Familia ya Alute Mughwai Lissu, kaka yake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imesema mazishi ya ndugu yao yatafanyika baada ya Novemba 6, 2026, siku inayotarajiwa kutolewa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili ndugu yao huyo.Uamuzi huo umefikiwa ili kuwawezesha wanafamilia kusafiri kwenda Dar es Salaam na kushiriki katika usikilizaji wa hukumu hiyo itakayotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Dk. Vincent, mmoja wa ndugu wa familia hiyo, amesema wamekubaliana kusogeza mbele mazishi ili familia iweze kuwa pamoja wakati wa kusikiliza hukumu ya kesi ya Tundu Lissu.“Tumepanga mazishi ya kaka Alute yatafanyika Singida. Tunatarajia tutasukuma mbele mazishi ili Ijumaa (Novemba 6, 2026), wanafamilia tuweze kuwepo Dar es Salaam kuhudhuria hukumu ya kesi ya ndugu yetu Tundu,” amesema Dk. Vincent.Alute alifariki dunia Jumamosi usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu. Katika siku zake za mwisho, alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, huku hali yake ikielezwa kuzidi kuwa mbaya kuanzia siku mbili kabla ya kifo chake.Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, baada ya wanafamilia kushiriki katika shughuli za usomaji wa hukumu ya kesi ya Tundu Lissu.Tundu Lissu amekuwa mahabusu tangu Aprili 9, 2025, alipokamatwa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, na kufunguliwa mashtaka ya uhaini yanayohusishwa na matamshi aliyodaiwa kutoa kuhusu uchaguzi mkuu.Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kusomwa Novemba 6, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya hatua za usikilizwaji wa ushahidi na hoja za mwisho za pande zote kukamilika.
Mazishi ya Alute Lissu kufanyika baada ya hukumu ya Tundu Lissu







