Lissu Atumia saa Nane Kumuhoji Shahidi wa Jamhuri, Akumbushia Kupigwa Risasi na Kukamatwa na Polisi

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ametumia takribani saa nane katika kumuhoji shahidi wa upande wa mashtaka, ACP Amin Mahamba, katika kesi ya uhaini inayomkabili, akilenga zaidi namna upelelezi ulivyofanyika, video ya Jambo TV, utambulisho wa ushahidi na tofauti kati ya maelezo ya shahidi mahakamani na yale aliyowahi kutoa polisi.
Lissu Atumia saa Nane Kumuhoji Shahidi wa Jamhuri, Akumbushia Kupigwa Risasi na Kukamatwa na Polisi
Lissu pia alitumia sehemu ya mahojiano hayo kumkumbusha shahidi kuhusu historia ya kukamatwa kwake katika vipindi mbalimbali akiwa mwanasiasa na mbunge, pamoja na tukio la kupigwa risasi mwaka 2017.
Kesi hiyo ya uhaini inahusiana na tuhuma kwamba Lissu alitoa kauli zilizolenga kuzuia au kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Penal Code.
Katika sehemu ya mwanzo ya mahojiano, Lissu alirejea tarehe 8 Aprili 2025, siku ambayo Mahamba alisema alipigiwa simu na Mkuu wake wa Kazi, Ramadhani Ng’anzi, na kupewa jukumu la kusimamia upelelezi wa jalada la uhaini linalomhusu Lissu.
Lissu alitaka kujua kama maelezo hayo yalikuwepo katika maelezo ya awali aliyoyaandika Mahamba polisi.
Lissu: “Kwenye ushahidi wako wa jana ulisema ulipofika kwa Deputy ZCO George Bagemu uliona jalada mezani ambalo lilimtaja Tundu
Antipas Lissu. Hayo maneno yapo?”
Mahamba: “Hayapo.”
Lissu aliendelea kumhoji shahidi kuhusu madai kwamba kulikuwa na mwanasheria katika timu ya upelelezi.
Mahamba alisema mwanasheria alikuwepo, lakini Lissu akamkumbusha kwamba George Bagemu, shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alisema hakukuwa na mwanasheria.
Lissu: “Bagemu amesema hakuna, wewe umesema alikuwepo. Hapa tumuamini nani, Bagemu au wewe?”Mahamba: “Alikuwepo.”
-video ya jambo tv-Sehemu nyingine ya mahojiano ilihusu video ya Jambo TV ambayo imekuwa sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo.Mahamba alisema aliangalia video hiyo kwa karibu saa mbili, huku Lissu akimkumbusha kwamba Bagemu alisema aliangalia video hiyo kwa vipande vipande.
Lissu: “Majaji wachukue ipi kati ya alivyosema Bagemu au wewe?”
Mahamba: “Mimi nimeangalia video ya masaa karibu mawili.”
Lissu pia alimuuliza Mahamba kuhusu maelezo aliyotoa kuhusu mavazi aliyokuwa amevaa kwenye video na bendera ya Tanzania iliyokuwa nyuma yake.
Lissu: “Hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako?”
Mahamba: “Hayapo.”
Lissu akaendelea na swali kuhusu hitimisho la Mahamba kwamba baada ya kuiona video hiyo aliona Lissu alidhihirisha nia ya kufanya uhaini kwa kuichapisha kwenye akaunti ya Jambo TV.
Lissu: “Haya maneno yapo?”
Mahamba: “Hayapo.”
Lissu pia aliuliza kuhusu madai ya mipango ya kuvuruga uchaguzi kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kupiga watu mawe na kufanya vurugu.
Mahamba alikubali kwamba alitoa ushahidi huo, lakini alipoulizwa kama maelezo hayo yalikuwepo katika maelezo yake ya awali, akasema:“Hayapo.”
Video haikuwasilishwa na taarifa ya kisayansi haikuwasilishwa
Lissu alimuuliza Mahamba kama video hiyo yenyewe imewasilishwa mahakamani.
Mahamba: “Sijawasilisha.”
Alipoulizwa kama amewasilisha taarifa ya uchunguzi wa kisayansi kuhusu video hiyo, Mahamba pia alisema:“Sijawasilisha.”
Hoja hiyo ilikuwa miongoni mwa maeneo ambayo Lissu alitumia kuhoji msingi wa hitimisho la upelelezi.
Hata hivyo, kumbukumbu za kesi zinaonyesha kuwa uchambuzi wa kitaalamu wa video umewahi kutajwa katika ushahidi wa mashahidi wengine wa upande wa mashtaka.
-Mashahidi wa kificho na madai ya vitisho- [7:50 PM]
Lissu pia alimuuliza Mahamba kuhusu ushahidi wake kwamba baadhi ya mashahidi waliokuwa wakilindwa kwa usiri walikuwa wametishiwa kupigwa.
