Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Mulago mjini Kampala baada ya kuanguka akiwa mahakamani, mkewe Winnie Byanyima na vyanzo vya hospitali vimethibitisha.
Besigye mwenye umri wa miaka 70, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini kwa madai ya kupanga njama dhidi ya Rais Yoweri Museveni, alianguka Jumatano wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake baada ya kukataa mawakili aliopangiwa na serikali. Kabla ya kuanguka, alikuwa akilalamikia kuzuiwa kwa mawakili wake binafsi kumwakilisha.
Kupitia ukurasa wake wa X, mke wake Winnie Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), amesema Besigye amelazwa ICU akiwa hana fahamu, hawezi kuzungumza na hata hashituki anapochochewa kwa maumivu.
Msemaji wa Hospitali ya Mulago, Gladys Baligonzaki Kajura, amethibitisha kuwa Besigye amelazwa hospitalini na kwamba madaktari wanaendelea kumpatia matibabu, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu hali yake.
Chanzo cha kitabibu kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kimesema Besigye alifikishwa hospitalini Jumatano jioni akiwa katika hali mbaya na asiyeitikia mwitikio wowote.
Besigye, ambaye aliwahi kuwa daktari binafsi wa Rais Museveni kabla ya kujiunga na upinzani zaidi ya miaka 25 iliyopita, amekuwa akikabiliwa na hatua mbalimbali za serikali.
Mwaka 2024 alitekwa nchini Kenya na baadaye kuibuka Uganda, ambako awali alifikishwa katika mahakama ya kijeshi kabla ya kesi yake kuhamishiwa mahakama ya kiraia.
Kabla ya kuanguka kwake, mmoja wa mawakili wake, meya wa zamani wa Kampala Erias Lukwago, alikamatwa, huku wakili mwingine, aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kenya Martha Karua, akizuiwa kuingia Uganda.
Wakati huo huo, mahakama ya Uganda Alhamisi imekataa kwa mara nyingine ombi la kumwachia Lukwago kwa dhamana. Anakabiliwa na shtaka la kushindwa kutoa taarifa kuhusu kosa la uhaini, baada ya kudaiwa kukamatwa na jeshi nyumbani kwake.
Katika miezi ya hivi karibuni, Uganda imekuwa ikikosolewa kwa kuongeza ukandamizaji dhidi ya viongozi wa upinzani, mawakili na vyombo vya habari huru.
Hii ni mara ya tatu kwa Besigye kulazwa hospitalini tangu alipowekwa kizuizini. Mwezi Februari 2025 alipelekwa hospitalini baada ya mgomo wa kula, na baadaye akalazwa tena mapema mwaka huu. Mke wake ameendelea kulaani mazingira ya kizuizini anayoshikiliwa, akiyataja kuwa yasiyo ya kibinadamu na kudai kuwa kuna njama za kutaka kumuua.