika kifungu hicho.
Ameunganisha kifungu hicho na kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Sura ya 20, akisema sheria inataka hati ya mashtaka ieleze kosa ambalo mshtakiwa anashtakiwa nalo pamoja na maelezo ya namna kosa hilo lilivyofanyika ili mshtakiwa aweze kufahamu shtaka na kujitetea.
Katuga pia amerejea kifungu cha 138(a)(iii), akisema hati ya mashtaka inapaswa kutumia lugha ya kawaida ili maelezo yake yaeleweke.Kwa mujibu wa Katuga, katika kuandaa hati ya mashtaka Jamhuri ilizingatia kuwa Lissu ni raia wa Tanzania mwenye utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ikaweka wazi nia inayodaiwa kuwa ya kuchochea umma kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesema hati ya mashtaka imetumia neno “public” kueleza umma uliochochewa, huku akisema ushahidi wa Jamhuri unaonyesha kuwa Lissu hakulenga mtu mmoja au kundi maalumu la watu.
Kwa sababu hiyo, Katuga amesema Jamhuri imeomba neno “public” litafsiriwe kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo, akisema umma unaweza kumaanisha kundi la watu bila kuwepo idadi maalumu inayotakiwa kisheria ili kuitwa kundi la watu.
Katuga amesema pia baadhi ya maneno yaliyotumika katika kifungu cha sheria na yale yaliyotumika kwenye hati ya mashtaka hayapaswi kuchukuliwa kuwa na maana sawa kwa sababu kifungu kinatumia neno “or”, ambalo kwa tafsiri yake linaonyesha kuwa vitu vinavyotenganishwa si lazima viwe na maana inayofanana.
Amesema hoja hiyo si maoni yake binafsi bali inatokana na sheria iliyojadiliwa na kutungwa na Bunge, akirejea pia kifungu cha 13 cha sheria husika.
Kuhusu namna nia ya kutenda uhaini inavyoweza kudhihirishwa, Katuga amesema kifungu cha 39(2)(d) kinataja uwezekano wa nia hiyo kudhihirishwa kupitia usambazaji wa maandishi au michoro.
Amezungumzia tofauti kati ya dhana ya “manifestation”, “overt act” na “deep”, akirejea kesi ya Khatibu Ghandi na wenzake dhidi ya Jamhuri, ambapo suala la “overt act by individual” lilijadiliwa.
Kwa mujibu wa Katuga, katika mazingira ya kesi hiyo, kutoa maneno yenyewe kunaweza kuwa kitendo kinachoweza kuzingatiwa kisheria, na ameiomba Mahakama izingatie kifungu cha 89(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu kinachohusu kutoa maneno kama tendo.
Kuhusu suala la uchapishaji, Katuga amesema Lissu hakutamka tu maneno hayo bali pia Jamhuri inadai kuwa yalichapishwa au kusambazwa.
Amesema kifungu cha 39(2)(d) kinataja aina mbili za “publishing”, ikiwemo kuandika au kuchapisha, na kwamba hati ya mashtaka imenukuu maneno hayo kwa kuweka alama za kunukuu pamoja na nukta tatu zinazoonyesha kuwa sehemu ya maneno imeachwa.
Kwa hiyo, amesema Mahakama inapaswa kuyatazama maneno yaliyomo katika hati ya mashtaka kwa uelewa unaokubalika katika mazingira ya shtaka.
Kuhusu adhabu, Katuga amesema kifungu hicho kinaweka uwezekano wa adhabu ya kifo iwapo mshtakiwa atapatikana na hatia.
Amesema hoja hiyo imeletwa kwa sababu wakati wa mawasilisho ya utetezi kulikuwa na hoja kwamba adhabu ya shtaka hilo ni kunyongwa pekee.
Katuga ameeleza kuwa matumizi ya maneno “shall be liable” yana maana kwamba adhabu inaweza kuanzia kiwango cha chini hadi kifo, na kwamba Mahakama ina mamlaka ya kuamua adhabu iwapo mshtakiwa atapatikana na hatia, kwa kuzingatia aina ya kitendo kilichofanyika.Katika kuunga mkono hoja hiyo, amerejea kesi ya Bahati John dhidi ya Jamhuri, Criminal Case No. 114 ya mwaka 2019, iliyotolewa hukumu Julai 2022.