Alipoulizwa kama maelezo hayo yapo katika kiapo chake, Mahamba alisema:“Haipo.”
Lissu akauliza kama kuna shahidi yeyote aliyewahi kusema aliambiwa: “Tutachoma moto nyumba yako.”Mahamba akasema hakuna.
Aliulizwa pia kama kuna aliyesema: “Tutakuua.”
Mahamba akajibu: “Hapana.”
Lissu akaweka hoja yake mbele ya Mahakama:
Lissu: “Sasa mashahidi wote wa kificho walioletwa hapa walisema hawakutishiwa kupigwa wala kuuawa. Sasa kati ya wewe na wao, Mahakama iamini ushahidi upi?”
Mahamba: “Uchukuliwe ushahidi wangu.”
Lissu pia aliingia katika maelezo binafsi ya Mahamba, akimuuliza kuhusu kazi yake, dini na makazi.
Mahamba alithibitisha kuwa ameandika kazi yake kuwa Askari Polisi na dini yake kuwa Muislamu.
Alipoulizwa kuhusu makazi yake Goba na kama Goba iko katika Halmashauri ya Ubungo, Mahamba alisema hajui kama iko huko.
Lissu pia alimuuliza kuhusu jina la mtaa aliloliandika kwenye maelezo yake, akitaja Mwakasusa, na kumuuliza kama kuna mtaa huo katika Kata ya Goba.
Mahamba akajibu: “Hakuna.”
Lissu akaendelea kuhoji mazingira ya Kielelezo D15, akimuuliza Mahamba nani aliandika maelezo hayo.
Mahamba: “Mimi mwenyewe.”
Lissu alipouliza kama hayo yalikuwa maelezo ya onyo, Mahamba akasema yalikuwa maelezo ya shahidi.
Alipoulizwa utaratibu wa kuandika maelezo ya shahidi, Mahamba alisema shahidi kwa kawaida huandikiwa maelezo na afisa wa Polisi.
-Kitengo cha polisi, PGO na majukumu ya upelelezi-
Katika sehemu nyingine, Lissu alimuuliza Mahamba kuhusu majukumu ya kitengo alichokuwa akifanyia kazi na kuhusu PGO.Mahamba alikubali kuwa kazi yake kama Polisi inahusisha kulinda raia na mali zao.
Alithibitisha pia kuwa kuna kitengo kingine cha Polisi kinachohusika na usalama wa watu.
Lissu akamuuliza kama tofauti hiyo inamaanisha kwamba kitengo kimoja kinahusika na usalama wa nchi na kingine usalama wa raia.Mahamba akajibu: “Ndiyo.”
Lissu pia aliuliza kuhusu idadi ya maafisa wa Polisi wenye jina Amin Mahamba. Mahamba alisema wapo wawili.Katika hatua hiyo Lissu aliibua suala la kuwepo kwa Amin Mahamba mwingine ambaye aliwahi kuwa RCO Singida na ambaye, kwa mujibu wa hoja iliyotolewa na Lissu, aliwahi kutuhumiwa kumfhalilisha mtuhumiwa. Mahamba hakutoa jibu lililoandikwa katika kumbukumbu zilizowasilishwa.
-Nani aliratibu upelelezi?-Lissu alimuuliza Mahamba kuhusu jukumu la DPP katika uratibu wa upelelezi wa makosa ya jinai.Mahamba alikubali kwamba DPP au mawakili wake wana jukumu hilo. Lissu akataka jina la DPP au Wakili wa Serikali aliyeratibu upelelezi wa kesi hiyo.
Mahamba alisema ni Ofisi ya DPP na kumtaja kwa maelezo kwamba anatoka Dodoma na ana majina ya Kibantu, bila kutoa jina kamili katika majibu yaliyonukuliwa.
Mahamba alieleza kuwa ana uzoefu wa miaka 26 katika kazi ya upelelezi.Lissu alimuuliza kama amewahi kupeleleza kesi ya kisiasa.Mahamba akasema: “Sijawahi kushiriki.”
Aliulizwa pia kama amewahi kushiriki upelelezi wa kesi inayomhusu Mbunge au kiongozi wa chama cha siasa.Jibu likawa: “Sijawahi.”
Hata hivyo, Mahamba alikiri kwamba amewahi kushiriki kesi ya Uchochezi iliyowahusu Freeman Mbowe na Dk Slaa.
Alipoulizwa kesi hiyo iliishaje, Mahamba alisema DPP hakuwa na nia ya kuendelea kwa sababu ushahidi haukutosha.
Lissu akauliza: “Ushahidi ulioukusanya wewe?”
