, ,

Lissu: Kesi Ya Uhaini Ilitengenezwa Na Mtu Mmoja

Wadh Kassim Avatar

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, ameendelea na uwasilishaji wa hoja zake za mwisho katika kesi ya uhaini inayomkabili, ikiwa ni siku ya nne tangu aanze hatua hiyo Septemba 23, 2026.

Katika hoja zake, Lissu amedai kuwa kuna mashaka makubwa kuhusu namna kesi hiyo ilivyoanzishwa, akisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonyesha kuwa kesi hiyo “imetengenezwa na mtu mmoja au pengine watu wawili.”

Lissu amemlenga shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, George Bagemu, akisema ndiye aliyeamua kwamba maneno yanayolalamikiwa katika kesi hiyo yanatengeneza kosa la uhaini.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kuwa Aprili 3, 2025, alitamka na kuchapisha mtandaoni maneno yaliyotafsiriwa kuwa “tutazuia uchaguzi,” “tutahamasisha uasi” na “tutavuruga uchaguzi,” kwa madai kwamba yalilenga kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuitishia Serikali.

Lissu anakiri kutamka maneno hayo, lakini anapinga tafsiri kwamba maneno hayo yanaunda kosa la jinai la uhaini.

Alikamatwa jioni ya Aprili 9, 2025, mjini Mbinga mkoani Ruvuma, baada ya kuhutubia mkutano wa Chadema, na siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka, likiwamo shtaka la uhaini.

Katika hoja zake za mwisho, Lissu amesema Bagemu alichukua hatua ya kuamuru kufunguliwa kwa jalada la uhaini siku nne baada ya kuonyeshwa video, bila kuomba mwongozo kutoka kwa baadhi ya wakubwa wake wa kazi.

Amesema ushahidi wa Bagemu unaonyesha kuwa hakumjulisha ZPC wala DCI Ramadhani Kingai kabla ya kufungua jalada hilo, huku pia akidai hakutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kuhusu hatua hiyo.

Lissu ameunganisha hoja hiyo na mkanganyiko anaodai kuwepo katika ushahidi wa Bagemu na shahidi wa 16 wa upande wa mashtaka, Assistance Insepector Amini Mahamba, kuhusu uwepo wa mwanasheria katika timu ya upelelezi.

Kwa mujibu wa Lissu, Bagemu alisema timu ya upelelezi haikuwa na mwanasheria, wakati Mahamba alidai kuwa kulikuwa na afisa mwanasheria, lakini hakutaja jina lake wala mwanasheria huyo hakufika mahakamani kutoa ushahidi.

Lissu amesema tofauti hizo zinaongeza mashaka kuhusu namna kesi hiyo ilivyoandaliwa na uaminifu wa baadhi ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Ameendelea kuieleza mahakama kuwa katika maswali saba aliyoiweka mbele yake, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango cha uthibitisho kinachotakiwa katika kesi za jinai, ikiwamo hoja kama yeye ndiye aliyeandaa mkutano, aliwaalika waandishi wa habari, alikusudia kuchochea umma kuzuia uchaguzi, na kama Serikali ilitishika kutokana na maneno hayo.

Hoja za mwisho za Lissu zinaendelea leo mbele ya Mahakama Kuu, baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake na kuhamia hatua ya mwisho ya kuwasilisha hoja za kisheria na ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo.

Kesi inaendelea

Our Correspondent Avatar