Heche Aeleza Mauaji, Vurugu za Uchaguzi Katika Utetezi wa Lissu

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, ameeleza Mahakama mazingira ya chaguzi mbalimbali nchini alizodai ziliambatana na mauaji, kuenguliwa kwa wagombea na kuingiliwa kwa shughuli za chama, akisema matukio hayo ni sehemu ya sababu zilizokifanya chama hicho kuchukua msimamo wa “No Reforms, No Elections”.

Heche Aeleza Mauaji, Vurugu za Uchaguzi Katika Utetezi wa Lissu

Heche ametoa ushahidi huo jana Septemba 9,2026, katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, huku akieleza kuwa chama hicho kilianza kujadili kwa kina changamoto za uchaguzi baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, ambao alidai uliambatana na kuenguliwa kwa wagombea wa CHADEMA na mauaji ya baadhi ya watu.Akieleza mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa jaji Dastun Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde Heche alisema Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana Desemba 3, 2024 chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe na kujadili matukio hayo, kabla ya chama kuchukua msimamo wa kutaka mageuzi ya kikatiba na kisheria yafanyike kabla ya uchaguzi. Miongoni mwa mabadiliko aliyoyataja ni kuondoa baadhi ya mamlaka ya Rais na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.Heche, ambaye amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA tangu mwaka 2011 na sasa ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, alisema uzoefu wake wa kushiriki chaguzi kama mgombea na kiongozi wa chama umemfanya kushuhudia changamoto mbalimbali, ikiwamo kuenguliwa kwa wagombea, kunyimwa fomu za mawakala, kuondolewa kwa mawakala vituoni na kuvurugwa kwa mikutano ya kampeni.Katika ushahidi wake, Heche alitaja pia matukio kadhaa ya mauaji aliyodai yalitokea wakati wa shughuli za kisiasa na uchaguzi.

Alieleza kuhusu kifo cha Akwelina Akwelina mwaka 2018, akisema wakati huo polisi walikuwa wamewashambulia watu waliokuwa wakifuatilia masuala ya viapo vya mawakala, huku akidai baadaye viongozi wa CHADEMA kukamatwa badala ya askari ambao ndio watuhumiwa wa mauaji hayo.Alieleza pia mauaji ya Alphonce Mawazo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015, pamoja na matukio ya mwaka 2020 katika eneo la Nyamongo, ambako alisema watu wawili waliuawa wakati wa kufungwa kwa kampeni za uchaguzi. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika na mauaji ya Mawazo, alisema hakumbuki vizuri kilichofuatia na hivyo hakuweza kutoa maelezo zaidi.Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Heche alieleza kuhusu kifo cha mdogo wake, Suguta Heche, akidai alikamatwa na polisi mwaka 2018 na baadaye kuuawa.

Heche alisema RPC wa wakati huo alitoa taarifa kwamba Suguta aliuawa na askari polisi na akaahidi kuchukua hatua, lakini kwa mujibu wa ushahidi wake, askari huyo aliachiwa na baadaye kuhamishwa kituo na bado anaendelea kuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi.Akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Heche alisema alishuhudia pia kile alichodai kuwa ni matumizi ya nguvu na polisi katika kampeni za Lissu, akisema mkutano wa kufunga kampeni Nyamongo ulizuiwa kwa mabomu ya machozi na kusababisha vurugu kati ya polisi na wananchi. Alidai kuwa matukio kama hayo hayakuwakuta wagombea wa CCM kwa kiwango alichokiona kwa upande wa CHADEMA.Ushahidi wa Heche unakuja katika hatua ya utetezi wa Lissu, ambaye anakabiliwa na shtaka la uhaini linalohusishwa na kauli alizodaiwa kutoa Aprili 3, 2025 kuhusu msimamo wa “No Reforms, No Elections”. Kwa mujibu wa mashtaka, Lissu anadaiwa kuhamasisha umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikiwemo kupitia kauli zinazohusishwa na “kuzuia uchaguzi” na “kuhamasisha uasi”.Hata hivyo, ushahidi wa Heche umejikita katika kueleza historia na mazingira ambayo CHADEMA ilifikia msimamo huo, akieleza kuwa madai ya mageuzi ya uchaguzi yalitokana na uzoefu wa chama hicho katika chaguzi zilizopita na si suala lililoibuka Aprili 3, 2025 pekee.Kesi hii inaendelea leo katika Mahakama Kuu Dar es Salaam, ambapo Heche ataendelea kutoa ushahidi wake wa msingi akiwa ni shahidi wa tano kati ya mashahidi 12 wa Lissu