Na akaunti ya jambo tvMoja ya sehemu zenye mvutano mkubwa ilikuwa madai kwamba Lissu ndiye aliyechapisha video kwenye akaunti ya Jambo TV.Mahamba alisisitiza: “Ni sahihi.”
Lakini Lissu akamuuliza kama yeye ni mfanyakazi wa Jambo TV.
Mahamba: “Sina uhakika.”
Lissu akauliza kama ni mpiga picha au mtangazaji wa Jambo TV.
Mahamba: “Sina uhakika.”
Akauliza kama Mahamba ana ushahidi kwamba Lissu alikuwa na  uwezo wa kuingia kwenye akaunti ya Jambo TV.
Mahamba: “Sina hakika.”
Lissu pia alimuuliza kuhusu mtu aliyemtaja kama P1, ambaye ni mfanyakazi wa Jambo TV na ambaye alihusishwa na kurekodi video hiyo.Mahamba alisema si kweli kwamba video hiyo ilichukuliwa na P1. Lakini alikiri kwamba amesoma maelezo ya P1. Lissu akauliza kama P1 aliandika kwamba siku hiyo walikuwa wakitishiwa matangazo kwenye YouTube ya Jambo TV.
Mahamba: “Ndiyo.”Mahamba pia alikubali kwamba kuna maelezo ya shahidi P na kwamba P1 na P walikwenda kukutana na Mkurugenzi wa Jambo TV. Lakini alipoulizwa kama yeye alikwenda kumuhoji Mkurugenzi wa Habari, akasema: “Sijafanya hivyo.”
Hotuba ya lissu na uchaguziLissu alirudi kwenye maudhui ya hotuba iliyokuwa msingi wa kesi. Mahamba alikubali kwamba hotuba hiyo ilihusu uchaguzi mkuu na matatizo yake. Pia alikubali kwamba masuala ya uchaguzi yanahusiana na Katiba.
Lissu akauliza kama Katiba inaeleza kwamba mtu anayetaka kuvuruga uchaguzi anashtakiwa kwa uhaini.
Mahamba akajibu: “Katiba haijaeleza hayo.”
Lissu akauliza kama mtu anayeshutumiwa kwa kutishia Serikali, Bunge au Mahakama kwa kuchapisha nia yake moja kwa moja anakuwa ametenda kosa la uhaini.
Mahamba akasema: “Hapana.”
Alipoulizwa kama Lissu alitishia Mahakama, Mahamba alisema: “Hapana.”
Alipoulizwa kama alitishia Bunge, jibu pia likawa: “Hapana.”
Lissu alimuuliza Mahamba kama alisoma hati ya mashtaka dhidi yakeZ Mahamba akasema alisoma. Alipoulizwa maana ya neno Serikali, Mahamba alisema: “Serikali maana yake ni mamlaka inayoongoza nchi.”
Alipoulizwa hiyo ni kwa mujibu wa nini, akasema ni kwa mujibu wa Katiba. Lissu akamuuliza kama katika shtaka lake limetajwa neno “Serikali ya Jamhuri ya Muungano”.
Mahamba akasema: “Umeyataja.”
Lissu akauliza ni chombo gani kinachosimamia uchaguzi. Mahamba akajibu: “Tume ya Uchaguzi.”
Lissu akauliza kama katika maneno yanayomkabili ametaja Tume ya Uchaguzi.
Mahamba: “Hapana.”
Mahamba pia alikubali kwamba katika mkutano huo Lissu aliikosoa vikali mfumo wa uchaguzi, ikiwemo kusema kwamba Tume ya Uchaguzi inateuliwa na Rais na kwamba inaipendelea CCM.
-Haki ya vyama kufanya mikutano-Lissu alimwuliza Mahamba kama vyama vya siasa vilivyosajiliwa, ikiwemo Chadema, vina haki ya kufanya maandamano.Mahamba akasema: “Vina haki.”
Alikubali pia kwamba vyama hivyo vina haki ya kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara.
Kuhusu mkutano wa Chadema wa Aprili 3, Mahamba alisema hakumbuki kama mkutano huo ulikuwa umepata kibali.Lissu alipomuuliza kama Chadema haiwezi kufanya mkutano wa ndani bila kibali cha Polisi, Mahamba akasema: “Mpaka wapate kibali cha Polisi.”
Alipoulizwa msingi wa kauli hiyo, akataja PGO.
Lissu akampa Mahamba PGO na kumtaka asome kifungu cha 402.
-Waandishi wa habari waliokuwepo-Mahamba alikiri kwamba siku ya mkutano huo kulikuwa na waandishi kutoka Azam TV, ITV, Mwananchi Digital, Arusha One Digital TV, Clouds TV, Chanzo TV na Jambo TV. Alisema walichukua taarifa kutoka Jambo TV.
