Lissu awataka wanachama kuichangia CHADEMA, kesi ya kikatiba yaendelea Mahakama Kuu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuendelea kuchangia chama na Baraza Kuu, wakati akiwasili katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, ambako usikilizwaji wa shauri la kikatiba namba 7300/2026 unaendelea leo.

“Changieni Baraza Kuu, changieni chama cha ukombozi,” alisema Lissu alipokuwa akiingia katika ukumbi wa mahakama.

Katika shauri hilo, mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo wanailalamikia Mamlaka ya Magereza kwa madai ya kuwazuia kuingia Gereza la Ukonga kumwona mteja wao na kutowapatia faragha ya kufanya mazungumzo naye waliporuhusiwa kuingia gerezani.

Usikilizwaji wa shauri umeendelea baada ya maswali ya dodoso dhidi ya shahidi wa kwanza, Wakili Kulwa Maduhu, kukamilika jana. Leo, pande zote zinaendelea na hatua ya maswali ya dodoso mbele ya jopo la majaji watatu linaloundwa na Jaji Amir Mruma, Jaji Dkt. Angelo Rumisha na Jaji Dkt. Evaristo Longopa.

Tofauti na siku zilizopita, Lissu hakuketi ndani ya kizimba wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo. Badala yake, alitengewa kiti na meza ndani ya ukumbi wa mahakama kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama jana kwamba, kwa kuwa shauri linalosikilizwa ni la kikatiba na si la jinai, hakuna sababu ya yeye kukaa kizimbani wakati wa mwenendo wa kesi.