, , , , ,

“Damu Yangu Ilimwagika Hapa”: Makovu ya Ghasia za Uchaguzi Tanzania Bado Yanauma Mwaka Mmoja Baadaye

Victor Wanaswa Avatar

Mwaka mmoja baada ya ghasia zilizohusishwa na uchaguzi nchini Tanzania, waathiriwa bado wanadai haki kuhusu hatma ya wapendwa wao waliouawa au kutoweka huku walionusurika wakikabiliwa na majeraha ya kudumu na gharama kubwa za matibabu.

Uchaguzi huo wa Oktoba 29, ambapo Rais Samia alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 98 ya kura baada ya viongozi wa uoinzani kuzuiwa kuwania nafasi mbalimbali, ulisababisha maandamano yaliyodumu kwa siku kadhaa. Maandamano hayo yalizimwa kwa nguvu ya mtutu wa bunduki na jeshi la polisi.

Matokeo ya hatua ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi ilikuwa maelfu kupoteza Maisha yao na wengine wengi kupata majeraha mabaya.

(FILES) Tanzanian police officers try to disperse protesters amid clashes in Dar es Salaam on October 29, 2025, during Tanzania’s presidential elections.  (Photo by AFP)

Kwa familia nyingi na manusura kumbukumbu za gahsia hizo bado ni sehemu ya Maisha yao ya kila siku. Wanasema maswali kuhusu haki, uwajibikaji na msaada kwa waathiriwa bado hayajapata majibu.

Joseph Zakayo, mwenye umri wa miaka 37, anaonyesha kovu kubwa kwenye paja lake alipopigwa risasi wakati wa machafuko hayo. Sasa hawezi tena kuendesha biashara yake ya bodaboda.

“Maisha yangu yamerudi nyuma sana,” alisema Zakayo.

Kwa Twaha Bomeza, mwenye umri wa miaka 61, maisha yake yalibadilika ghafla siku ya uchaguzi baada ya vipande vya risasi kumuingia jichoni wakati wa makabiliano ya risasi yaliyolenga kuwatawanya waandamanaji. Sasa anahitaji kufanyiwa upasuaji ambao hana uwezo wa kuugharamia.

“Nilijaribu kujiokoa, lakini nikapigwa risasi. Nilianguka hapa na kupoteza meno manne ya mbele,” Bomeza alisema akiwa katika mitaa ya Dar es Salaam, jiji kuu la kibiashara nchini Tanzania, huku akionyesha meno yake ya bandia.

“Bado ninaugulia jeraha la ndani kwenye macho yangu,” alisema, akiongeza kuwa kwa sasa anasumbuliwa na upungufu wa pumzi na maumivu ya kichwa yasiyokoma.

“Damu yangu ilimwagika hapa, lakini mwaka mmoja umepita na sasa damu haipo hapa,” aliongeza Bomeza.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na upinzani yanasema maelfu ya watu waliuawa, huku tume iliyoteuliwa na serikali ikikadiria idadi ya waliofariki kuwa 518.

Kwa upande mwingine wanaharakati, viongozi wa upinzani na wakosoaji wa serikali wanaishi kwa hofu ya kutekwa nyara, kukamatwa kiholela au kushtakiwa kwa makosa ya uhaini na ugaidi.

“Wanajaribu kuwanyamazisha wakosoaji wote na viongozi wa upinzani ili kuhakikisha kuwa hakuna mengi yatakayotokea kuhusiana na matukio hayo mawili,” alisema Fulgence Masawe, mkurugenzi wa utetezi na mageuzi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Masawe alisema kuwa taasisi yake inawakilisha takribani watu 56 wanaokabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi.

Serikali ya Tanzania ilibuni tume ya rais kuchunguza ghasia za mwaka jana zilizosababisha vifo vya watu wengi, lakini hadi sasa hakuna hatua kubwa iliyopigwa. Wakosoaji wanasema tume hiyo ilibuniwa kwa nia isiyo ya dhati, kwa lengo la kuisaidia serikali “kusafisha taswira ya Tanzania” katika medani za kimataifa.

“Serikali inajaribu kukana na kufuta historia ya kuhusika kwake katika mauaji ya halaiki iliyotekeleza mwaka jana,” alisema Tito Magoti.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeikosoa Tanzania kwa kushindwa kuwawajibisha waliohusika na ghasia hizo, likisema badala yake serikali imekuwa “ikitumia vibaya sheria za kupambana na ugaidi kama silaha ya kuwanyamazisha wakosoaji na kupandikiza hofu.”

Licha ya serikali kukandamiza juhudi za kuadhimisha kumbukumbu za ghasia hizo, wengi bado wana makovu yanayowakumbusha yaliyotokea.

Kanisa Katoliki limetoa wito wa kufanyika kwa misa nchini kote kwa heshima ya waathiriwa, huku chama kikuu cha upinzani, Chadema, kikitangaza siku saba za maombolezo.

Hata hivyo, polisi wameonya dhidi ya mipango yoyote ya kuhamasisha watu kwa kile walichokiita vitendo vya “kihalifu”, licha ya tume ya rais kupendekeza kuwekwa kwa kumbukumbu ya kuwakumbuka waathiriwa.

Wachambuzi kadhaa waliozungumza wanasema Tanzania iko katika hali ya “tahadhari na mvutano”, huku kukamatwa kwa watu kiholela kukiongezeka.

“Nchi haiko tu katika hali ya maombolezo, bali pia katika hali ya hofu kubwa. Tunaishi kwa wasiwasi na mashaka kila wakati,” alisema mtetezi wa haki za binadamu Tito Magoti.

Katika wiki iliyopita, kiongozi mwandamizi wa upinzani John Pambalu alishtakiwa kwa uhaini, huku mkosoaji wa serikali ya Tanzania, Twaha Mwaipaya, akidaiwa kutekwa nyara nchini Kenya na hadi sasa hajulikani aliko.

“Serikali ina wasiwasi mkubwa na iko tayari kutumia nguvu kupita kiasi kukandamiza jambo lolote linaloweza kupangwa kuhusiana na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu ghasia hizo,” alisema Anna Bwana, mkurugenzi wa shirika la kiraia la Twaweza Afrika Mashariki.

“Unapoadhimisha, unakiri kuwa yaliyotokea yalitokea na unatambua idadi ya watu waliopoteza maisha yao. Lakini unawezaje kufanya maadhimisho huku watu wengine wakiendelea kutekwa nyara?” aliuliza.

Aliongeza kuwa watu wengi bado hawajapata fursa ya kuwazika wapendwa wao.

Jambo jingine linaloweza kuongeza mvutano ni kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA Tundu Lissu, ambaye hukumu yake inatarajiwa kutolewa Novemba 6.

Our Correspondent Avatar