Akizungumzia mzigo wa kuthibitisha shtaka, Katuga amesema jukumu hilo liko kwa Jamhuri chini ya kifungu cha 3(2)(a) cha Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6, na kwamba kwa tafsiri ya kifungu cha 39(2)(d) pamoja na namna hati ya mashtaka ilivyoandaliwa, Jamhuri inaona ushahidi uliowasilishwa umeweza kuthibitisha shtaka.
Amesema upande wa utetezi haujaweza kutikisa ushahidi wa Jamhuri, akieleza kuwa majibu mengi yaliyotolewa yalikuwa kama “sijui” na “sikumbuki”.
Katuga ameiomba Mahakama katika kuamua kesi hiyo iangalie viini vya kosa na kujiuliza maswali matatu makuu.
Swali la kwanza ni kama Lissu ana wajibu wa utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Swali la pili ni kama Lissu alitengeneza nia ya kuitishia Serikali.
Na swali la tatu ni kama alidhihirisha nia hiyo ya kuitishia Serikali kupitia kitendo cha kusambaza na kuchapisha maneno hayo.
Kwa mujibu wa Katuga, viini hivyo vinafanana na viini vilivyojadiliwa katika kesi ya Khatibu Ghandi na wenzake dhidi ya Jamhuri, ingawa kesi hiyo ilihusu kifungu cha 39(2)(a), wakati shtaka linalomkabili Lissu liko chini ya kifungu cha 39(2)(d).
Katika kiini cha kwanza, Katuga amesema suala la Lissu kuwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halikupingwa wakati wa hoja za awali.
Amesema katika ukurasa wa 133 wa rekodi ya Mahakama, Lissu mwenyewe alieleza kuwa ni Mtanzania mwenye utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katuga amesema baada ya hoja za awali kukubaliwa, Jamhuri ina jukumu la kuthibitisha kile kilichoelezwa katika hati ya mashtaka, akisisitiza kuwa hoja zilizojadiliwa katika hatua za awali hazibadilishi mzigo wa kisheria wa kuthibitisha shtaka.
Amesema “summary of evidence” inayowasilishwa katika hatua za awali haijatengenezwa kuwa shtaka lenyewe bali hutumika kuthibitisha mambo yanayobishaniwa.
Kuhusu kiini cha pili, Katuga amesema Jamhuri inapaswa kuthibitisha kama Lissu alitengeneza nia ya kuchochea umma kwa madhumuni ya kuitishia Serikali.
Amesema neno “Serikali” katika kifungu cha 39(2)(d) halina tafsiri mahsusi inayolitenganisha na Executive au Judiciary, hivyo Mahakama inapaswa kulitafsiri kwa namna sheria ilivyoandikwa.
Katuga amerejea ushahidi wa shahidi wa kwanza wa Jamhuri, ambaye aliiambia Mahakama kuwa Lissu alilenga kuitishia Serikali kwa sababu Serikali ina wajibu wa kulinda sheria na kwamba kuvuruga uchaguzi unaofanyika kwa mujibu wa sheria ni kuitishia Serikali.
Pia amerejea ushahidi wa shahidi wa 16 wa Jamhuri, ambaye alisema maneno ya “tutazuia uchaguzi” na “tutahamasisha uasi” yalilenga kuitishia Serikali yenye wajibu wa kulinda amani na utulivu.
Kwa mujibu wa Katuga, shahidi huyo alisema kauli hizo hazikulenga tu kuvuruga amani bali pia kuvuruga uchaguzi uliowekwa kwa mujibu wa sheria na Katiba, huku akieleza kuwa kauli kuhusu “kukinikisha” zililenga pia kuwaumiza watu, kuwarushia mawe na kuzuia watu kupiga kura.
Katuga amesema ushahidi wa mashahidi hao wawili uliungwa mkono na ushahidi wa upande wa utetezi, ukiwemo ushahidi wa Lissu mwenyewe.
Kwa msingi huo, amesema Jamhuri inaona kuwa imethibitisha kwamba Lissu alitengeneza nia ya kuitishia Serikali, na kwamba nia hiyo imeonyeshwa kupitia maneno aliyoyatamka na ambayo Jamhuri imeyaweka katika hati ya mashtaka.
Amesema maneno hayo yalihusisha kuhamasisha uasi, “kukinikisha” na kuzuia uchaguzi kama njia ya kupata mabadiliko.