Lissu alimuuliza kama mtu anayepata taarifa zinazohusu uhaini anatakiwa kutoa taarifa Polisi.Mahamba akasema: “Kweli.”
Alipoulizwa kama mtu anayefahamu taarifa za uhaini na asitoe taarifa Polisi anaweza kuwa ameficha uhaini, Mahamba alisema: “Sijafuatilia.”
Lissu akauliza kama kuna mwandishi yeyote aliyekuwepo wakati wa hotuba ambaye alitoa taarifa Polisi.Mahamba akasema: “Hakuna.”
Lissu pia aliuliza kuhusu watu waliosambaza video hiyo kama walikuwa wamefanya kosa la uhaini.Mahamba akajibu: “Hawakufanya.”
Kuhusu zaidi ya viongozi na wanachama 300 waliokuwa wakisikiliza hotuba hiyo, Mahamba alisema hakuwa na taarifa hiyo. Alipoulizwa kama kuna hata mmoja wao aliyekamatwa na kushtakiwa kwa kuficha uhaini, alisema: “Hakuna.”
-Nani alitoa maelekezo ya kukamatwa kwa Lissu?- Lissu pia alimuuliza Mahamba, ambaye aliiambia Mahakama kwamba alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa kesi hiyo, kama ndiye aliyetoa maelekezo ya kukamatwa kwake. Mahamba akasema: “Sikuwa mimi.”
Alipoulizwa kama maelekezo yalitolewa na Deputy ZCO George Bagemu, akasema: “Sifahamu.”
Lissu pia alimuuliza kama DCI Ramadhani Kingai ndiye aliyetoa maelekezo ya kukamatwa kwake. Mahamba akasema: “Si kweli.”
Hata hivyo, Mahamba alikubali kwamba DCI Ramadhani Kingai aliwapa maelekezo kwamba mawasiliano yangepitia kwa DCP Ramadhani Ng’anzi. Pia alikubali kwamba DCP Ng’anzi alikuwa coordinator.
Kuhusu madai kwamba Kingai alimpa Ng’anzi taarifa kuwa Lissu angekamatwa Mbinga na kuletwa Dar es Salaam, Mahamba alisema:“Sifahamu.”
-Lissu akumbushia historia ya kukamatwa na kupigwa risasi-Katika sehemu ya mwisho ya mahojiano, Lissu aligeuza maswali kuelekea historia yake ya migogoro na Jeshi la Polisi. Alimuuliza Mahamba kama anafahamu kwamba kwa karibu robo karne amekuwa akikumbana na kukamatwa na kesi mbalimbali. Mahamba alisema: “Sifahamu.”
Lissu akataja mwaka 2011, alipokuwa Mbunge, alipokamatwa baada ya kwenda kusimama na wananchi wa Tarime na Nyamongo na kupelekwa sehemu aliyotaja kuwa Uchuno, ambako baadaye alifunguliwa kesi za jinai. Mahamba: “Sifahamu.”
Lissu akaendelea kutaja tukio la mwaka 2012, aliposema alikamatwa baada ya kusimama na wananchi wa Arusha kufuatia mauaji ya watoto wao. Jibu la Mahamba likabaki: “Sifahamu.”
Lissu pia alitaja mwaka 2013 na madai ya kusimama na wananchi waliokuwa wakipigania haki ya watoto wao waliouawa katika maandamano. Mahamba: “Sifahamu.”
Lissu akaingia katika kipindi cha utawala wa Rais John Magufuli, akitaja kukamatwa kwake mwaka 2016 baada ya kusema uchaguzi uliosimamiwa na Jecha ukirudiwa ungeweza kusababisha machafuko. Mahamba alisema: “Sifahamu.”
Alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Lissu mwaka 2017 na Polisi Singida na kusafirishwa usiku hadi kupewa kesi ya uchochezi, Mahamba alisema: “Sifahamu.”
Lissu pia alimuuliza kama anafahamu kukamatwa kwake nje ya ukumbi wa Bunge mwaka huo huo baada ya kumkosoa Magufuli kuhusu namna alivyokuwa akiendesha nchi. Mahamba: “Sifahamu.”
Lissu akauliza kama Mahamba anafahamu kwamba katika kesi hizo hakuna hata moja aliyowahi kushtakiwa.Mahamba: “Sifahamu.”
Hatimaye, Lissu alimkumbusha Mahamba tukio la kupigwa risasi mwaka 2017 akiwa Dodoma, akisema alishambuliwa katikati ya Bunge na kwamba Bunge lilikataa kutoa fedha kwa ajili ya matibabu yake. Mahamba alijibu: “Sifahamu.”
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Agosti 12 saa tatu asubuhi ambapo Lissu atamalozia kumuhoji shahidi maswali ya dodoso