, , ,

Basata Yamfungia Harmonize Kufanya Mziki, Yapiga Faini Wengine Akiwemo Nandy

Wadh Kassim Avatar

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limechukua hatua dhidi ya wasanii na waandaaji wa matukio ya sanaa kwa tuhuma za kukiuka maadili ya sanaa nchini, huku Harmonize na Nandy wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa hatua.

Basata Yamfungia Harmonize Kufanya Mziki, Yapiga Faini Wengine Akiwemo Nandy

Harmonize amesitishiwa kujishughulisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi ya BASATA, ikiwemo kulipa faini ya shilingi milioni tano ndani ya siku 14 na kuondoa video ya wimbo wake Kudos kwenye mitandao yote nchini.

BASATA imesema wimbo huo hauzingatii maadili ya Mtanzania na unakiuka heshima kwa mtazamaji na msikilizaji.

Muongozaji wa video hiyo, Kennedy Sanga, naye amechukuliwa hatua zinazofanana, ikiwemo kusitishiwa kujishughulisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa na BASATA.

Kwa upande wa Nandy, BASATA imemchukulia hatua kwa tuhuma za kukiuka maadili kutokana na mavazi aliyovaa wakati akitumbuiza katika fainali za Miss Universe Tanzania 2026.

Nandy amekiri kosa, akaondoa video hiyo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kulipa faini ya shilingi milioni tatu, hatua iliyomfanya aruhusiwe kuendelea na shughuli za sanaa chini ya uangalizi wa BASATA.

Aidha, BASATA imechukua hatua dhidi ya mwandaaji wa mashindano ya Miss Grand Tanzania kwa kuendesha mashindano hayo bila kibali cha BASATA, ambapo mwandaaji huyo ameagizwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu na kusitisha kujishughulisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.

Hatua nyingine imechukuliwa dhidi ya mwandaaji wa Miss Universe Tanzania kwa kumruhusu Nandy kutumbuiza akiwa amevaa mavazi ambayo BASATA imeyataja kuwa hayakuwa na maadili.

Mwandaaji huyo ameagizwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu, huku akipewa onyo kali na kutakiwa kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisanaa.

Our Correspondent Avatar