Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, ametimiza wito wa Jeshi la Polisi na kuhojiwa kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo madai kwamba chama hicho kimeacha kutekeleza majukumu yake ya kitaaluma na badala yake kujikita katika harakati za uanaharakati, pamoja na madai ya kufadhili maandamano yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano hayo, Wakili Jebra ambaye alikuwa miongoni mwa mawakili waliohudhuria kusimamia mahojiano ya Mwabukusi, akiwa pamoja na Wakili Ziada Mkwazu, amesema Mwabukusi aliitwa na kuhojiwa katika nafasi yake kama Rais wa TLS, bila kutajwa tuhuma maalumu za kosa la jinai analotuhumiwa nalo, kwa kuwa hakuhojiwa kama mtuhumiwa bali kwa mujibu wa Kifungu cha 36(2)(c) cha Sheria ya Ushahidi Tanzania.
Amesema pamoja na kutokuwa na tuhuma maalumu za kosa la jinai dhidi yake katika mahojiano hayo, Mwabukusi aliulizwa maswali kuhusu shughuli za TLS, video mbalimbali alizoonyeshwa na madai yanayohusisha chama hicho na maandalizi ya maandamano ya Oktoba 29, 2026.
Jebra amesema moja ya masuala yaliyoibuliwa na polisi ni madai kwamba Mwabukusi, akiwa Rais wa TLS, amekifanya chama hicho kuacha shughuli zake za kitaaluma na badala yake kujikita katika shughuli za uanaharakati.
Akieleza majibu ya Mwabukusi kuhusu suala hilo, Jebra amesema alieleza kuwa TLS inafanya harakati za kitaaluma na si harakati za vurugu wala uchochezi.Kwa hiyo, shughuli alizokuwa akifanya Mwabukusi zilikuwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake kama Rais wa chama hicho.
Katika mahojiano hayo, Jebra amesema Mwabukusi alionyeshwa video mbalimbali zilizokuwa zikimuonyesha katika shughuli tofauti, zikiwemo kongamano, mikutano na shughuli nyingine zilizohusiana na masuala ya DP World.
Kwa mujibu wa Jebra, Mwabukusi alikana madai kwamba video hizo zilikuwa na maudhui ya uchochezi, akieleza kuwa zilihusu taarifa za kawaida zilizowasilishwa na wananchi mbalimbali kwa TLS.Amesema Mwabukusi alifafanua kuwa akiwa Rais wa TLS ana wajibu wa kuwasemea mawakili na kutetea jamii kwa ujumla, hivyo alisisitiza kuwa alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kiuongozi na kitaaluma.
Amesema baadhi ya tuhuma zilizoibuliwa wakati wa mahojiano hayo ziliwashangaza mawakili, hususan madai kwamba Baraza la Uongozi la TLS limepokea fedha kwa ajili ya kufadhili maandamano yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2026 ambayo bado kimsingi hayajafanyika.
Jebra amesema Mwabukusi alikanusha madai hayo, akieleza kuwa Baraza la Uongozi la TLS halijawahi kukutana wala kujadili suala la maandamano hayo, na kwamba si shughuli za baraza hilo kujadili maandamano ya aina hiyo.
Amesema Mwabukusi alieleza wazi kuwa akaunti za TLS ziko wazi na zinajulikana, hivyo hakuna fedha inayoingia katika chama hicho bila kujulikana inakotoka, wala fedha inayotumika bila kujulikana inakokwenda.
Tuhuma nyingine zilizoulizwa katika mahojiano hayo ni madai kwamba Mwabukusi, akiwa Rais wa TLS, amefadhili vijana wengi kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kupata mafunzo na maarifa yanayoweza kutumiwa katika maandalizi ya maandamano ya Oktoba 29, 2026.
Jebra amesema tuhuma hizo zilimshangaza Mwabukusi, ambaye alizikanusha na kueleza kuwa si za kweli.
Katika maelezo yake, Jebra amesema mawakili walisisitiza mbele ya Jeshi la Polisi kwamba hakuna sehemu yoyote katika matamko ya TLS inayoonyesha chama hicho kimejihusisha na harakati za vurugu.Amesema wanachama wa TLS wana wajibu wa kisheria kuhakikisha kunakuwa na marekebisho ya kimfumo kwa kufuata taratibu za kisheria, kisera na kimuundo.
