Kwa nini Kenya imeendelea kuwa kimbilio la wanaharakati wa kisiasa licha ya hofu ya utekaji?

Kwa miongo kadhaa, Kenya imekuwa ikitajwa kama moja ya nchi salama zaidi kwa wanasiasa wa upinzani, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki. Wanaokimbia vitisho, kukamatwa au mashitaka ya kisiasa kutoka Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Ethiopia na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mara nyingi huelekea Nairobi wakiamini watapata usalama na nafasi ya kuendelea na shughuli zao.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, taswira hiyo imeanza kutikiswa. 

Kenya yenyewe imekuwa ikikumbwa na tuhuma za kuongezeka kwa matukio ya utekaji wa wakosoaji wa serikali na wanaharakati. Hali hiyo imeibua swali muhimu: ikiwa hata Kenya kuna hofu ya kutekwa, kwa nini bado ndiyo chaguo la kwanza kwa wanaokimbia ukandamizaji wa kisiasa katika ukanda huu?

Simulizi ya David Djumbe

David Djumbe, aliyekuwa msaidizi wa karibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ni miongoni mwa Watanzania waliokimbilia Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Djumbe alisema aliamua kuondoka nchini baada ya kupokea vitisho vya maisha kupitia simu. Alidai kuwa aliambiwa alikuwa amebakiwa na siku tatu kabla ya “kutoweka.”

Baada ya nyumba yake kuvamiwa mara mbili na watu waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi, Djumbe alisema alilazimika kuvuka mpaka kwa njia zisizo rasmi usiku na kuingia Kenya.

Aliishi kwa miezi sita katika nyumba ya siri nchini humo kabla ya kurejea Tanzania akiamini hali ilikuwa imetulia. Hata hivyo, siku tatu tu baada ya kurejea, alisema alitekwa barabarani na kulazimishwa kuingia kwenye gari.

Kwa mujibu wa simulizi yake, waendesha bodaboda walioshuhudia tukio hilo walilifuatilia gari hilo, hali iliyozua taharuki na kumwezesha kutoroka. Baada ya tukio hilo, alirejea tena Kenya, ambako anaishi huku akisema bado anaishi kwa hofu ya kutekwa.

Si Watanzania pekee

Simulizi kama hiyo haisikiki kwa Watanzania pekee.

Wanaharakati kadhaa kutoka Uganda pia wameeleza kuikimbilia Kenya wakihofia kukamatwa au kushambuliwa baada ya uchaguzi wa Januari 2026 uliompa Rais Yoweri Museveni muhula mwingine wa uongozi.

Mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu kutoka Uganda, aliyefahamika kwa jina la Eriza ili kulinda usalama wake, alisema aliamua kuondoka baada ya kuona watu waliokuwa wakifanya kazi naye wakikamatwa na wengine kutoweka.

Mwanasheria mwingine wa shirika la haki za binadamu nchini Uganda naye alisema alikimbilia pwani ya Kenya baada ya kupewa taarifa kuwa alikuwa katika hatari ya kukamatwa.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, makumi ya wanaharakati kutoka Tanzania na Uganda wameingia Kenya katika miezi ya hivi karibuni wakisaka usalama.

Kwa nini Kenya?

Wachambuzi wa siasa za Afrika Mashariki wanaeleza kuwa, licha ya changamoto zake, Kenya bado ina taasisi ambazo zimeendelea kuwa na nguvu zaidi kuliko nchi nyingi jirani.

Mwanaharakati wa mtandao wa Pan-African Solidarity Network, Mwanase Ahmed, anaeleza kuwa Kenya bado ina mazingira ambayo yanatoa nafasi kubwa zaidi kwa shughuli za kiraia.

Kwa maoni yake, vyombo vya habari vya Kenya vina uhuru mkubwa zaidi wa kuripoti masuala nyeti kuliko ilivyo katika baadhi ya nchi jirani. Aidha, asasi za kiraia zina uwezo mkubwa wa kushinikiza uwajibikaji, huku mahakama zikionekana kuwa na kiwango fulani cha uhuru katika kusikiliza mashauri dhidi ya serikali.

Mbali na hilo, Nairobi ni kitovu cha mashirika mengi ya kimataifa, yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa, taasisi za haki za binadamu na balozi mbalimbali. Uwepo wa taasisi hizo huwapa wanaokimbia ukandamizaji fursa ya kupata msaada wa kisheria, kibinadamu na kidiplomasia.

Kenya pia ina jumuiya kubwa ya wahamiaji kutoka nchi za Afrika Mashariki, jambo linalorahisisha kwa wanaowasili kupata makazi ya muda na mtandao wa kuwasaidia.

Lakini Kenya nayo imeanza kutikiswa

Pamoja na sifa hizo, Kenya yenyewe imekuwa ikikabiliwa na lawama zinazohusu matukio ya utekaji.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameripoti visa kadhaa vya watu wanaodaiwa kutekwa, hasa baada ya maandamano makubwa ya mwaka 2024 dhidi ya serikali ya Rais William Ruto. Serikali ya Kenya imekuwa ikikanusha kuhusika na matukio hayo.

Zaidi ya hapo, kumekuwa na madai ya operesheni zinazovuka mipaka.

Mwaka 2024, kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizza Besigye, alikamatwa akiwa Nairobi kabla ya kurejeshwa Uganda, ambako anakabiliwa na mashtaka ya uhaini ambayo amekuwa akiyapinga.

Baadaye, mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi naye aliripoti kutekwa akiwa nchini Kenya kabla ya kuachiwa huru kufuatia shinikizo kutoka kwa wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu.

Matukio hayo yameibua wasiwasi kuhusu usalama wa wanaharakati hata wanapokuwa nje ya nchi zao.

Kwa nini bado hukimbilia Kenya?

Licha ya matukio hayo, wengi wanaamini Kenya bado ni salama zaidi kuliko mbadala uliopo.

Tofauti kubwa ni kwamba matukio yanapotokea nchini Kenya hupata uangalizi wa haraka kutoka kwa vyombo vya habari, asasi za kiraia, mawakili na jumuiya ya kimataifa.

Shinikizo hilo mara nyingi hulazimisha mamlaka kutoa maelezo au kuanzisha uchunguzi.

Kwa upande mwingine, wanaharakati wengi wanaamini kuwa katika baadhi ya nchi jirani nafasi ya kupata msaada huo ni finyu zaidi.

Hivyo, kwao, Kenya si mahali pasipo na hatari, bali ni mahali penye nafasi kubwa zaidi ya kupata ulinzi wa kisheria na uungwaji mkono wa taasisi mbalimbali.

Mustakabali wa Kenya kama kimbilio

Hata hivyo, swali linalobaki ni iwapo Kenya itaendelea kubaki kimbilio la wanaharakati ikiwa matukio ya utekaji yataendelea kuongezeka.

Wachambuzi wanaonya kuwa sifa ya Kenya kama nchi yenye nafasi ya kidemokrasia inaweza kudhoofika endapo mamlaka hazitachunguza kwa uwazi madai ya utekaji na kuhakikisha wanaohusika wanawajibishwa.

Kwa sasa, licha ya hofu inayoongezeka, Kenya bado inaendelea kuwa kituo kikuu kinachowapokea wanaharakati na wakosoaji wa serikali kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki.

Kwa wengi wao, safari ya kuelekea Kenya si kwa sababu wanaamini hakuna hatari, bali kwa sababu wanaona hatari waliyoiacha nyuma ni kubwa zaidi kuliko ile inayowakabili wanapofika Nairobi.