Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakijawahi kufanya mazungumzo ya siri na serikali kuhusu maridhiano ya kisiasa, kikisisitiza kuwa msimamo wake unabaki ule ule wa kutaka Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuachiwa huru bila masharti kabla ya hatua nyingine zozote za kisiasa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika amesema kauli iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wake na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu kuwepo kwa “mwenzetu anayeendelea kutafakari” imezua tafsiri mbalimbali, lakini kwa mtazamo wa chama hicho haimaanishi kuwa tayari kuna makubaliano kati ya pande hizo.
Mnyika amesema CHADEMA haijawahi kuingia katika makubaliano ya faragha na serikali na kwamba misimamo yake yote imekuwa ikitangazwa hadharani kupitia maazimio ya Kamati Kuu ya chama. Amesisitiza kuwa msimamo wa chama unabaki kutaka Lissu aachiliwe huru, ukweli na uwajibikaji upatikane kuhusu matukio yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, pamoja na kupatikana kwa katiba mpya itakayoweka mazingira ya uchaguzi huru na taasisi zinazojitegemea.
Katibu huyo mkuu amesema CHADEMA bado kinaamini Lissu hana hatia katika kesi inayomkabili na kimetoa wito kwa wanachama pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam tarehe 10 Agosti, wakati kesi yake itakapoitwa.
Aidha, amesema taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa afya ya Lissu imezorota kwa kiwango fulani, akidai kuwa kutokana na maumivu ya nyonga na sehemu nyingine za mwili, ameshindwa kuendelea na kiwango cha mazoezi aliyokuwa akifanya akiwa mahabusu.
Mnyika pia amekosoa kauli ya Rais Samia kuhusu kuanzishwa kwa tume ya maridhiano na kushughulikia suala la katiba mpya, akisema haiwezi kutafsiriwa kuwa mwanzo wa maridhiano ya kweli wakati mwenyekiti wa chama hicho bado yuko gerezani na viongozi wengine wa CHADEMA wanaendelea kukabiliwa na kesi mbalimbali.
Kwa mujibu wake, chama hicho hakijawahi kubadili msimamo wake wala kufanya mazungumzo ya siri, huku akidai kuwa kauli hizo zinaweza kuleta taswira isiyoendana na hali halisi ya kisiasa nchini.
CHADEMA pia kimetoa wito kwa jumuiya mbalimbali za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Madola pamoja na wadau wengine kuendelea kufuatilia hali ya demokrasia nchini Tanzania.
Mnyika amesema chama hicho kinaamini bado kuna umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu matukio ya baada ya uchaguzi na kuhakikisha misingi ya utawala wa sheria inazingatiwa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Mnyika amesema kwa takwimu za chama hadi jana, wanachama na viongozi 63 wa CHADEMA walikuwa wamekamatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali.
Amesema chama kinaamini kesi hizo zina misingi ya kisiasa na kimemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutumia mamlaka yake kusitisha mashauri hayo.
Katika hatua nyingine, Mnyika amewashukuru wanachama na wafuasi wa CHADEMA kwa kuendelea kuchangia fedha kwa ajili ya maandalizi ya Baraza Kuu la chama. Amesema bado zinahitajika takribani shilingi milioni 68 kukamilisha maandalizi hayo na kusisitiza kuwa michango yote ipitie katika akaunti rasmi za chama ili kuhakikisha uwajibikaji.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini kushiriki katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa nchini, akisema Tanzania inahitaji uponyaji wa kitaifa na upatanisho unaojengwa katika misingi ya haki na uadilifu.