, , , , , ,

Linda Mwananchi yalaani kutekwa kwa Mwaipaya, yaitaka serikali ya Kenya kubaini aliko mara moja

Victor Wanaswa Avatar

Vuguvugu la Linda Mwananchi limelaani kutekwa nyara kwa mwanaharakati wa upinzani wa Tanzania, Twaha Mwaipaya, eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, na kuitaka serikali ya Kenya kuchukua hatua za kubaini aliko na kumhakikishia usalama.

Vuguvugu hilo pia limeitaka serikali ya Kenya kuhakikisha usalama wa Mwaipaya, kukiwa na hofu kwamba huenda akasafirishwa kwa lazima hadi Tanzania, ambako maisha yake yanaweza kuwa hatarini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Amnesty International Kenya pamoja na Defenders Coalition, Mwaipaya alidaiwa kutekwa mwendo wa saa nane alasiri Jumapili alipokuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake.

Walioshuhudia walieleza kuwa watu waliohusishwa na tukio hilo walikuwa wakitumia magari matatu, yakiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop. Hata hivyo, utambulisho wa watu hao na mahali alipo mwanaharakati huyo haujabainika.

Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yamewaomba wananchi kutoa taarifa zozote zinazoweza kusaidia kubaini aliko Mwaipaya, huku yakizitaka mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wake.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Linda Mwananchi ililaani tukio hilo, ikisema linazua wasiwasi kuhusu usalama wa wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu kutoka nchi jirani wanaotafuta hifadhi nchini Kenya.

Vuguvugu hilo lilitaja kisa cha kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, ambaye alidaiwa kutekwa jijini Nairobi mwezi Novemba 2024 na kupelekwa Uganda, ambako alifikishwa katika mahakama ya kijeshi. Besigye bado anazuiliwa, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya na mazingira ya kizuizini.

Linda Mwananchi pia ilirejelea tukio la kutekwa kwa mwanaharakati wa Tanzania, Maria Sarungi Tsehai, na watu waliokuwa na silaha katika eneo la Kilimani jijini Nairobi, Januari 2025. Sarungi aliachiliwa baadaye siku hiyo kufuatia ghadhabu za umma na juhudi za watetezi wa haki za binadamu.

Sarungi, ambaye amekuwa akikosoa utawala wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameelezea hofu kwamba maisha ya Mwaipaya yanaweza kuwa hatarini iwapo atapelekwa nchini Tanzania.

Sarungi alionya kuwa huenda mwanaharakati huyo akauawa iwapo atavushwa hadi Tanzania, huku akitoa wito wa kuimarisha uangalizi katika mipaka ya nchi hizo mbili.

Linda Mwananchi imeshutumu utawala wa Rais William Ruto kwa kile ilichokitaja kuwa kuruhusu Kenya kugeuka kuwa eneo ambako watu wanaokimbia mateso ya kisiasa wanaweza kufuatiliwa, kutekwa na kurejeshwa katika nchi wanazohofia.

“Kenya imekuwa ikijivunia kuwa hifadhi salama ya watetezi wa demokrasia na haki za binadamu wanaokimbia dhuluma katika ukanda huu, ila kutekwa kwa Mwaipaya yanatishia sifa hiyo.” ilisema taarifa hiyo.

Linda Mwananchi sasa inataka serikali yar ais Ruto kuweka wazi aliko Mwaipaya mara moja, uchunguzi huru ufanywe kuhusu kutekwa kwake, na wote waliohusika wawajibishwe bila kujali nyadhifa zao au uraia wao.

Vuguvugu hilo limesisitiza kuwa Kenya inapaswa kuendelea kuwa katika mstari wa mbele katika kutetea demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wakati huo huo, Amnesty International Kenya na Defenders Coalition zimewataka wananchi walio na taarifa kuhusu aliko Mwaipaya kuzifikisha kwa mamlaka husika mara moja, huku wito ukiongezeka kwa serikali kuhakikisha usalama wake na kubaini mazingira ya kutoweka kwake.

 

 

Our Correspondent Avatar