ACT Wazalendo yapinga matokea ya uchaguzi mdogo wa ubunge Mbarali

Chama upinzani nchini Tanzania chama cha ACT Wazalendo kimesema hakikubaliani na matokeo ya Ubunge yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo  (NEC) na kutangazwa leo na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali Ndugu Missana K. Kwangura, ambapo Chama cha Mapinduzi kimeshinda uchaguzi huo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbarali ambapo alimtangaza ndugu Bahati Keneth Ndingo kwa kura 44334 dhidi ya kura 10014 za Modestus Kirufi wa ACT Wazalendo.

“Uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi sana. Mosi, Msimamizi wa Uchaguzi alivuruga sana zoezi la kuapisha mawakala. Maeneo ambayo aliahidi kuja kuapisha mchana alifika usiku. Hiyo ilisababisha baadhi ya Mawakala wetu na wa vyama vingine wasiapishwe. Lakini hata CCM iliapisha mawakala wachache sana kuliko ACT Wazalendo. Cha kustaajabisha, asubuhi ya siku ya kupiga kura, CCM ilikuwa na mawakala katika vituo vyote” alisema Ndugu Ado.

“Pili, CCM ilitumia vituo ambavyo mawakala wetu walizuiwa, kuweka matokeo ya uongo. Ni jambo la kustaajabisha eneo lenye vyumba vitatu, vyumba vyenye mawakala vina mahudhurio hafifu lakini chumba ambacho hakina mawakala kinapewa mahudhurio ya asilimia 100 au zaidi” aliongezea Ado na kusisitiza:

“Maombi yetu ya kutaka vituo vyote vyenye utata masunduku yake yahesabiwe upya yalipingwa na Msimamizi wa Uchaguzi. Tunatafakari kuangalia hatua za kuchukua ikiwemo kuyapinga matokeo haya mahakamani”.

Marudi ya uchaguzi huo ni kufuatia aliyekuwa Mbunge Mbarali Francis Mtega kufariki dunia kwa ajali ya treka dogo aina ya Power Tillar.

 Ado amesema kuwa kasoro zinazojitokeza kwenye chaguzi za marudio zinaitia doa Serikali ya Awamu ya Sita hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Amesema kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitafanya uchambuzi wa kina wa kasoro zilizojitokeza kwenye Chaguzi zote za marudio na kuandaa Ripoti Maalum itayowasilishwa kwa wadau ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa.

Naye Mgombea wa Ubunge Ndugu Modestus Dickson Kirufi amesema uchaguzi umekuwa na kasoro nyingi na ni muhimu mamlaka zinazohusika ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi zifanyie kazi kasoro hizo. Pia amesema anasikiliza msimamo wa Chama kujua hatua inayofuata baada ya matokeo kutangazwa.

Katika uchaguzi huo vyama 13 vilishirki isipokuwa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA wao walisusia uchaguzi huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchaguzi kufanyika chini ya sheria ambazo bado hazifanyiwa marekebisho