Chadema yadai Tundu Lissu yuko hatarini gerezani, yataka hatua za haraka

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimepokea taarifa kinazodai zinaashiria kuwepo kwa tishio dhidi ya usalama wa Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, ambaye anaendelea kushikiliwa katika Gereza la Ukonga, na kuitaka serikali pamoja na Jeshi la Magereza kuchukua hatua za haraka kuhakikisha analindwa.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu, Julai 27, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, CHADEMA imesema imepokea taarifa kutoka kwa shirika la World Liberty Congress, linalojihusisha na masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, zikieleza kuwepo kwa hofu kuhusu usalama wa Lissu.

Kwa mujibu wa chama hicho, taarifa hizo zimeongeza wasiwasi kuhusu hali ya Lissu akiwa gerezani, hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa kizuizini kwa zaidi ya siku 470.

CHADEMA imeeleza kuwa katika kipindi hicho, Lissu amekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, kwa mujibu wa chama hicho, kunyimwa fursa ya kuonana kwa faragha na mawakili wake, madai ya kuwepo kwa njama za kumdhuru, pamoja na kile ilichodai ni mashitaka yenye misingi ya kisiasa kutokana na msimamo wake kuhusu demokrasia, haki za binadamu, mageuzi ya Katiba na utawala wa sheria.

Katika taarifa hiyo, chama hicho kimesisitiza kuwa Jeshi la Magereza lina wajibu wa kikatiba na kisheria kuhakikisha usalama wa wafungwa wote, na kwamba halitakubali tishio lolote dhidi ya maisha ya Mwenyekiti wake akiwa chini ya ulinzi wa dola.

CHADEMA pia imemtaka Mkuu wa Gereza la Ukonga kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa Lissu unalindwa na kutoa taarifa kuhusu hali yake, huku ikisisitiza kuwa haki zake za kikatiba na za kibinadamu zinapaswa kuheshimiwa kikamilifu.

Aidha, chama hicho kimerudia wito wake wa kutaka Lissu aachiwe huru bila masharti, kikidai kuwa si mhalifu na kwamba hana hatia yoyote.

Katika hatua nyingine, CHADEMA imezitaka jumuiya za kimataifa, taasisi zinazotetea demokrasia na haki za binadamu pamoja na mashirika ya kidiplomasia kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Lissu na kutumia njia za kidiplomasia na kisheria kuhakikisha haki zake zinalindwa.

Tundu Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA, anaendelea kushikiliwa akikabiliwa na kesi ya uhaini. Kesi hiyo imeendelea kuvuta hisia za wadau wa ndani na nje ya Tanzania, huku chama chake na wafuasi wake wakisisitiza kuwa haki zake za msingi zinapaswa kulindwa wakati mchakato wa kisheria ukiendelea.