Kuhusu ushahidi wa kutamka maneno hayo, Katuga amesema ingawa maneno hayo hayakukubalika katika hatua ya awali kwa namna hiyo, wakati wa usikilizwaji wa kesi upande wa Jamhuri kupitia mashahidi wake 16 ulileta ushahidi kwamba Lissu aliyatamka katika mkutano wa Aprili 3, 2025 uliokuwa ukihusishwa na Jambo TV.
Amesema shahidi wa 17 naye alieleza kuwa aliyasikia maneno hayo kwa sababu alikuwa kwenye mkutano huo.
Katuga amesema wakati wa maswali ya dodoso Lissu hakupinga kutamka maneno hayo, bali alipinga kwamba maneno hayo yanaunda kosa la uhaini na pia alipinga suala la yeye kuyasambaza.
Kwa hiyo, kwa mtazamo wa Jamhuri, ushahidi wa upande wa mashtaka uliungwa mkono na ushahidi wa utetezi na hakuna shaka kwamba Lissu alitamka maneno hayo Aprili 3, 2025.
Amesema ushahidi wa Jamhuri umeeleza namna maneno hayo yalivyopokelewa na namna Jamhuri ilivyofikia hitimisho kuhusu nia ya Lissu.
Katuga amesema maneno yaliyonukuliwa katika hati ya mashtaka ni sentensi zilizokamilika na zenye maana, na kwamba ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri umeunga mkono maneno hayo.
Amesema hata ushahidi wa DW3 na DW4 uliunga mkono kuwa maneno yaliyonukuliwa katika hati ya mashtaka yalikuwa maneno yaliyokamilika na yenye maana.
Katuga pia amesema ushahidi wa Lissu mwenyewe unaweza kuibeba hoja ya Jamhuri, akisema Lissu alitamka maneno hayo huku akiamini kwamba angefunguliwa kesi ya uhaini.Amesema ushahidi wa mshtakiwa ni muhimu katika kuangalia mazingira ya kesi hiyo.
Kuhusu suala la kama kauli hizo zilichochea umma, Katuga amesema Jamhuri imeleta mashahidi waliodai kuathiriwa na maneno ya Lissu, ambao wanatoka sehemu tofauti za jamii ya Watanzania.
Amesema baadhi yao ni wafuasi na wengine ni watu waliokuwa wapenzi wa Chadema, na kwamba mashahidi hao waliieleza Mahakama namna walivyochocheka kutokana na maneno ya mwenyekiti wao.
Akiirejea rekodi ya Mahakama, Katuga amesema mmoja wa mashahidi alieleza namna alivyosema watu wangeungana kupiga, kufanya vurugu na kuwarushia mawe wale waliokuwa wakienda kupiga kura.
Amesema ushahidi wa mashahidi hao uliungwa mkono pia na mashahidi wa upande wa utetezi kuanzia DW1 hadi DW4.
Kwa ujumla, Katuga amesema Jamhuri inaona kuwa kupitia maneno yaliyomo katika hati ya mashtaka pamoja na ushahidi ulioungwa mkono na upande wa utetezi, imeweza kuthibitisha hoja yake kwamba Lissu alitengeneza nia ya kuitishia Serikali kwa kuwa Serikali ndiyo yenye mamlaka kisheria.
Amesema pia suala la uchapishaji au usambazaji wa maneno hayo limethibitishwa kupitia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ulioungwa mkono na ushahidi wa upande wa utetezi.
Katika hitimisho lake, Katuga amesema ushahidi wa mashahidi 17 wa Jamhuri ukiungwa mkono na mashahidi watano wa utetezi ndio msingi wa hoja ya Jamhuri kwamba imethibitisha shtaka pasi na shaka.
“Tunaiambia Mahakama hii kwa ushahidi wa mashahidi 17 ukiwa unaungwa mkono na mashahidi watano wa utetezi ni hoja yetu kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha pasi na shaka,” amesema Katuga, akiomba Mahakama irekodi kuwa mshtakiwa ametenda kosa.
Baada ya kukamilika kwa mawasilisho hayo, Mahakama imetaja Novemba 6, 2026 kuwa siku inayotarajiwa kutolewa hukumu ya kesi hiyo.








