, ,

Lissu aingia tatu bora kinyang’anyiro cha tuzo ya Sakharov 2026

Asia Gamba Avatar

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameingia katika orodha ya wagombea watatu wa mwisho wa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026 inayotolewa na Bunge la Ulaya, tuzo inayotambua mchango wa kipekee katika kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi.

Lissu amefikia hatua hiyo baada ya wajumbe wa kamati zinazoshughulikia masuala ya mambo ya nje na maendeleo katika Bunge la Ulaya kumchagua kutoka orodha ya awali ya wagombea sita.

Katika hatua ya mwisho, mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Tanzania atachuana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na maofisa wake, na dada mapacha kutoka Iran, Taraneh na Romina Rahimi, wanaowakilisha watu wanaokabiliwa na ukandamizaji nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu mchakato wa tuzo hiyo, washindi watatangazwa Alhamisi, Oktoba 22, 2026, na Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, anatarajiwa kutangaza jina la mshindi wakati wa kikao cha bunge hilo mjini Strasbourg, Ufaransa.

Uteuzi wa Lissu unakuja wakati kiongozi huyo akiwa mahabusu tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025, na akikabiliwa na kesi ya uhaini inayosikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam. Tuhuma zinazomkabili zinahusiana na madai ya kuchochea wananchi kuzuia uchaguzi, tuhuma ambazo hukumu yake ni kifo.

Wagombea wengine watatu waliokuwa katika orodha ya awali ni Rais wa El Salvador, Nayib Bukele; daktari wa watoto na mkurugenzi wa hospitali ya Gaza, Hussam Abu Safiya; pamoja na Standing Together, harakati ya pamoja ya raia wa Kiyahudi na Kipalestina nchini Israel.

Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ilianzishwa mwaka 1988 na hutolewa kila mwaka na Bunge la Ulaya kwa watu binafsi, makundi au taasisi zinazotambuliwa kwa juhudi zao za kutetea haki za binadamu, demokrasia na uhuru wa msingi.

Tuzo hiyo ina thamani ya euro 50,000, sawa na zaidi ya Shilingi milioni 148 za Tanzania, huku hafla ya kukabidhi tuzo ya mwaka huu ikitarajiwa kufanyika Desemba 16, 2026, mjini Strasbourg, Ufaransa.

Iwapo Lissu atashinda, utakuwa utambuzi wa kimataifa kwa kiongozi huyo wa upinzani katika masuala ya demokrasia na haki za binadamu, huku macho yakielekezwa Alhamisi kujua nani atakayenyakua tuzo hiyo mwaka huu.

Our Correspondent Avatar