Msigwa:Uchunguzi bado unaendelea kuhusu kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda

Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa eneo la Kibiti mkoani Pwani ambako ndio kituo chake cha kazi.

0
Azory Gwanda

Msemaji Mkuu wa Serikali nchini Tanzania, Gerson Msigwa, amesema Jeshi la Polisi nchini humo, linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio la kupotea kwa aliyekuwa Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda.Mwandishi huyo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa eneo la Kibiti mkoani Pwani ambako ndio kituo chake cha kazi.

Oktoba 17, Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa kupitia mkutano wa wanahabari jijini Mwanza alijikuta anajibu swali aliloulizwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari mkoani Mwanza, Edwin Soko, aliyetaka seriakali itoe taarifa za wapi alipo Azory au kutoa uchunguzi wa tukio la kupotea kwake kwani tukio hilo linaleta taswira mbaya nchini.

Msigwa alisema kwamba bado jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na ukikamilika litatoa ripoti ya uchunguzi wa tukio hilo.

 “Polisi wameshatoa taarifa na wanaendelea kufanya uchunguzi, sababu Polisi wanajukumu kufanya uchunguzi na hawafanyi kwa Azory peke yake, wanafanya kwa watu wote wanaopata madhila kama hayo ya kupotea, kufariki dunia na matatizo yote.”amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa kwa sasa ni kuliachia jeshi la polisi lifanye kazi yake.

“Ninachoomba tuendelee kuwasikiliza Polisi, watatuambia nini juu ya hatma ya wanayoendelea kufanya ya kulichunguza jambo hili na baadae watatuambia uchunguzi wao utakapokamilika, nini wamekiona na tutajua cha kufanya. Lakini sasa hivi hakuna ripoti imeandaliwa maalum ya Azory zaidi ya uchunguzi unaofanywa na Polisi,” amesema Msigwa.

Tangu kupotea kwake polisi nchini Tanzania mara kadhaa imesikika ikisema kwamba uchunguzi bado unaendelea.

Azory Gwanda ambaye alikuwa akifanya kazi na kampuni ya magazeti ya Mwananchi nchini Tanzania, ni mmoja ya waandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauwaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji wa Kibiti mkoani Pwani.

Kupotea kwa mwandishi huyo kunahushishwa na kufuatilia kwake yaliyokuwa yakiendelea hasa madai kwamba vyombo vya usalama vilikuwa vikitekeleza vitendo vya unyanyasaji dhidi ya raia katika juhudi za kudhibiti matukio ya mauaji kwenye mji huo

Alitoweka tarehe 21 Novemba 2017, ambapo hadi sasa ni takribani miaka 4.Mke wa Azory, Anna Pinoni aliviambia vyombo vya habari kuwa siku ya tukio aliwaona watu wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser walimchukua mume wake na kisha  kutoka katikati ya mji huo, na kwenda naye nyumbani kabla ya baadae kutoweka hadi sasa.

Kampeni kadhaa zimeanzishwa kutaka maelezo juu ya kupotea kwa Azory, lakini hakuna hadi sasa majibu yaliyopo kwa vyombo vya upelelezi na mamlaka husika ni kwamba uchunguzi bado unaendelea.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted