
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameshinda uchaguzi wa urais na kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa, Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) imetangaza leo Jumanne.
Uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini ya shaba ulikuwa kwa kiasi kikubwa wa amani, ingawa mchakato wa kuelekea uchaguzi huo ulitawaliwa na madai ya vitisho, kukamatwa kwa wapinzani, vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Ushindi wa Hichilema, mwenye umri wa miaka 64, ulitarajiwa kwa kiasi kikubwa. Alikuwa akikabiliwa na wagombea 13, akiwemo aliyekuwa waziri wa zamani wa mkoa, Brian Mundubile, ambaye alikuwa akigombea urais kwa mara ya kwanza.
Mundubile, mwenye umri wa miaka 55, amepata karibu asilimia 38 ya kura, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Mwangala Zaloumis.
Zaloumis amesema kura kutoka majimbo matano kati ya 226 bado hazijajumlishwa, lakini akaongeza kuwa kura hizo haziwezi kubadili kwa kiasi kikubwa matokeo yaliyotangazwa.
Baada ya kutangazwa kwa ushindi wake, Hichilema alisema amenyenyekezwa na imani ambayo wananchi wameiweka kwake.
“Kwa kweli tumenyenyekea kutokana na imani ambayo mmeiweka mikononi mwetu,” alisema Hichilema.
Aliongeza kuwa serikali yake itasikiliza pia wananchi waliounga mkono vyama vya upinzani na kuendelea kuwafanyia kazi.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo, mamia ya wafuasi wa chama cha Hichilema, UPND, waliingia mitaani katika mji mkuu Lusaka wakiwa wamevalia rangi nyekundu za chama hicho, wakishangilia, kuimba na kucheza huku wakifyatua fataki.
-Madai ya ukiukwaji wa taratibu-
Kabla ya matokeo kutangazwa, Mundubile alidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa kuhesabu kura.Alidai, bila kutoa ushahidi, kwamba baadhi ya nyaraka zilizokuwa zikionyesha matokeo zilichezewa, jambo ambalo alisema lilihatarisha uadilifu wa mchakato wa kujumlisha kura.
Pia alidai kuwa kulikuwa na taarifa kwamba baadhi ya maafisa katika Mkoa wa Kusini walishinikizwa kubadilisha baadhi ya takwimu za kura.
Madai hayo yalitolewa wakati chama chake cha NRPUP kikikanusha kwa nguvu tuhuma za serikali kwamba baadhi ya wanachama wake walihusika katika shughuli za kijeshi au uasi wa kutumia silaha.
Serikali ya Zambia ilitangaza Jumapili kuwa polisi walikuwa wamewakamata watu 11, akiwemo viongozi sita wa upinzani, katika operesheni iliyolenga kile ilichokiita “shughuli za wanamgambo”.
Kwa mujibu wa serikali, watuhumiwa walikutwa na silaha za kijeshi, risasi na vifaa vingine vilivyodaiwa kutumika katika uasi wa kutumia silaha.
NRPUP ilisema milio ya risasi ilisikika wakati wa uvamizi huo uliofanyika nyumbani kwa Mundubile, na kwamba mbunge mmoja alipigwa.
Chama hicho kilikanusha kabisa madai ya serikali kwamba uongozi au wanachama wake walihusika katika uasi, shughuli za wanamgambo au vitendo vingine vinavyohusiana na uasi wa kutumia silaha.
-Kuhesabu kura kwasimamishwa-

Tume ya Uchaguzi ya Zambia pia imekosolewa baada ya kusimamisha kwa takribani saa sita mchakato wa kuhesabu kura siku ya Ijumaa.
Uamuzi huo ulifuatia taarifa za vurugu dhidi ya maafisa wa uchaguzi pamoja na madai ya kuibiwa kwa baadhi ya karatasi za kura.
Tume ilisema mchakato huo ulirejeshwa baada ya “tishio la kiusalama” kudhibitiwa.
Waangalizi wa kimataifa, akiwemo ujumbe wa Umoja wa Ulaya, walisema kusimamishwa kwa zoezi hilo kulihatarisha uaminifu wa mchakato wa uchaguzi pamoja na imani ya wapiga kura.
Waangalizi hao pia walionya kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya vyama vya upinzani wakati wa kampeni huenda vilisababisha ushindani usio sawa.
Taasisi ya Oxford Economics Africa ilisema matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi, yakiwemo kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani, yameibua maswali makubwa kuhusu uadilifu wa matokeo.
-Uchumi na maisha ya wananchi-
Uchaguzi huo pia ulionekana kuwa mtihani kwa kipindi cha kwanza cha miaka mitano cha Hichilema madarakani, ambacho kimeshuhudia uchumi wa Zambia kurejea katika ukuaji.
Hichilema amekuwa akitaja mchakato wa marekebisho ya deni la taifa na kupungua kwa mfumuko wa bei miongoni mwa mafanikio makubwa ya serikali yake.
Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema mafanikio hayo bado hayajatafsiriwa kikamilifu katika kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 70 ya watu milioni 22 wa Zambia wanaishi kwa chini ya dola tatu za Marekani kwa siku.
Zambia ni nchi ya pili kwa uzalishaji mkubwa wa shaba barani Afrika na ina historia ndefu ya kubadilisha madaraka kwa njia ya amani kupitia sanduku la kura.
Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, kila mabadiliko ya rais nchini humo yamefanyika kupitia uchaguzi.