Jebra amesema Mwabukusi alieleza kuwa pale wanapoona jambo haliko sawa, wajibu wao ni kulifanyia kazi na kupendekeza marekebisho yanayofaa, akisisitiza kuwa hakuna jambo ambalo Rais wa TLS amelizungumza bila kuwa na suluhisho analopendekeza.
Akifafanua namna TLS inavyotekeleza majukumu yake, Jebra amesema Mwabukusi alieleza kuwa chama hicho hufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kwamba pale kunapokuwa na jambo muhimu, taasisi husika huandikiwa barua rasmi huku akitolea mfano wa suala la Ngorongoro, akisema barua ziliandikwa na kuwasilishwa kwa taasisi husika, huku tume ya utafiti ikiundwa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, Jebra amesema licha ya Mwabukusi kuhojiwa kama shahidi, aliambiwa kuwa kabla ya kuondoka alitakiwa kujidhamini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza taratibu hizo za polisi, Mwabukusi amesema huu si wakati wa mawakili kunyamaza au kuogopa, bali ni wakati wa kusimamia utawala wa sheria na kutuma ujumbe kwa wale wanaofikiri wanaweza kuwatisha.
Mwabukusi amesema:“Huu ni wakati wa kuunguruma kwa sauti ambayo haijawahi kusikika katika taifa hili, sio wakati wa unyonge, ni wakati wa kuthibitisha maana halisi ya utawala wa sheria na naomba tutume ujumbe kwa wote wanaofikiri kwamba wanatubabaisha kwamba hatubabaiki, mimi binafsi sibabaiki, na naomba mawakili wote msibabaike.”
Ameendelea kusema kwamba TLS haiwezi kuendelea na shughuli zake kama kawaida kana kwamba kila kitu kiko sawa wakati, kwa mtazamo wake, kuna matatizo yanayoikabili taasisi hiyo.
Mwabukusi amesema chama hicho kinashambuliwa na watawala, akieleza kuwa shambulio analolizungumzia ni la wazi na la kimkakati, hivyo linapaswa kukabiliwa kwa hatua madhubuti.
“Hatuwezi kuendelea kawaida tu kama mambo yote yako sawa wakati mambo hayako sawasawa, taasisi inashambuliwa na watawala, shambhulio ni dhahiri na shambulio hili ni la kimkakati lazima tulikabili.”
Kutokana na hali hiyo, Mwabukusi amesema atakutana na Baraza la Uongozi la TLS ili kujadili na kuamua hatua za kuchukua, akionya kuwa hatua hizo zitakuwa nzito na za aina ambayo haijawahi kuchukuliwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
“Kwa iyo tunakaa na Baraza la Uongozi na tutachukua hatua nzito ambazo hazijawahi kuchukuliwa toka TLS iundwe.”
Katika hatua nyingine, Mwabukusi ametangaza kuwa atamchukulia hatua Jaji Mtulia kwa kumfikisha mbele ya Kamati ya nidhamu, akidai kuwa hawezi kukubali kuwepo kwa jaji ambaye, kwa maoni yake, haheshimu sheria na maamuzi ya mahakama.
Mwabukusi amesema jaji ni mtu anayetarajiwa kuheshimu sheria na maamuzi ya mahakama, akisisitiza kuwa mahakama ndiyo taasisi ambayo jaji anapaswa kuwa mfano wa kuilinda na kuheshimu maamuzi yake.
“Nitamchukulia hatua Jaji Mtulia, ninampeleka kwenye Kamati ya nidhamu kwa sababu hatuwezi kuwa na Jaji asiyeheshimu sheria, Jaji ni mtu tunaemtarajia haeshimu maamuzi ya Mahakama ambayo ndio nyumbani kwake.”
Ameongeza kuwa hatua hiyo haitakuwa ya kusitasita, akisisitiza kuwa atamfikisha jaji huyo mbele ya kamati husika.
“Kwa hiyo sio kwamba tutayumbayumba lazima tutamchukua na kumpeleka kwenye Kamati husika.








