IGP Wambura, DCI Kingai, CDF Mkunda Kuja Kutoa Utetezi Dhidi ya Lissu

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubali ombi la Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, la kuwaita Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camilius Wambura, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI Ramadhani Kingai na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama CDF. Generali Jacob John Mkunda, kuwa mashahidi wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili.

IGP Wambura, DCI Kingai, CDF Mkunda Kuja Kutoa Utetezi Dhidi ya Lissu

Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 10, 2026, baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote kuhusu ombi la Lissu la kutaka Mahakama itoe wito kwa mashahidi aliowataja ili wafike kutoa ushahidi katika hatua ya utetezi.Lissu alikuwa ametaja orodha ya mashahidi 11 wa utetezi kuwa mashahidi wake, ambapo wa kwanza akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP. Camilius Wambura, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Generali Jacob Mkunda Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Suleiman Mombo, na DCI Ramadhani Kingai. Wengine aliwataja Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Chadema.Baada ya kutaja majina hayo, Lissu aliomba Mahakama itoe wito kwa mashahidi hao.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo, ukirejea Kifungu cha 281(1) pamoja na Kifungu cha 314 cha Sheria inayoeleza hiari ya Mahakama, ukidai kuwa mashahidi hao hawakupaswa kuitwa kwa namna iliyoombwa na utetezi.Jamhuri iliwasilisha hoja sita za kupinga wito huo. Miongoni mwa hoja hizo ilikuwa kwamba wakati shauri lilipokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mashahidi hao hawakuorodheshwa kwa mujibu wa utaratibu uliotakiwa, hivyo kasoro hiyo haiwezi kutibiwa katika hatua hii ya kesi ya msingi.Upande wa mashtaka pia ulipinga baadhi ya mashahidi kwa hoja kwamba ushahidi wao hauna uhusiano wa moja kwa moja (relevance) na mashtaka yanayomkabili Lissu. Kwa mujibu wa hoja hiyo, jukumu la kuthibitisha mashtaka ni la Jamhuri na si la mshtakiwa, hivyo baadhi ya mashahidi waliopendekezwa hawakuwa na ulazima wa kuitwa.Kwa upande wake, Lissu aliiambia Mahakama kuwa mashahidi aliowataja ni muhimu katika utetezi wake na kwamba kuwaita ni sehemu ya haki yake ya kikatiba ya kujitetea. Alisisitiza kuwa hakuna sheria inayowazuia viongozi hao kuitwa mahakamani endapo wana ushahidi unaohusiana na shauri.Lissu pia alieleza kuwa baadhi ya mashahidi hao, akiwamo Rais na viongozi wengine wa vyombo vya dola, wanaweza kuwa na taarifa muhimu zinazohusiana na tuhuma zinazomkabili, hasa kwa kuzingatia kwamba shtaka lenyewe linahusu madai ya kutishia Serikali.Katika kutolea uamuzi hoja hizo, Mahakama imekubaliana na sehemu ya hoja za Jamhuri kwamba kutotajwa kwa mashahidi hao katika hatua za awali za shauri katika Mahakama ya Kisutu ni jambo ambalo haliwezi kurekebishwa kwa hoja kwamba baadaye walitajwa katika Mahakama Kuu.Hata hivyo, Mahakama imesisitiza kuwa suala la msingi katika kuamua kama shahidi aitwe ni pamoja na kuangalia umuhimu na uhusiano wa ushahidi wake na shauri.Katika mazingira hayo, Mahakama imeona kuwa IGP, DCI na Mkuu wa Majeshi ni mashahidi wenye uhusiano “relevance” katika kesi hiyo na kwamba wanaweza kuitwa na upande wa utetezi.Kwa uamuzi huo, Lissu sasa ameruhusiwa kuendelea na hatua ya utetezi akiwa na uwezekano wa kuwaita viongozi hao watatu kutoa ushahidi katika kesi hiyo.Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la Lissu la kupewa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Philip Mpango, Kassim Majaliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa.Kuhusu baadhi ya mashahidi hao, Mahakama imeeleza kuwa hoja ya iwapo viongozi hao walitishwa au hawakutishwa haiwezi kuwa msingi wa kuwaita mahakamani, kwa sababu hati ya mashtaka inahusisha madai kwamba Lissu alitengeneza nia ya kutenda kosa, badala ya kuwa msingi wa kesi kuwa viongozi hao walithibitisha kwamba walihisi kutishwa.Mahakama pia imeitofautisha kesi hiyo na shauri la Khatibu Ghandi lililotumiwa na Lissu katika hoja zake, ikieleza kuwa katika shauri hilo shahidi aliyerejelewa alikuwa ameitwa na upande wa mashtaka, tofauti na mazingira ya kesi ya sasa ambako Lissu anataka mashahidi hao waitwe na upande wa utetezi.Lissu ambaye ni Mwanasiasa mashughuli wa Upinzani na mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Tanzania, anakabiliwa na kesi ya uhaini akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali, kinyume na  kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) Rekebu ya mwaka 2023.Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika (kuchapisha) mtandaoni maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.Maneno hayo yanayodaiwa kuwa ya uhaini, Lissu alitamka kuwa : “Wanasema kitu kimoja hapa, msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”